Vipimo vya Corona Kutolewa Ndani ya Saa 24
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi, ameuagiza uongozi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, kutoa majibu ya sampuli za ugonjwa wa COVID-19 ndani ya saa 24, badala ya saa 72 kwa hospitali zinazopeleka sampuli hizo au kwa wananchi wanaojitokeza kupima kwa ajili ya kusafiri.
Mganga Mkuu wa Serikali ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na uongozi wa maabara hiyo, waganga wakuu na wasimamizi wa maabara kutoka hospitali za rufaa za serikali na za binafsi, kutoka mkoa wa Dar es Salaam.
Prof. Makubi amesema pamoja na kuweka mifumo mizuri katika maabara hiyo lakini bado kumekuwepo na malalamiko wanayapokea kutoka kwenye baadhi ya hospitali na hata kwa wasafiri wanaofika katika maabara hiyo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo, ucheleweshaji ambao umekuwa kero kwa wananchi hao na kamwe hautaweza kuvumiliwa.
"Tafuteni njia mtakayofanya ila hakikisheni kuanzia sasa majibu yote ya COVID-19 yanatolewa ndani ya saa 24 kwa wale wote watakaofanyiwa vipimo kwa Dar es Salam na masaa 48 kwa mikoani, na lazima suala hili lisimamiwe na wasimamizi wote wa maabara zinazohusika ili kuhakikisha kero hii inaondolewa", amesema Prof. Makubi .
"Aidha mfumo wa kufuatilia vipimo na majibu kati ya maabara kuu na hospitali lazima uboreshwe na kufanyiwa tathimini kila wakati na kila msimamizi atimize wajibu wake bila kuchelewesha", ameongeza.
Katika hatua nyingine Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi, ameshangazwa na kitendo cha kupotea kwa baadhi ya sampuli za COVID-19 ambazo zimekuwa zikifikishwa katika maabara hiyo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.
"Kwa hili la kupotea kwa sampuli kwa kweli haliwezi kuvumilika, naelekeza kwa sasa hivi nisisikie tena kuna sampuli yoyote ambayo imepotea, si vyema katika mfumo wa maabara kupoteza kwa sampuli, iwe mwiko kupotea kwa sampuli yoyote ndani ya Maabara Kuu ya Taifa na maabara zote nchini” amesema Prof. Makubi.
No comments