Kocha Mkuu Namungo Afutwa Kazi
IMEELEZWA kuwa Hitimana Thiery amefutwa kazi ndani ya Klabu ya Namungo FC inayotumia Uwanja wa Majaliwa kwa mechi zake za nyumbani. Kocha huyo ambaye alikipandisha kikosi hicho Ligi Kuu Bara na msimu wake wa kwanza ndani ya ligi aliweza kumaliza ndani ya tano bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Ikiwa imecheza jumla ya mechi 38 msimu wa 2019/20 ilishinda mechi 17, sare 13 na ilipoteza mechi nane huku ikikusanya jumla ya pointi 64. Msimu huu ikiwa inaiwakilisha nchi kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ipo nafasi ya tisa na pointi zake ni 14 baada ya kucheza mechi 10 jambo ambalo limewafanya viongozi wa Namungo kuamua kumfuta kazi.
Kibarua chake cha kwanza kimataifa kwa Namungo ni kati ya Novemba 27-29 ambapo itacheza na Al Rabita ya Sudan Kusini Uwanja wa Azam Complex. Habari zinaeleza kuwa nafasi yake imechukuliwa na Hemed Morocco ambaye alikuwa Kocha Mkuu wa Mbao msimu uliopita kabla ya kubwaga manyanga.
No comments