Watanzania Waliokamatwa Kenya Kwa Kosa la Kutokuvaa Barakoa Waachiwa
Moshi. Watanzania wanne waliokuwa wakishikiliwa Kenya kwa kosa la kuingia nchini humo bila kibali na kuacha kuvaa barakoa wameachiliwa huru baada ya kulipa faini ya Sh2.8 milioni sawa na (Ksh140).
Wafanyabiashara hao wanne ambao ni wakazi wa Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi walikamatwa Novemba 11, baada ya kuvuka mpaka kupitia Kitobo ambako sio eneo rasmi wakati walipokwenda kununua nyanya.
Akizungumza na gazeti la Mwananchi jana, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Edward Mwenda aliwataja wafanyabiashara hao kuwa ni Wilfred Moshi, Shaban Rajab, Witness Omary na Fatuma Msangi.
“Wafanyabiashara hawa ambao ni wakazi wa Himo, Wilaya ya Moshi, Novemba 11 mwaka huu walikamatwa Kenya kwa kosa la kuingia nchini humo kinyemela; walikamatwa na kutozwa faini ya Sh700,000 kwa kila mmoja; lakini mmoja pekee ndio alifanikiwa kulipa faini hiyo juzi,” alisema Mwenda.
Pia, alisema mpaka kufikia jana wafanyabiashara wengine watatu walifanikiwa kulipa faini hizo Sh2.1milioni,wote waliachiwa huru na kusema baadhi ya waliocha mali zao huko zinafuatiliwa ili waweze kuzipata.
“Mpaka jana tayari wafanyabiashara wote wanne wamefanikiwa kulipa faini zote, hivyo wameachiwa huru na muda huu wamepita mpakani Holili kurejea Tanzania,” alisema Kamishna Mwenda.
Pia, aliwaasa wafanyabiashara na wananchi kuacha tabia ya kuvunja sheria zilizowekwa na mamlaka na kusema kuwa endapo sheria hizo zikivunjwa hatua kali dhidi yao zinachukuliwa ikiwemo kupigwa faini.
“Sheria zetu zinasema ni kosa kupitia njia ambazo sio rasmi na zinasema kwa uwazi kabisa kwamba atakayevunja sheria hizo anachukuliwa hatua kali, kwa mfano ukitaka kwenda Kenya kama huendi zaidi ya kilomita 10 unaruhusiwa kupita mpakani kwa sababu ya ujirani mwema lakini ukipita njia za panya na ukakamtwa lazima upelekwe mahakamani,”alisema
No comments