Header Ads

Header ADS

Wolper: Nimetukanwa Sana, Namwachia Mungu




DAR: Wiki iliyopita kwenye mitandao ya kijamii, kuliibuka tafrani kubwa baada ya staa wa sinema za Kibongo, Jacqueline Wolper Masawe kuvishwa pete ya uchumba na mbunifu wa mavazi, Rashid Juma ‘Chid Designs’, lakini uchumba ukavunjika hata kabla ya kumaliza wiki moja.

 

Kufuatia sarakasi hiyo, Wolper amesema; “Nimetukanwa sana, lakini ninamwachia Mungu!”

Katika mahojiano maalum (exclusive) na Gazeti la IJUMAA, Wolper alisema kwa uchungu kuwa, katika maisha yake hajawahi kuachwa, hivyo aliumia mno.

 

Alisema yeye siyo mwanamke wa kufanyiwa kiki kama watu wanavyosema.

Wolper alifunguka kuwa, hakuna kitu kilichomuuma kama kusambaa kwa taarifa zake za uongo kwenye mitandao na kutafsiriwa ndivyo sivyo.

 

Alisema kama watu wangejua ukweli wa mambo, wasingeweza kusema wanavyosema.

“Unajua watu wanaweza kuongea mambo mengi sana bila kujua undani wake, lakini kama Mungu angewafunua na kujua ukweli, nafikiri wasingefungua mdomo hata kidogo.

 

“Watu wanapaswa wakumbuke mimi sijaachwa, bali nimeacha, nataka wafahamu hilo kwanza,” alisema Wolper kwa uchungu.

Mwigizaji huyo aliongeza kuwa, watu wengi wamemchafua mno kwa kumuongelea vibaya, lakini kamwe hawezi kufungua mdomo wake kuwajibu, badala yake atamuachia kazi hiyo Mungu.

 

“Fikiria nipo kwenye msiba wa mtu niliyempenda, bibi yangu kipenzi, halafu mtu anakuletea picha za tofauti kabisa, mimi nilishasema sitaki kubishana nao. Mungu atashughulika nao,” alisema Wolper.

 

Staa huyo aliongeza kuwa, hataki tena kuzungumza chochote kuhusiana na pete aliyopigiwa changa la macho kwa sababu hahitaji tena kufanya hivyo.

Alisema kama ni kusemwa na kutukanwa, amefanyiwa hivyo sana, lakini anamwachia Mungu.

 

“Sina muda wa kuzungumza chochote kuhusiana na kitu kilichokea na wala sitazungumza tena, leo ni mwisho kwani imetosha kwangu. Nimechafuliwa sana,” alisema Wolper ambaye Chid ni mwanaume wa nne kumchumbia kisha kumwacha solemba.




No comments

Powered by Blogger.