Header Ads

Header ADS

Esma: Ndoa Yangu Inawaka Moto!




ESMA Khan almaarufu kama Esma Platnumz, ni dada wa supastaa wa Bongo Fleva, Afro- Pop na Afro-Beat, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

Esma amejizolea ustaa kupitia mgongo wa Diamond kutokana na tabia yake ya kuingilia uhusiano wa kimapenzi wa kaka yake huyo.

 

Kutokana na ishu hiyo, Esma ambaye ni maarufu kwenye mitandao ya kijamii (sosholaiti), amepachikwa jina la Yuda Msaliti au Yuda Iskariote kutokana na kuonesha usaliti kwa wapenzi wa kaka yake. Anafananishwa na yule Yuda aliyemsaliti Yesu, akasulubiwa na kufa msalabani.

 

Esma ambaye alikuwa mke wa ndoa wa meneja wa wasanii wa Bongo Fleva, Hamad Manungwi ‘Petit Man’ kabla ya kutengana na kurudiana kisha kuachana tena, anasema anawashangaa watu wanaomtuhumu kila kukicha kuhusiana na uhusiano wa kaka yake na wachumba zake kwa sababu hata yeye ana majanga kwenye ndoa yake.

 

Kwenye mahojiano maalum (exclusive) na Gazeti la IJUMAA, Esma ambaye pia ni mwanamke mjasiriamali, anafunguka mambo mengi yanayoendelea kwenye ndoa yake na familia yao kwa ujumla;

 

IJUMAA: Esma maisha yanaendaje kwa sasa katika kipindi hiki ambacho upo singo?

ESMA: Maisha ya usingo nimeyazoea kabisa. Kikubwa Mungu anajaalia maisha yanaendelea vizuri na baraka zinaendelea kumiminika.

 

IJUMAA: Kwa nini kunakuwa na migogoro kati yako na Petit kila mara maana mlishaachana zaidi ya mara tatu na kurudiana?

ESMA: Hata mimi kwa kweli sijui ni nini kwa sababu unajua kuna wakati Mungu hapendi upite njia unayopita, matokeo yake ukilazimisha, ndiyo inakuwa hivyo.

 

IJUMAA: Kwa kuwa ni kawaida ninyi kugombana na kurudiana, mnaweza kurudiana siku za usoni?

ESMA: Sidhani na wala sifikirii. Kwanza nimeshazoea maisha ya usingo, hakuna mtu wa kunigasi.

 

IJUMAA: Najua mna mtoto ambaye anapenda kuwaona wazazi wake pamoja, inakuwaje sasa kwa upande wenu?

ESMA: Mtoto hana shida, baba yake akimuhitaji anamchukua wakati wowote na ni rafiki wa wote.

 

IJUMAA: Lakini huoni kama kutengana kwenu kila mara mnamjengea mtoto taswira mbaya kwenye maisha yenu?

ESMA: Naelewa, lakini ni kitu ambacho kinatokea tu ‘automatic’ hata sisi wenyewe hatupendi.

 

IJUMAA: Najua una watoto wawili, je, unawalea katika malezi ya aina gani?

ESMA: Wanangu ninawalea kawaida sana, lakini kikubwa ninawalea kwenye maadili ya dini (Uislam).

 

IJUMAA: Ukisema maadili ya dini, una maanisha nini?

ESMA: Yaani wajue kuwa wanatakiwa kumjua Mungu zaidi, kama kwenda chuo na kujua vizuri na kusoma kwa ufasaha Qur’an tukufu.

 

IJUMAA: Watoto wako wamezaliwa kwenye familia ya staa (Diamond), je, malezi yao ni tofauti na watoto wengine?

ESMA: Hapana, watoto wangu wote kwa kweli wanaishi maisha ya kawaida sana kama ilivyo kwa wengine na ninapenda hivyo kwa sababu hata mimi nililelewa maisha ya kawaida sana.

 

IJUMAA: Najua sasa hivi unaishi mwenyewe baada ya kutengana na Petit, unawezaje kulea ukiwa peke yako?

ESMA: Kwa kweli Mungu amenijaalia kutafuta pesa kwa nguvu zote na ninafanya hayo kwa ajili ya wanangu, nachakarika kila kukicha ili tu wasome vizuri na wawe na maisha bora. Kwa hilo halinisumbui, labda tu watoto wawamisi baba zao.

 

IJUMAA: Kila mara watu wamekuwa wakikutuhumu kuwa huwa unachochea uhusiano wa kaka yako kuvunjika kiasi cha kupewa jina la Yuda, hili limekaaje?

 

ESMA: Kwanza, watu watambue kuwa mimi sihangaiki na uhusiano wa mtu kwa sababu ndoa yangu mwenyewe inawaka moto, halafu wanafikiri wakiniita Yuda nitabadilika kuwa Petro? Haiwezekani.

 

IJUMAA: Mwanzoni ulikuwa ukimsifia mno Tanasha na kusema kuwa ndiye mwanamke anayemfaa Diamond, lakini tunashangaa ukaanza tena kumponda mara tu alipoachana na kaka yako, nini mtazamo wako?

 

ESMA: Kama nilimsifia ujue alikuwa akifanya jambo jema, lakini kama alivurunda ndiyo maana nikasema hivyo.

IJUMAA: Kuna tetesi kuwa Zari anarudi Madale, hili lina ukweli kiasi gani?

 

ESMA: Zari ni mwanamke ambaye ana watoto wetu wawili, hata akija Madale anawaleta watoto nyumbani kwao. Kuhusu kurudiana na Nasibu (Diamond), yeye akiamua sisi hatupingi.




No comments

Powered by Blogger.