Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima Aipongeza Halmashauri Ya Bunda Kwa Hati Safi
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Mkuu wa Mkoa wa Mara ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kupata hati safi kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa uwasilishaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Selikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019, Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima aliipongeza Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kupata hati safi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017, 2017/2018 na 2018/2019.
“Halmashauri hii ni ya mfano katika mkoa wa Mara na ninawaomba msibweteke kwa vile mmepata mafanikio haya, bali muongeze bidii” alisema mkuu wa mkoa Malima
Aidha, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali katika mkoa wa Mara, Patrick Lugisi alisema kuwa mafanikio hayo ni matokeo mazuri ya kazi wanayofanya watumishi wa Halmashauri ya mji wa Bunda.
“Ushirikiano na uwajibikaji wa Menejimenti ndio umepelekea Halmashauri hii kuwa na hoja chache na kuwa na ufanisi, niziombe Halmashauri zingine kuiga mfano huu” alisema Lugisi.
Halmashauri ya mji wa Bunda ilianzishwa Mwaka 2015 na ilianza kutekeleza majukumu yake Mwaka 2016. Hati safi kwa halmashauri hii imekuwa chachu ya kuongeza tija kwa watendaji wote na hivyo kuwawezesha wananchi kunufaika na huduma bora zinazotolewa katika sekta za afya, elimu, maji,miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Mwisho
No comments