Makala: Haile Selassie, ‘Masiha’ Aliyeuawa na Kutupwa Chooni, Kutukuzwa na Kupingwa
Machi Mosi 1896, Kibanga alimshushia mkoloni kipigo cha mbwa koko katika ardhi ya Ethiopia. Majeshi ya Dola ya Italia yaliyojaa uroho wa kujimilikisha rasilimali za Ethiopia yalipata tabu sana mbele ya vikosi vya jeshi la Mfalme Menelik II. Yaliwekwa kati ya milima ya Mji wa Adwa, yakatepeteshwa na kuchakazwa kwa mbinu za kijeshi ambazo hawakutegemea kuziona kwa majeshi ya watu weusi.
Masikini mabeberu wale walijuta kujaribu kuivamia ardhi Takatifu ya Afrika, inayoaminika pia kuwa ndiyo Israel ya Afrika. Ilikuwa ni kilio na kusaga meno. Wamakonde wanasema, ‘wakikimbia nchale, wakisimama nchale.’ Waitaliano wakaisoma namba…! Kikosi cha Italia chenye wanajeshi 20,000 na silaha za kisasa, kilichoongozwa na Jenerali Baratier, mzoefu wa vita ya ardhini, kilizungukwa na wanajeshi 100,000 wa Ethiopia wakiwemo wanawake waliofanya kazi kubwa ya kugawa chakula na maji kwa wapiganaji. Wanajeshi wa Italia waliuawa kikatili sana, haikuwahi kutokea.
Taarifa ya kipigo hicho ilipofika Italia iliwashtua watawala. Warumi walitaka kujua nani aliongoza kikosi cha Mfalme Menelik II. Kwa dharau ya wazungu wa enzi hizo waliamini hawezi kuwa mtu mweusi. Lakini ukweli ulikuwa wazi, ni Mkuu wa Majeshi ya Ethiopia aliyeingia vitani siku hiyo, mwenye ngozi ngumu nyeusi, Ras Makonnen Woldemikael.
Huyu ndiye aliyepewa heshima ya kuwa ‘Shujaa wa pambano hilo katika mji wa Adwa Maarufu kama Battle of Adwa.
Hata hivyo, Waswahili husema, ‘mwenye kisasi hafi mara moja’. Masikini Ras Makonnen hakujua kisasi na chuki za kipigo alichotoa siku hiyo kingemuangukia mwanaye mpendwa, Lij Tafari ambaye miaka kadhaa baadaye alikuwa Mfalme aliyebatizwa jina ‘Haile Selassie’, aliyetukuzwa na hata kuabudiwa. Aliitwa Mfalme wa Wafalme, Simba wa Yuda, Messiah/Masiha (Mkombozi) na ‘Nguvu ya Utatu Mtakatifu’. Ni Mfalme Haile Selassie ambaye jamii ya Rastafari inasadiki kuwa alitajwa kwenye kitabu cha Ufunuo cha Biblia Takatifu; lakini aliyapitia mengi kabla ya kuuawa na kutupwa chooni.
Ifuatilie makala hii hadi mwisho tuzipitie kurasa za historia ya Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia aliyetawala kati ya Aprili 2, 1930 – Septemba 12, 1974 katika ardhi takatifu inayoaminika kuwa ishara ya uhuru wa bara la Afrika kwa kuwa haikutawaliwa na wakoloni, sawa na Liberia.
Siku zote embe haliunguki mbali na muembe, Julai 23, 1892 jemedajari na mkuu wa majeshi ya Ethiopia, Ras Makonnen, shujaa wa ‘Battle of Adwa’ alizaa jembe aliloliita Lij Tafari ambalo liliibuka kuwa tufani la Afrika lililotikisa dunia ya mabeberu.
Jina la mtoto huweza kuwa baraka au laana na mikosi kwenye maisha yake, ndio sababu kwenye vitabu vitakatifu vya Mungu, Mungu mwenyewe alikuwa akiwaita watu majina au kuwabadili majina yao pale alipotaka kuwabariki zaidi. Ukimuita mwanao ‘Shida’, ‘Mateso’, ‘Chuki’ unadhani atakuwaje? Nakumbuka ndugu yetu mmoja alikuwa anaitwa Chuki, mwaka 2000 alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kukutwa na hatia ya kuua kisa chuki. Kwa bahati, aliachiwa kwa msamaha wa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2012.
Jina Lij Tafari lilikuwa na maana nzito, Lij (mtoto mwenye damu ya kifalme) na Tafari mtu anayeheshimiwa na kuogopwa.
Aliipata damu ya kifalme, kwa kuwa alikuwa mwanafamilia wa Ufalme unaoaminika kuwa ni Ufalme wa Suleiman yule wa kwenye Biblia, uliopitia kwa Mfalme Menelik wa Kwanza. Ni kitukuu cha Mfalme Sahle Selassie. Babu yake, Woldemikael alizaliwa na binti wa Mfalme Sahle Selassie. Mama yake mzazi alikuwa binti wa kiongozi mkuu wa eneo la Bete Amhara aliyefahamika kama Ras Ali. Kwa taarifa yako tu, Ras sio nywele ndefu zilizojisokota kama wengi wanavyooamini. Ni cheo, maana yake ‘Mkuu’. Hivyo, alipata nafasi ya kuishi kwenye himaya ya kifalme na kutazamwa kama damu ya kifalme.
Tangu akiwa mdogo, aliwashangaza wengi kwa uwezo mkubwa wa kung’amua mambo. Hekima, busara na hoja zilimfanya kutazamwa kwa jicho la tatu. Wengine waliamini ni ‘genius’. Hilo lilimfanya kuanza kukabidhiwa vijiti vya madaraka ya awali katika ngazi mbalimbali, hadi akaitwa Ras Tafari.
Hatimaye, mwaka 1930, baada ya kifo cha Zauditu aliyekuwa kiongozi wa Ethiopia na binti wa Mfalme Menelik wa Pili, Ras Tafari alitawazwa rasmi kuwa Mfalme wa Ethiopia. Alipewa jina la kiutawala la ‘Mfalme Haile Selassie I’. Jina hilo lilikuwa na maana kubwa, Haile (Nguvu) na Selassie (Utatu Mtakatifu). Hivyo, maana yake ni ‘Nguvu ya Utatu Mtakatifu’.
Kutokana na kuvuma kwa jina lake duniani, sherehe za kuapishwa kwake zilivunja rekodi. Viongozi lukuki walihudhuria sherehe hizo, wengine wakienda kushuhudia jeuri ya taifa hilo la Afrika iliyoyashinda mabavu ya wakoloni.
Kwa mara ya kwanza katika historia, Jarida la Marekani la ‘Time Magazine’ lilitumia picha ya Mfalme huyo mpya wa Ethiopia kwenye jarada lake ikieleza kuwa sherehe zake tu za kuapishwa ziligharimu takribani $3 Milioni. Ilikuwa rekodi nzito ya dunia. Kuvuma kwa jina lake kulitokana na namna alivyofanikiwa kujijengea umaarufu akiwa kama kiongozi wa kawaida, akiwa kama Ras (mkuu) Tafari. Mwaka 1924, alipata nafasi ya kutembelea Ulaya na kukutana na viongozi waandamizi wa nchi hizo ambao walishangazwa na uwezo wao. Alitembelea pia Misri na Israel na huko aliacha alama.
Mfalme Haile Selassie aliianza kazi yake kwa kasi ya mabadiliko. Punde, utawala wake ulifanikisha kuandika Katiba ya kwanza ya taifa hilo. Alitenga mhimili wa Bunge na Serikali na kuanza harakati za kuhubiri umoja, amani na mshikamano. Hata ndani ya Afrika, aliongeza nguvu kubwa kwenye uhuishaji wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU). Juhudi hizo zilizaa matunda, ambapo Mei 25 mwaka 1963, Umoja huo ulizaliwa rasmi na mkutano wake wa kwanza ulifanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Rais wa kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pia alihudhuria na kuwa mgeni wa Mfalme Haile Selassie I.
Wakuu wa nchi za Afrika, waanzilishi wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) wakiwa Addis Ababa baada ya mkutano wao wa kwanza kati ya Mei 22-25, 1963
Hata hivyo, kwa Jamaica jina la Haile Selassie halikuwa jina la mtawala wa kawaida. Kwao alikuwa mtu muhimu aliyetabiriwa na manabii pamoja na vitabu vya Mungu hasa Kitabu cha Ufunuo cha Biblia, kuwa ndiye Messiah (Mkombozi) wa dunia. Kwa Wakristo wao huamini Messiah ni Yesu. Pia, Rastafari waliamini kuwa Israel inayotajwa ilipaswa kuwa Ethiopia. Kuna maelezo mengi ya hoja nzito zinazojengwa kuhusu imani hii. Leo tusiingie huko.
Imani hiyo kwa Mfalme Haile Selassie, ilizaliwa kutoka kwenye unabii wa mwanaharakati na Mwanafalsafa wa Jamaica aliyeheshimika sana, Marcus Garvey.
“Iangalieni Afrika, sehemu ambayo Mfalme atasimikwa, kwa sababu ukombozi umekaribia,” alisema Marcus Garvey mwaka 1924. Unabii huo ulikoreza imani ya dini ya Rastafari au Rastafarianism ambayo ilikuwa imechipua nchini Jamaica hususan katika eneo la Kingston.
Waamini wa imani ya Rastafari pamoja na wafuasi karibu wote wa Marcus Garvey waliamini kusimikwa kwa Haile Selassie ni ishara ya kutimia kwa unabii huo. Pia, waliamini ni muda wa kurejea barani Afrika hususa katika ardhi takatifu ya Ethiopia. Kwa wafuatiliaji wa historia mtakumbuka harakati zilizoanzishwa na Marcus Garvey na wenzake za kulikomboa bara la Afrika kwa kurejea barani Afrika zilizoitwa ‘Back to Africa Movement’ katika miaka ya 1920. Baadhi yao walifanikiwa kurejea Afrika kwa njia ya melikebu.
Cha ajabu, ingawa Marcus Garvey hakuwahi kuwa muumini wa imani ya Rastafarian/Rastafari, waumini wa imani hiyo wao wanamchukulia kama nabii wao na unabii wake waliuamini na kuufanyia kazi. Falsafa zake zimetumika katika kuunda imani hiyo. Mshangao huo pia utaupata kwa Mfalme Haile Selassie mwenyewe ambaye wao wanaamini ndiye Messiah wao, ingawa katika maisha yake yote yeye alikuwa muumini wa dini ya Kikristo aliyesali katika makanisa ya Orthodox.
Mfalme Haile Selassie I apigwa, akimbia:
Kuinuliwa kwa Mfalme Haile Selassie, kuliziamsha hasira za kisasi cha Italia. “Si huyu ndiye mwana wa yule Ras Makonnen, Jenerali aliyetupiga kwenye ‘Battle of Adwa’?” Jibu la swali hili liliyainua masikio ya Dikteta Mbabe, Benito Mussolini. Mwaka 1935, ikiwa ni miaka mitano tu tangu kutawazwa kwa Haile Selassie, Mussolini aliamua kulipa kisasi cha nchi yake dhidi ya damu ya adui yake. Alipeleka vikosi vyenye silaha nzito kumshughulikia Mfalme Haile Selassie.
Ilikuwa piga ni kupige kati ya vikosi vya Mfalme Haile Selassie na vile vya Dikteta Mussolini. Wakati huu, kipigo kilimzidi Haile Selassie na aliamua kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza kukwepa kunyongwa. Wahenga husema, “kuanza upya sio ujinga.”
Huu ulikuwa mwaka mbaya kwa Haile Selassie, akiwa na maumivu, alizipata kejeli na kukosolewa vikali na baadhi ya waliomsifu sana mwanzo. “Pata shida uwajue marafiki na maadui.”
Yule nabii aliyemtabiri awali kuwa ndiye Mfalme atakayesimikwa Afrika kama ishara ya ukombozi, Marcus Garvey alimgeuka. Alimkosoa vikali kwa hatua yake ya kukimbilia ughaibuni. Alisema hafai kuwa kiongozi, akijenga hoja kuwa amewatelekeza watu wake na kukimbia kulinusuru shingo lake na familia yake.
Imani bwana! Waliomshangilia Yesu Mnazareti akipita juu ya punda pale Yerusalem, itakuwa ni walewale waliopaza sauti za ‘asulubiwe’. Wakati huu, wale waumini wa Rastafari nao walimgeuka kabisa nabii wao Marcus Garvey alipomkosoa Messiah wao, Haile Selassie. Sijui waliamini amepandwa na pepo au amekula maharage ya wapi! Wao waliendelea kumuombea mema kwa Jah (Mungu) wakiamini kweli ukombozi unakaribia.
Ni kama maombi ya Rastafari yalimfikia Jah. Haile Selassie alizicheza kete zake vizuri akiwa Uingereza na nchi nyingine za Ulaya. Aliwatafuta maadui wa Mussolini wenye nguvu na kuwaomba wamsaidie. Aliamini “adui wa adui yako ni rafiki yako, chuma hufua chuma, beberu hung’oa beberu,.”
Hatimaye, Mfalme Haile Selassie alipewa nafasi ya kuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa (League of Nation) uliofanyika jijini Geneva nchini Uswizi. Hotuba iliyokuwa maarufu sana na kufanikisha ushawishi wake. Iliitwa ‘kurejesha ardhi iliyopokonywa na wavamizi’.
Mwaka 1941, Vikosi vya jeshi la Uingereza kwa kushirikiana na Afrika Kusini vilifanikiwa kuung’oa utawala wa Italia nchini Ethiopia. Mfalme Haile Selassie alirejea rasmi nyumbani na kupata mapokezi ya aina yake, “Shujaa amerudi.”
Haile Selassie aitembelea Jamaca, ‘Messiah uso kwa uso na waumini wake’
Baada ya kuweka mambo sawa na kurejesha jina lake kileleni tena kama kiongozi pendwa wa Ethiopia, Aprili 21, 1966 ‘Simba wa Yuda’ aliitikia wito na kuitembelea Jamaica. Wakati huo, yule nabii aliyetabiri kuja kwake na baadaye akageuka kuwa mkosoaji wake mkuu, Marcus Garvey alikuwa ameshafariki dunia. Jamii ya Rastafarian iliyokuwa na watu wengi nchini Jamaica na sehemu kadhaa duniani ni kama iliuzika pia ukosoaji wa Garvey. Hivyo, Selassie aliingia Kingston Jamaica akiwa Messiah asiye na mkosoaji mwenye nguvu.
Mapokezi yalimshangaza Haile Selassie. Kila mmoja alitaka kumuona mkombozi wao. Wachambuzi wengine wanadai ilikuwa siku ya shangwe kama ile ya ‘Yesu kuingia Yerusalemu akiwa juu ya mwana-punda.’ Mmoja kati ya waliojitokeza kumpokea Haile Selassie ni mke wa mwanamuziki Bob Marley, Rita ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 21.
Ziara hiyo iliongeza nguvu kubwa ya imani ya Rastafari nchini Jamaica na kusambazwa duniani kote kupitia muziki. Bob Marley, akiwa na bendi ya Wailers waliachia albam mbili za moto zilizobeba ujumbe wa imani ya Rastafarian, Catch a Fire (1973) na Natty Dread (1975). Na humo Haile Selassie alitukuzwa. Albam hizo zilipanda mbegu iliyosambaa na kuzaa matunda ya waumini wengi duniani wa imani hiyo, wakiamini Mungu ni mmoja (Jah) na Messiah ni Haile Selassie, yaani Simba wa Yuda.
Mfalme wa Rhymes, Selemani Msindi, maarufu kama Afande Sele wa Morogoro, ambaye ni muumini wa Rastafari amewahi kusema kwenye wimbo wake ‘Kioo cha Jamii’, “adui muombee njaa, atanyoosha mikono juu hata kama alikuwa shujaa.”
Mwaka 1973, baa la njaa liliipiga vikali Ethiopia. Takribani watu 200,000 walikufa kwa njaa. Maombi ya maadui wa Haile Selassie ni kama yalitimia. Kwakuwa kwenye njaa kuna udhaifu, taifa la Ethiopia liligawanyika vipande viwili. Likaibuka kundi la wanajeshi linaloitwa ‘The Derg’. Wakaasi Serikali na kumpindua Mfalme Haile Selassie wakati huo wa njaa.
Wanajeshi wa Derg, walimkamata Mfalme Haile Selassie I kama mwizi na kumfunga kwenye chumba kimoja ndani ya himaya ya kifalme. Mfalme wa Wafalme akawa mfungwa. Katika chumba hicho, walimnyanyasa mzee huyo aliyekuwa na umri wa miaka 81. Idadi kubwa ya watu wa familia yake walifungwa katika jela yenye mateso makali ya Kerchele iliyoko Addis Ababa. Novemba 1973, waliokuwa maafisa wa Serikali ya Haile Selassie waliuawa kwa kupigwa risasi hadharani kama adhabu.
Mwaka 1975, ikiwa ni miaka miwili ya ufungwa, Haile Selassie alikufa mikononi mwa watesi wake akiwa na umri wa miaka 83. Watesi wake hao ndio waliotangaza kifo chake na kueleza kuwa alikufa kwa sababu ya ugonjwa na uzee. Sababu ambazo zilipingwa vikali.
Tangazo hilo la kifo cha Haile Selassie I lilizaa imani nyingine kwa jamii ya Rastafari. Wao sio tu walipinga sababu hiyo, lakini pia waliamini kuwa Messiah wao hakufa bali alipotea tu na kwamba amejiunga na Mungu Baba. Sababu hizo waliziita ‘Lie of Babylon (Uongo wa Mabeberu). Waliamini kuwa Haile Selassie sasa anaishi kiroho na mwili wake umechukuliwa na Jah (Mungu).
Ikazaliwa nguzo ya nyingine ya imani inayoahamika kama ‘I and I’. Naamini umeshasikia sana kwenye nyimbo za Reggae msemo huu ‘I and I’, maana yake ni kwamba binadamu wana miili tofauti lakini wote wanaunganishwa kwa roho. Hivyo, Rastafari hadi leo wanaungana kiroho na Messiah wao, Haile Selassie.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Blata Merse Hazen Wolde Kirkos, mbali na Rastafari, familia ya Haile Selassie ilipinga vikali sababu zilizotolewa na kundi la Derg. Pingamizi hilo liliendelea kuzitafuna Serikali zilizofuata, hadi mwaka 1994 baada ya Mahakama kuanika matokeo ya uchunguzi rasmi wa kifo cha Haile Selassie. Ilibainika kuwa, aliuawa kikatili na wanajeshi wa Derg akiwa kitandani. Nyaraka za amri ya kuuawa kwake zilibainika na wahusika waliokuwa hai walihukumiwa kifo.
Mwaka 1992, mabaki ya mifupa iliyoaminika kuwa ni ya Haile Selassie yalipatikana ndani ya sinki la choo cha jengo ya Himaya ya Kifalme alikokuwa amefungwa. Mifupa hiyo ilikusanywa na kuandaliwa mazishi ya heshima ya kifalme, yaliyofanyika Addis Ababa mwaka, Novemba 2000. Mifupa hiyo ilizikwa pembeni mwa kaburi la Mfalme Menelik II.
Ingawa mazishi hayo ya heshima yalihudhuriwa na watu maarufu katika imani ya Rastafari kama Rita Marley ambaye ni mke wa marehemu Bob Marley, idadi kubwa ya waumini wa Rastafari waliyapinga vikali kwani hawaamini kama mifupa hiyo iliyokutwa kwenye shimo la choo ni ya Messiah, Haile Selassie. Hivyo, wanaamini ni uongo mwingine wa mabeberu (Lie of Babylon). Wanaamini, Haile Selassie ameungana na Mungu, hivyo wanamuabudu kama sehemu ya Mungu (God Incarnate).
Nani wa kutatua utata wa kifo cha Mfalme Haile Selassie? Imani hujibiwa/kukosolewa kwa imani nyingine. Uchunguzi hukosolewa kwa uchunguzi mwingine.
Je, ni kweli mwili wa Mfalme wa Wafalme, Simba wa Yudah, Mkombozi wa Rastafari, Nguvu ya Utatu Mtakatifu, Mwenye Damu ya Kifalme inayoeshimiwa na kuogopwa, mteule wa Jah, Lij Tafari… King Haile Selassie ulitupwa ndani ya choo!? Je, ni kweli mifupa iliyozikwa tena kwa heshima ni mifupa yake halisi? Ni maswali ya vizazi na vizazi.
Falsafa za Haile Selassie za upendo, umoja na amani na kupinga ubaguzi wa aina yoyote, zimeendelea kudumu hadi leo.
Februari mwaka huu, Umoja wa Afrika (AU) uliweka sanamu ya Mfalme Haile Selassie nje ya jengo la Makao Makuu yake yaliyoko Addis Ababa, kama ishara ya kuthamini mchango wake katika kuanzisha umoja huo.
No comments