Vifo vya Vigogo Vyatikisa
DAR: Licha ya kwamba kila mwanadamu ataonja umauti kama maandiko ya vitabu vya dini yanavyoeleza, katika kipindi cha mwaka 2019 na kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu, idadi kubwa ya vifo vya watu maarufu wa kada mbalimbali imeshika kasi na kuitikisa nchi.
Hatua hiyo imekuja katika kipindi hiki ambacho pia kumeibuka wimbi la vifo vya ghafla ambavyo watalaam wa afya wanahusisha na magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, shinikizo la damu, kisukari na matatizo ya figo.
Watalaam wa afya wanaeleza kuwa, kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii, kumesababisha taarifa za vifo hivyo kusambaa kama moto wa kifuu kuliko miaka yote.
Vilevile wamebainisha kuwa, mabadiliko ya mfumo wa maisha kwa Watanzania, ni moja ya sababu zinazochangia kuongezeka kwa vifo vingi vya ghafla tofauti na miaka iliyopita.
Sababu hizo zinalandana na ongezeko la vifo hivyo vya viongozi wa dini, siasa, uchumi, afya na jamii kwa jumla hali ambayo imeibua taharuki hasa ikizingatiwa sasa kuna maambukuzi ya Virusi vya Corona vinavyoendelea kusababisha hofu kwa jamii.
VIFO VILIVYOTOKEA; WANASIASA, VIONGOZI WA SERIKALI
Katika kipindi cha miezi 16 kumetokea vifo kadhaa vya watu maarufu ikiwamo wanasiasa na viongozi mbalimbali wa Serikali kama vile Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Agustine Mahiga aliyefariki dunia Mei mosi, mwaka huu nyumbani kwake mkoani Dodoma.
Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Agustine Ramadhani aliyefariki dunia Aprili 28, mwaka huu katika Hospitali ya Aghakan jijini Dar alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani na kabla ya kupata mshtuko wa moyo.
Aprili 29, mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la Sumve kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Richard Ndassa, alifariki dunia baada ya kuugua ghafla wakati anahudhuria vikao vya Bunge jijini Dodoma.
Aprili 27, mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evodi Mmanda alifariki duniani baada ya kuugua kwa muda wa siku mbili.
Machi 23, mwaka huu, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema wa Ilala, Dk Milton Makongoro Mahanga na mbunge wa zamani wa Segerea alifariki dunia.
Septemba 11, 2019 aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Airtel Tanzania na waziri wa zamani wa uchukuzi, Dk Omary Nundu alifariki dunia.
Aprili 20, mwaka huu, aliyekuwa Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah (CCM) alifariki dunia.
Machi 28, mwaka huu, Waziri Kiongozi wa Kwanza Zanzibar, Brigedia Ramadhan Haji Faki, alifariki dunia.
Januari 15, mwaka huu, Mbunge wa Newala-Vijijini, Rashid Ajali Akbar alifariki dunia.
Mei 5, mwaka huu, wakili maarufu nchini, Masumbuko Lamwai, aliyepata kuwa Mbunge wa Ubungo (NCCR-Mageuzi) na mbunge wa kuteuliwa alifariki dunia baaa ya kuugua ghafla.
Oktoba 23, 2019, aliyekuwa mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, James Mapalala alifariki dunia katika Hospitali ya Kairuki.
Tarehe 27, Aprili pia ilishuhudia majaji wawili wastaafu nchini humo wakifariki dunia, Jaji Ali Haji Pandu ambaye aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na moja ya waasisi wa chama cha CUF na Jaji Mussa Kwikama ambaye alikuwa kiongozi mwandamizi wa Chama cha ACT-Wazalendo.
Aprili 27, mwaka huu, Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Isihaka Sengo alifariki dunia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Sokoine.
VIONGOZI WA DINI
Kwa upande wa viongozi wa dini pia kulikumbwa na pigo ambapo Mei 4, Mchungaji Peter Mitimingi wa Kanisa la Ghala la Chakula cha Uzima (Warehouse Christian Centre- WCC) alifariki dunia baada ya kupata homa ya mapafu, Mchungaji Dk Getrude Lwakatare, ambaye alikuwa Mchungaji Mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto jijini Dar na Mbunge wa Viti Maalum aliaga dunia ghafla Aprili 20 jijini Dar.
Mwingine ni Mwanazuoni wa Tanzania na Afrika Mashariki, Sheikh Suleiman Amran Kilemile aliyefariki dunia Mei 5, mwaka huu jijini Dar kwa matatizo ya kisukari.
WACHUMI
Mei 2, 2019, Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP na mmoja wa matajiri na mashuhuri nchini, Dk Reginald Mengi alifariki dunia baada ya kuugua ghafla.
Februari 26, mwaka 2019, Mkurugenzi wa Vipindi na Uendeshaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba alifariki dunia nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu kwa muda mrefu.
Disemba 8, 2019, mfanyabiashara mashuhuri Tanzania, Ali Mufuruki alifariki nchini Afrika Kusini baada ya kuugua kwa muda mfupi matatizo ya homa ya mapafu.
WENGINE
Aprili 28, mwaka huu, Mdogo wa Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa anayefahamika kwa jina la Bernard Lowassa, alifariki dunia.
Aprili mosi mwaka huu, aliyekuwa mtangazaji mkongwe wa kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC), Marin Hassan Marin alifariki dunia.
Machi 30, mwaka huu aliyekuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte alifariki dunia.
Mei mosi mwaka huu, Mganga wa Tiba Asili na Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Tiba Asilia Tanzania (Chawatiata), Dk Maneno Tamba alifariki dunia.
Machi 25, mwaka huu, aliyekuwa Ofisa Habari wa Simba SC na mwandishi wa habari za michezo, Asha Muhaji alifariki dunia.
Februari 24, mwaka huu, Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Mzee Iddi Mohamed Simba alifariki dunia kwa matatizo ya moyo.
WATALAAM WATOA SABABU
Kufuatia mfululizo wa vifo hivyo ambavyo vingi ni vya ghafla, Gazeti la IJUMAA lilizungumza na Dk Isack Maro ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya TMH ya jijini Dar ili kupata ufafanuzi na sababu halisi ya hali hiyo inayotokea ndani ya jamii sasa.
Dk Maro alisema ongezeko la magonjwa ya yasiyo ya kuambukiza ambayo yanatoka na mtindo wa maisha ambao unachagizwa na vyakula vinavyotumika zaidi kwa sasa.
“Watu wanakula sana vyakula vya mafuta na wanga kwa wingi, wanakula vyakula visivyoweza kuupa mwili kinga jambo linalozidisha watu kuwa na uzito kupindukia.
“Vilevile mtindo wa kutofanya mazoezi mara kwa mara ni jambo ambalo linachangia ongezeko la vifo hivi vya ghafla hasa ikizingatiwa magonjwa kama ya moyo, kisukari, saratani na shinikizo la damu yamezidi kushika kasi,” alisema.
Aidha, alisema tabia ya watu kutofanya ‘checkup’ ya afya zao ni mojawapo ya sababu ya kutokea vifo vya ghafla.
“Kwa sababu mtu kama atafanya checkup kila mara, ataweza kubaini madhaifu ya mwili wake na kupatiwa matibabu mapema,” alisema.
Dk Maro alionya kuwa watu lazima wabadilike kwa kuanza kubadilisha mfumo wa kula, kufanya mazoezi na vipimo vya afya mara kwa mara.
Naye Dk Walter Kweka kutoka Hospitali ya TMJ jijini Dar, naye alifafanua mtindo wa watu kutofanya vipimo vya afya kila mara huchangia wagonjwa kwenda hospitali wakiwa katika hali mbaya.
“Pia katika nchi zinazoendelea, watu wanafanya kazi zaidi kuliko kujali afya zao, wanakosa muda wa kufanya mazoezi na kujali afya zao,” alisema.
Hoja hizo za Dk Maro pia ziliungwa mkono na Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar, Dk George Kahangwa alisema ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii vilevile imechangia taarifa za vifo hivyo kuongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita.
“Lakini pia tutambue kuwa idadi ya watu inaongezeka kama sasa duniani kuna watu zaidi ya bilioni saba, wakati Tanzania kuna idadi ya watu zaidi ya milioni 60, hivyo lazima kuwepo na ongezeko la vifo ikilinganishwa na miaka iliyopita,” alisema.
Kwa upande wake Mwanasaikolojia Christian Bwaya alisema baadhi ya vifo vya ghafla pia vinachagizwa na magonjwa yatokanayo na mfumo wa maisha.
Alitolea mfano kuwa watu wanakumbwa na matatizo ya sonona, ambayo huwazidishia huzuni, hali ya kukata tamaa na hata kumnyima mtu hamu ya kula au kula kupita kiasi jambo ambalo si afya kwenye mwili wa binadamu.
“Jambo la msingi watu wanapaswa kulinda afya ya mwili na akili, kwa sababu vyote vinategemea, kama usipokuwa na utulivu wa nafsi unaweza kupata matatizo mengine kama vile shinikizo la damu na mwishowe vifo vya ghafla,” alisema.
MAGONJWA YANAYOONGOZA KUSABABISHA VIFO DUNIANI
Katika takwimu mbalimbali zilizotolewa na mtandao wa ‘worldlifeexpectancy.com’ ambao unatoa taarifa za papo kwa hapo kuhusu matukio mbalimbali ikiwemo afya, umebainisha kuwa matatizo ya moyo ndiyo yanayoongoza kusababisha vifo.
Kwa mujibu wa mtandao huo, matatizo mbalimbali ya moyo ndiyo yanayoshika namba moja duniani kwa kusababisha vifo milioni 8.7, matatizo ya kupooza yapo katika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo milioni 6.2
Magonjwa ya homa ya mapafu na mafua yamesababisha vifo milioni 3.3, wakati magonjwa ya ini milioni 3.1, saratani ya ini milioni 1.6 na kisukari milioni 1.5.
TANZANIA
Kwa upande wa Tanzania, magonjwa ya homa ya mapafu na mafua ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo ambapo vifo 39,020, Ukimwi unashika namba mbili kwa kusababisha vifo 35,234, magonjwa ya kuhara unashika namba tatu kwa vifo 29,645, kifua kikuu vifo 28,867 na magonjwa ya moyo vifo 19,082 kwa mwaka.
Stori: GABRIEL MUNSHI, Ijumaa
No comments