Dawa ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) yatoa mwanga wa matumaini kwa wagonjwa wa corona
DAWA iliyofanyiwa kazi na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imetoa mwanga wa matumaini kwa wagonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya corona.
Dawa hiyo iliyopewa jina la NIMRCAF (pichani), inatokana na mchanganyiko wa vyakula; na katika majaribio imeonesha ina uwezo mkubwa wa kudhibiti virusi vya corona.
Akielezea mchanganyiko huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Tiba Asili cha NIMR, Dk Justine Omolo alisema ni fomula ya tiba lishe, ambayo ina mchanganyiko wa pilipili kichaa, tangawizi, limao na kitunguu saumu, asali na maji. Alisema dawa hiyo inasaidia kumpa nafuu mgonjwa wa corona, kwa kutibu dalili zinazotokana na ugonjwa huo, na kwamba tayari imeshaonyesha matokeo chanya.
“Mchanganyiko wa tiba lishe hiyo sio dawa ya corona, lakini inasaidia kumpa nafuu mgonjwa wa corona kwa kuwa inatibu dalili zinazoambatana na ugonjwa huo,” Dk Omolo amesema na kuongezea kwamba
mpaka sasa tiba lishe hiyo imeshaleta matokeo chanya kwa kuwa imesaidia wagonjwa wengi wa corona. Alisema kwa sasa mahitaji yamekuwa ni mengi, tofauti na awali.
“Mwanzo tulikuwa tukitengeneza chupa 1,000 na tumekuwa tukisambaza hospitali kwa wagonjwa kwa siku chupa 120 hadi 200, lakini sasa mahitaji yamekuwa makubwa na imeonyesha matokeo mazuri kwa wagonjwa,” alisema
Alisema kutokana na mafanikio hayo, serikali imewaongezea vifaa ambapo kuanzia wiki ijayo wataanza kuzalisha chupa 5,000 kwa siku.
Alisema chupa hiyo yenye ujazo wa nusu lita, inauzwa Sh 10,000 na ni dozi ya mtu mmoja ambayo inanyweka kwa siku tano, ambapo mgonjwa atalazimika kunywa mara tatu kutwa.
Dalili za ugonjwa huo wa corona ni joto mwilini na kikohozi kikavu; na baada ya wiki moja kikohozi hicho kinaweza kusababisha tatizo la kushindwa kupumua.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya duniani (WHO) kwa wagonjwa 56,000, ulibaini kuwa asilimia 80 ya wale walioambukizwa, hupata dalili zisizo kali kama vile kukohoa, joto mwilini na mara nyingine homa ya mapafu, asilimia 14 hupatwa na dalili kali, kama vile tatizo la kupumua.
Asilimia sita hukumbwa na tatizo la mapafu kushindwa kufanya kazi na viungo vingine mwilini na hata kusababisha kifo.
Miongoni mwa dalili nyingi zilizoripotiwa na wagonjwa, asilimia 88 walidai kuwa na joto mwilini, asilimia 68 kikohozi kikavu na asilimia 38 waliripoti uchovu. Tatizo la kupumua liliwapata asilimia 19 ya wagonjwa, asilimia 13 waliripoti kuumwa na kichwa na asilimia nne waliripoti kuharisha.
Omolo alisema kwa mtu ambaye hana dalili, anapaswa kutumia dawa hiyo mara moja kwa siku na hiyo itamsaidia kujikinga na ugonjwa huo wa corona, ambao takwimu za WHO zinaonesha hadi Mei 6, mwaka huu, ulikuwa mewakumba watu 3,588,773.
“Watu wanapaswa kujua kwamba virusi vya corona au Covid 19 ni mojawapo ya homa, hivyo basi vina dalili nyingi zinazofanana na homa ya kawaida’’, alisema
“Lazima uwe makini iwapo unahisi tatizo la kupumua.
Ni muhimu kutafuta msaada wa matibabu haraka. Tiba lishe hii haina madhara, watu waitumie ili kujikinga na janga hili la corona, “ alisisitiza Watalamu wanasema zipo njia nne za kudhibiti vimelea vya magonjwa hasa virusi ambavyo havina tiba.
Njia ya kwanza ni chanjo na ya pili ni kuzuia virusi visiweze kujishikiza kwenye seli zilizopo mwilini. Njia ya tatu ni kudhibiti visizaliane au kuongezeka mwilini na njia ya nne ni kuongeza protini mwilini ili kusaidia kupambana na virusi hivyo.
Kwa mujibu wa Dk Omolo, NIMRCAF ina vitamini C kwa wingi na vitamini K, na kitaalamu mchanganyiko unaopatikana katika tiba lishe hiyo unaitwa ‘Polyphenols’.
Mchanganyiko huo unazuia damu kuganda.
Alisema seli zinazopokea virusi vya corona, zipo kwenye mapafu na virusi vikiingia humo, husababisha damu kuganda na kuleta matatizo kwenye mfumo wa upumuaji. “Mgonjwa akitumia tiba lishe hii, ndani ya nusu saa lazima atasikia nafuu.
Wagonjwa wengi waliokuwa hoi walipoitumia, wamepata matokeo mazuri na wengine wamepona kabisa,”alisema Alisema walianza utafiti wa dawa hiyo muda mrefu, kabla dunia haijakumbwa na janga la corona.
Walifanya utafiti huo kwa kushirikiana na watalamu mbali mbali wa tiba asili. Walikuwa katika kutafiti tiba ya Ukimwi.
NIMR imekuja na dawa lishe hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya WHO kutoa taarifa yake, ambayo ilieleza kuwa wanatambua na kuthamini mchango wa tiba asili kutoka Afrika. WHO ilieleza kwamba dawa hizo, pia zinapaswa kupewa nafasi sawa katika kufanyiwa majaribio, kama dawa kutoka maeneo mengine duniani.
No comments