Moshi Mweupe Chanjo ya Corona, Italia Wadai Kupata Majibu!
WANASAYANSI duniani kote wanaumiza vichwa kutafuta chanzo ya ugonjwa ulioitikisa dunia wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona (Covid- 19) ambao mpaka sasa unaweza kusema kwamba tayari moshi mweupe umeanza kuonekana angani!
Taarifa zenye kutia matumaini makubwa, ni kwamba ukiachana na Madagascar kutangaza kugundua dawa ya kutibu ugonjwa huo, inayopigiwa debe na Rais wa nchi hiyo, Andy Rajoelina, Covid Organics inayotengenezwa kutoka kwenye mmea ambao kitaalamu huitwa Artemisia, wanasayansi nchini Italia wanadai kuwa wamegundua chanjo.
Ipo tofauti kubwa kati ya chanjo na tiba, Madagascar wanayo dawa, Covid Organics ambayo hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kwamba bado haijafanyiwa majaribio ya kitaalamu na haijathibitika kuwa na uwezo wa kutibu Corona lakini Italia wao wanadai kugundua chanjo ambayo itaweza kuwakinga watu dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu.
Utakumbuka kwamba kabla ya mambo kuwa mabaya barani Afrika, Italia ilipigwa na kimbunga cha mauti, watu takribani 30,000 wakafariki kwa maambukizi ya Corona huku jumla ya watu 214,457 wakipata maambukizi nchini humo.
Pengine majeraha makubwa waliyoyapata Waitaliano yamewapa nguvu ya kufanya kazi usiku na mchana, kwa uchungu na nguvu zote mpaka kufikia kugundua chanjo hiyo, wakiuthibitisbhia ulimwengu kitu cha tofauti tangu Marekani ilipotangaza kwamba itachukua zaidi ya miezi 18 kugundua chanjo hiyo.
Kabla hatujaendelea, ni vyema kwanza tukatazama jinsi chanjo inavyofanya kazi kwenye mwili wa binadamu na hapa tunazungumzia chanjo kwa jumla, bila kujali ni ya ugonjwa gani.
“Kwa kawaida, mfumo wa kinga ya mwili, unaoundwa kwa asilimia kubwa na chembe hai nyeupe za damu (white blood cells) ndiyo unaohusika na kuukinga mwili dhidi ya maambukizi ya maradhi mbalimbali,” anasema Dokta Godfrey Charles, mtaalamu wa magonjwa ya wanawake na watoto kutoka Hospitali ya Temeke na kuongeza:
“Mazingira tunayoishi yanakuwa na vimelea vingi vya maradhi, kuanzia hewa tunayovuta, maji tunayokunywa, vyakula tunavyokula mahali tunapokaa au kulala na kadhalika lakini kwa kuwa mwili una mfumo wake wa kujilinda wenyewe, huweza kupambana na maambukizi haya yanayosababishwa na virusi au bakteria, wakati mwingine bila sisi kujua.”
Jarida la Journal of Medical Research la nchini Marekani katika chapisho lake la Natural Immunity (Kinga Asilia), linafafanua kwamba kwa kawaida, seli za mwili zinazohusika na ulinzi, hufanya kazi ya kuzitambua haraka seli za vimelea vya maradhi vinavyoingia katika mfumo wa damu na kuzishambulia. Inapotokea vimelea vya magonjwa vimepambana na seli za ulinzi wa mwili na kuzizidi nguvu, ndipo pale mtu anapoanza kujihisi kama anaumwa!
Maelezo ya kitaalamu yanazidi kuongeza kwamba katika utengenezaji wa chanjo, kinachofanyika huwa ni kuifundisha kinga asili ya mwili, namna ya kuvitambua kwa haraka vimelea vya aina fulani na kuvishambulia kabla havijaleta madhara katika mwili.
Kivipi? Chembechembe za bakteria au virusi wanaosababisha ugonjwa fulani (antigens), huchukuliwa kitaalamu na kupunguzwa makali kisha kuingizwa kwenye mwili wa binadamu kwa kiasi kidogo, kwa lengo la kwenda kuishtua kinga ya mwili kuweza kutambua uwepo wa vimelea hivyo, na kupambana navyo mpaka kuvishinda.
Japokuwa hawatakuwa na madhara, lakini bado seli za mwili zitawashambulia na kujenga uwezo wa kupambana tena ikitokea wameushambulia tena mwili. Kwa kawaida, mwili unaposhambuliwa na vimelea fulani, seli za mwili huviweka vimelea hivyo kwenye kumbukumbu zake na ikitokea vimelea vya aina hiyohiyo vikauvamia tena mwili, seli zinakuwa tayari zinazo kumbukumbu za jinsi ya kupambana kwa haraka na vimelea hivyo.
Hicho ndicho kilichofanyika kwenye aina hii ya chanjo ambayo kitaalamu huitwa Live Attenuated Vaccines (L.A.V) ambapo magonjwa yaliyokuwa yakitisha kwa kukatisha maisha ya watu kama Polio, Surua, Ndui na kadhalika, yameweza kudhibitiwa kabisa kwa watoto wadogo kupewa chanjo ambayo huwalinda katika kipindi chote cha maisha yao.
Pengine unaweza kujiuliza, kama ni rahisi kiasi hicho kutengeneza chanjo, yaani unachukua antibodies za vijidudu vinavyosababisha maradhi halafu vinapelekwa maabara na kufanyiwa ‘genetic engineering’ na tayari chanjo inakuwa imepatikana, kwa nini imekuwa kazi nzito kiasi hiki kupata chanjo ya Corona?
Lazima utambue kwamba kuna vimelea vya aina tofautitofauti ambavyo husababisha maradhi kwenye mwili wa binadamu lakini vinavyoongoza ni bacteria na virusi. Magonjwa yanayosababishwa na bakteria, huwa mepesi kutibika na hata chanjo zake, hupatikana kwa urahisi, tofauti na magonjwa yanayosababishwa na virusi.
Corona inasababishwa na virusi na sifa moja kubwa ya virusi, vinapoingia ndani ya mwili wa binadamu, ndani ya muda mfupi tu huingia kwenye seli na kujibadilisha kufanana na seli za mwili, kitendo ambacho kitaalamu huitwa camouflage! Kitendo hiki huzichanganya seli za mwili na kushindwa kuelewa adui ni yupi na rafiki ni yupi, hivyo kushindwa kuelewa wapi pa kushambulia.
Mbaya zaidi, licha ya kujibadilisha na kufanana na seli za mwili, virusi huanza kubadilisha DNA (vinasaba) vya seli za mwili, kwenda kwenye RNA na kudhoofisha zaidi seli za mwili wakati vyenyewe vikiendelea kuzaliana kwa wingi.
Kingine ni kwamba virusi vina uwezo wa kuwa vinabadilikabadilika maumbo yake na kuzidi kuzichanganya seli za mwili zinazohusika na ulinzi na pengine hii ndiyo sababu inayofanya magonjwa yanayosababishwa na virusi, yawe magumu sana kutibika, chukulia mfano rahisi wa jinsi dawa ya HIV/AIDS inavyoendelea kusumbua vichwa vya wanasayansi kwa miaka nenda rudi.
CHANJO YA ITALIA
Wakati duniani kote hali kizidi kuwa tete, wanasayansi nchini Italia wametangaza kwamba wamegundua chanjo ya Corona, ambayo imeonesha mafanikio makubwa katika majaribio yaliyofanywa kwenye seli za panya ambazo zinafanya kazi sawa na seli za mwili wa binadamu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini humo, majaribio ya awali yamefanyika katika Hospitali ya Spallanzani jijini Rome ambapo inaelezwa kwamba baada ya panya kuingizwa virusi vya Corona, seli zake zilizalisha antibodies nyingi kwa ajili ya kupambana na antigens za virusi hivyo.
Taarifa hizo zimepokelewa kwa shangwe kubwa duniani kote ambapo waziri wa ulinzi wa Israeli, Naftali Bennett amewapongeza Italia kwa hatua hiyo na kuongeza kwamba taasisi ya Israel’s Institute for Biological Research (IIBR) nayo ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha majaribio ya chanjo na kutaka ushirikiano kati ya nchi hizo mbili uzidi kuimarishwa kuhakikisha chanjo kamili inapatikana.
Wakati hayo yakiendelea nchini Italia, Marekani nayo haiko nyuma ambapo Chuo Kikuu cha Oxford kipo kwenye awamu ya kwanza ya majaribio ya chanjo ya Corona iliyoanza April 23 ambapo tofauti na Italia, Marekani inawatumia watu (volunteers) kwenye majaribio ya chanjo hiyo.
Hata hivyo, bado mafanikio hayajawa makubwa kama ilivyo nchini Italia na endapo mafanikio yaliyoonekana kwenye panya yataonekana pia kwa binadamu, maana yake ni kwamba Italia itakuwa ndiyo nchi ya kwanza kugundua chanjo hiyo.
Ni suala la muda tu lakini hakika yajayo yanaleta matumaini!
No comments