Waziri Mkuu Majaliwa awaonya waamuzi mpira wa Miguu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka waamuzi watakaochezesha mashindano ya mpira wa miguu ya jimbo la Ruangwa wawe makini na wajiepushe na vitendo vya rushwa.
“Waamuzi msiingize maslahi binafsi wala msijiingize kwenye rushwa kutoka timu yoyote, tunahitaji michezo hii ichezwe kwa jitihada za wachezaji wenyewe.”
Ametoa agizo hilo jana (Alhamisi, Agosti 19, 2021) alipokabidhi vifaa vya michezo kwa timu nane zilizofikia hatua ya robo fainali. Mashindano yalihusisha timu 38 kutoka katika jimbo hilo.
Vifaa alivyovitoa ni jezi na mpira mmoja kwa kila timu, kombe ambalo litagawiwa kwa timu itakayoibuka mshindi wa kwanza katika fainali zinazotarajiwa kufanyika Agosti 30, 2021.
Amesema lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuwahamasisha vijana wanaopenda mpira wa miguu waweze kucheza kwa bidii na kuongeza tija. Amesema kwa sasa mpira wa miguu ni ajira.
Amewataka viongozi Chama cha Mpira wa Miguu wilaya ya Ruangwa (RUDIFA) wasimamie vizuri mashindano hayo ili kuwawezesha vijana wanaoshiriki waweze kutimiza malengo yao.
Waziri Mkuu amesema mbali na kuleta afya na ajira kwa washiriki michezo pia ina tabia ya kuwaunga watu pamoja na kuwawezesha kujadili shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Majaliwa ameahidi kuunga mkono mipango inayofanywa na RUDIFA ili kuhakikisha sekta ya michezo inakuwa na mafanikio na kuwawezesha vijana wengi kujiajiri.
“Vijana wa Ruangwa jengeni wivu na mjitume sana ili muweze kupandisha viwango vyenu vya uchezaji na hatimaye muweze kupata nafasi ya kucheza katika vilabu vinavyoshiriki ligi kuu.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa RUDIFA Yussuf Mpame, amesema mashindano hayo ni muhimu kwa maendeleo ya mpira wa miguu wilayani Ruangwa kwani uwepo wake unafaida kubwa sana.
Aidha, Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa kwa msaada anaoutoa katika maendeleo ya michezo.
No comments