Mikutano ya hadhara ya Waziri Mkuu yasitishwa Mbeya
Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema Serikali imesitisha kuwepo kwa mikutano minne ya hadhara iliyopangwa kufanywa katika ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Homera amesema hayo leo Jumamosi Julai 31, 2021 wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uzinduzi wa mafunzo ya uanagenzi awamu ya tatu kitaifa yatakayofanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknoknolojia (Must).
Homera amesema kuwa Serikali imefikia hatua ya kufuta mikutano kwa lengo la kuepukana na uwekano wa ongezeko la wagonjwa wa Covid-19.
"Ilipangwa Waziri Mkuu kuwa na mikutano ya hadhara katika baadhi ya Wilaya hususan Mbarali na Chunya, Mbeya Jiji na Mbarali na Mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya, lakini tumeona ni vyema isiwepo kwani kutakuwa na mikusanyikp mikubwa ya watu watakaojitokeza kumsikiliza Waziri Mkuu" amesema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama amesema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa kwa vijana na ndio maana imewekeza udhamini wa mafunzo ya Uanagenzi kwa vijana nchini kwa lengo la kuzalisha wataalamu wa nyanja mbalimbali watakaowezesha utekeleza wa miradi inayoelekezwa hususan reli za kisasa, nishati ya umeme ni miundombinu.
"Program itakayozinduliwa na Waziri Mkuu Agosti, 2 Mwaka huu katika Chuo cha Must kuna vipengele vikuu vinne ikiwa ni pamoja na mafunzo ya uzoefu wa kazi, urasimishaji ujuzi unaopatikana nje ya mafunzo rasmi (RPL) pamoja na mafunzo ya uanagenzi na mafunzo ya kuhuisha ujuzi kazini (Skill upgrading) "amesema.
ADVERTISEMENT
Amesema kuwa mafunzo hayo kwa asilimia 100 yamedhamiwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan huku vijana wanaopata fursa kutotakiwa kulipia gharama zozote na kuonywa vitendo vya rushwa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknoknolojia (Must), Aloyce Mvuma amesema wanashukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapa heshima ya kuwa sehemu ya uzinduzi wa program hiyo na kwamba watahakikisha wanatoa mafunzo kwa uaminifu.
"Hii ni heshima kubwa wametupa sisi Must, na kwa niaba ya uongozi nashukuru sana kwa nafasi hii na niahidi kwa uwezo na uzoefu wetu tutatoa mafunzo haya kwa uaminifu" amesema Mvuma.
No comments