Header Ads

Header ADS

Biashara ya ukahaba ni kaa la moto Dar



Licha ya juhudi zilizowahi kufanywa na viongozi wa Jiji la Dar es Salaam kudhibiti biashara ya ukahaba na uzururaji jijini humo, shughuli hiyo inaendelea kama kawaida, Mwananchi limebaini.

Baadhi ya viongozi waliowahi kuongoza Dar es Salaam, akiwemo Paul Makonda walianzisha kampeni za kupambana na biashara hiyo bila mafanikio na sasa imeonekana kuchukua sura mpya.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo umebaini kuwepo kwa madanguro ambapo wanawake na wasichana walio na umri kati ya miaka 15 - 40 hujihusisha na biashara hiyo.

Biashara hiyo kongwe katika historia ya maisha ya binadamu, imekithiri zaidi katika majiji makubwa duniani ambapo wanawake huuza miili yao ili kujipatia fedha za kuendesha maisha.


Jambo hilo jijini Dar es Salaam limekuwa la kawaida katika baadhi ya mitaa ambako makahaba wanaishi katika nyumba zao au wanapita katika mawindo na wengine hujichanganya katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo misiba, harusi au biashara.

Wateja wao wakubwa ni wanaume wa rika na kipato tofauti, wakiwemo ambao wameoa na bado wanawafuata makahaba kukidhi tamaa zao.

Dar es Salaam ina maeneo mengi ambayo yanatumika kama madanguro, tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wanajipanga barabarani, achilia mbali maeneo kongwe ya Manzese na Temeke. Maeneo mengi zaidi sasa “yamerasimishwa” kwa ajili ya shughuli hiyo, yakiwaingizia pesa wao na wamiliki wa nyumba hizo.

Uchunguzi umebaini biashara hii katika maeneo ya Ubungo, Ilala, Kinondoni na Temeke ambako inahusisha hadi wasichana chini ya umri wa miaka 18 ambao wanaonekana katika maegesho ya magari pembeni mwa baa mbalimbali maarufu majira ya usiku.

Wasichana hawa hufanya shughuli hiyo saa 24, kwa kuwa majira ya mchana wanapatikana zaidi kwenye madanguro, jioni wanakwenda katika baa maarufu na usiku wanahamia katika klabu na baa zinazokesha na wengine wamekuwa wa kisasa zaidi wakitumia simu.

Ubungo Riverside

Pembezoni mwa Baa ya Zambezi iliyopo River Side, Ubungo wasichana hujipanga kuanzia karibu na kituo cha mafuta na kuzunguka baa hiyo kuanzia majira ya saa 12 jioni. Wasichana hao wana vyumba vyao katika nyumba moja ya kulala wageni iliyopo jirani na baa hiyo.

Wasichana hao wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 16 hadi 25 wamegeuza eneo hilo kuwa kijiwe chao maarufu, jambo ambalo huwashtua wageni wanaotembelea maeneo hayo kwa mara ya kwanza.

“Hawa ni maarufu hapa yapata mwaka sasa, wanazidi kuongezeka kila siku na ukiangalia wapo wadogo zaidi. Kinachoumiza wateja wao ni watu wazima wanaojielewa kabisa wanapaki magari na hawa wasichana wanawasogelea na mteja huchagua anayemhitaji,” anasema Mudy Mustapha, dereva wa bodaboda.

Mkazi wa Riverside, Lutufyo Mwakalinga anasema watoto wanajifunza maadili yasiyofaa kutoka kwa makahaba hao kuanzia wanavyovaa, wanavyozungumza na wanavyotembea.

“Hawa wanasimama hapa, njia ambayo kila mtu anapita. Watoto watakuwa salama kweli? Sijui kwa nini Serikali imeshindwa kulidhibiti hili?” alisema.

Manzese Tiptop

Eneo jingine maarufu kwa biashara hiyo ni Mtaa wa Mnazi Mmoja (Tip Top) uliopo Manzese ambapo wanawake wanaofanya biashara hiyo wamepanga nyumba maalumu katikati ya makazi ya watu.

Gazeti hili lilitembelea mtaa huo kuanzia majira ya saa 1 hadi saa 8 usiku kuangalia jinsi biashara hiyo inavyofanyika na maeneo ambayo biashara hiyo imeshamiri katika mkoa huu.

Katika mtaa huo, waandishi wanaonyeshwa nyumba yenye vyumba zaidi ya 10 ambavyo vinakaliwa na makahaba kwa ajili ya biashara hiyo ambako wateja wao huwafuata.

“Ukipita hapo kwenye kichochoro utatokea kwenye nyumba ambayo wanakaa hao makahaba,” alisema dereva bodaboda anayefanya biashara katika eneo hilo, akiwaelekeza waandishi.

Waandishi walifanikiwa kufika kwenye nyumba hiyo maarufu kama “kwa Wahaya”. Ni nyumba chakavu na ina vyumba zaidi ya 10 ambavyo vimefuatana mithili ya fremu za maduka zilizopo barabarani.

Kila kahaba ana chumba chake na anakaa nje ya mlango wake akisubiri wateja huku mlango wa chumba chake ukiwa wazi. Mtu anayepita katika kichochoro hicho anawaona wanawake hao na ukitupa jicho ndani ya chumba unaona kitanda huku taa yenye mwanga hafifu ikiwa inawaka.

Njia hiyo inatumiwa na watu wengine wanaoishi katika mtaa huo, lakini makahaba hao wanatambua mtu anayepita kwa shughuli zake nyingine na yule aliyekwenda kupata huduma yao.

“Shemeji, karibu!” alisema kahaba mmoja akimwambia mwandishi wa gazeti hili ambaye alikuwa akiwaangalia wakati anapita kwenye njia hiyo.

Akizungumzia biashara hiyo, Diwani wa Kata ya Manzese, Eliam Manumbu alisema ni haramu na haikubaliki hapa nchini kwa sababu ni kinyume cha maadili.

Alikiri kuwepo kwa biashara hiyo katika kata yake, hata hivyo, anasema amepokea taarifa ya wenyeviti wake wa mitaa kwamba makahaba wanaondolewa katika baadhi ya mitaa wanayopenda kusimama.

Anasema alipoambiwa kwamba makahaba hao hivi sasa hawasimami barabarani bali wanapanga nyumba, diwani huyo ameahidi kufuatilia suala hilo na kuchukua hatua.

“Hili sasa umeniambia, nitafuatilia kwa kushirikiana na wenyeviti wa Serikali za mitaa, hasa huo mtaa wa Mnazi Mmoja unaouzungumzia,” alisema Manumbu.

Sehemu nyingine huko Manzese ni baa moja maarufu. Baa hiyo inatumika kama danguro na ndani yake kuna vyumba ambavyo vinatumiwa na makahaba hao kwa biashara yao.

Baa hiyo inajaa zaidi siku za mwisho wa wiki na inakuwa na makahaba wengi kutoka maeneo mbalimbali na wanaipenda kwa sababu ina miundombinu ambayo inawawezesha kufanya biashara yao kwa urahisi.

“Ukitaka makahaba nenda pale, utawakuta wa kila aina, wangine ni vitoto kabisa, ukienda pale utawakuta hasa Jumamosi ndiyo wanakuwa wengi,” anasema mhudumu wa baa nyingine jirani, aliyejitambulisha kwa jina moja la Zawadi.

Timu ya gazeti hili ilifika mpaka baa iliyotajwa ambayo jina lake linahifadhiwa na kushuhudia jinsi eneo hilo lilivyo na nafasi ya kutosha na wasichana wapo wengi zaidi kuliko wanaume, baadhi yao walikuwa wamejipanga huku baadhi wakicheza muziki na wengine wakipata vinywaji.

Moja ya masharti katika baa hiyo ni kutopiga picha au kurekodi video kutokana na biashara inayofanyika humo na kuweka usiri kwa makahaba na wateja wao.

Ushuhuda wa wahusika

Mmoja wa makahaba wanajiuza katika baa moja maarufu ya Manzese akijitambulisha kwa jina la Jack (28) alizungumza na gazeti hili na kubainisha kuwepo kwa makahaba walio na umri chini ya miaka 18, lakini akisema ni vigumu kuwabaini kwa sababu ya mwonekano wa maumbile yao kufanana na watu wazima.

Anasema makahaba wanaoonekana wadogo huwa wanafukuzwa wanapojaribu kuingia katika baa hiyo lakini wenye wenye maumbo makubwa wanaruhusiwa kuingia.



No comments

Powered by Blogger.