Makada wa Chadema wadaiwa kushikiliwa na Polisi Mbeya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya kimedai kuwa makada wake watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Mbozi Pascal Haonga.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa yuko kwenye msafara wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anayetembelea mkoa huo.
Akizungumza kwa simu na Mwanachi leo Jumatatu Agosti 2, 2021 Mwenyekiti wa Chadema Mkoa, Joseph Mwasote maarufu kwa jina la China, amesema kuwa amepata taarifa za kukamatwa kwa makada hao jana walipokuwa wakihudhuria mkutano wa muungano wa wanafunzi wa Chadema (Chaso).
Amesema kuwa awali alipata taarifa ya kukamatwa kwa wafuasi 39 ambao inadaiwa waliachiwa usiku wa jana na mpaka sasa wanaoshikiliwa ni pamoja na katibu wa Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga na Katibu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Emily Mwakilembe.
"Awali walifuatwa na polisi katika ofisi kanda na mkoa kutakiwa wasiwepo kwenye mikusanyiko na kulazimika kwenda kwenye ukumbi wa baa ya Banyamulenge eneo la Forest na kukodi ukumbi ambapo walifuatwa na kukamatwa," amesema Mwasote.
Huku akilaani ukatwaji huo, Mwasote amesema vyama vya siasa vina haki na uhuru wa kufanya mikutano ya ndani kwa mujibu wa sharia.
No comments