Matapeli waanza kuwarubuni walimu ajira mpya 6,000
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe amesema amepata taarifa kuwa wapo watu ambao wamekuwa wakiwatapeli fedha baadhi ya walimu wanaotaka kuomba ajira kwa kuwataka watoe pesa ili wapate ajira.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe
Prof. Shemdoe ametoa taarifa hiyo wakati akitolea ufafanuzi kuhusu ajira 6000 za walimu ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliamuru kuwa walimu waajiriwe ili kukabiliana na uhaba wa watumishi wa kada hiyo.
“Nimepata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa baadhi ya watu kwa nia ovu wamekuwa wakiwatapeli kwa kuwaomba fedha baadhi ya walimu wanaotaka kuomba ajira na kuwataka watoe pesa ili zifikishwe Wizarani kwa ajili ya kuwapatia ajira, nipende kusema wazi kwamba jambo hili halipo,” amesema Prof.Shemdoe.
"Niwaombe watumishi wenzangu tusijiingize kwenye jambo hili, nitoe tahadhari kubwa kwa wale vishoka ambao wameamu kujichukulia fedha za watanzania wenzetu iliwajifanye watawatafutia ajira TAMISEMI hao tukiwapata tutapambana nao vikali" amesema Prof.Shemdoe
Mnamo tarehe 6/ 04/2021 Rais Mhe. Samia Suluhu alitoa maagizo kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kuajiri walimu 6,000 haraka
No comments