Ukweli Kuhusu Alama ya Mnyama Inayosemwa Kwenye Biblia na Namba 666
(NB: maneno “alama”, “muhuri”, “ishara” au “dalili” ni visawe).
Ufunuo 13:16-17 “Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa masikini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake.”
Kwanini alama hii ni ya muhimu kuelewa? Kama ukitaka kuthibitisha kwamba kitu flani ni chako, au ukitaka kuonyesha kuwa wewe ni mmiliki wa kitu flani, au ukitaka kutia alama kitu flani kuwa chako, siku zote kutakuwa na vitu vitatu tofauti.
*. Jina lako.
*. Cheo chako.
*. Mahali unapomiliki.
Hivyo, kama mtu akitaka kuthibitisha kwamba kitu flani kimetoka kwake lazima athibitishe kama hivi:
*. Jina = John S Samweli
*. Cheo = Raisi
*. Anapomiliki = Tanzania
Kuna serikali mbinguni (Isa. 9:6), na alama au muhuri wa Mungu ni sheria yake. Angalia katikati ya amri kumi na utaona muhuri wa Mungu, “Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba;…” Kut. 20:11
JINA LAKE = BWANA (“Mimi ni BWANA; ndilo jina langu…” Isa. 42:8).CHEO CHAKE = MUUMBA (…BWANA…yeye aliyeziumba mbingu, na…nchi…” Isa. 42:5).ANAPOMILIKI = MBINGU NA NCHI (“Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA…” Zab. 24:1).
Hivyo, BWANA alipoziumba mbingu na nchi kwa siku sita, siku ya saba alipumzika ili kuweka alama au muhuri kwamba yeye ndiye aliyeziumba mbingu na nchi, kwa hiyo Sabato ni muhuri unaothibitisha kwamba BWANA:
Aliziumba mbingu na nchi.Alituumba sisi pamoja na vitu vingine vyote.Anamiliki mbingu na nchi, pamoja na vitu vyote vilivyomo.
Kwanini shetani anafanya bidii sana kuwaongoza watu wasiitambue Sabato? Ni kwa sababu shetani anataka kujifanya yeye kuwa kama muumba wa mbingu na nchi, hivyo anainaingiza alama yake ambayo ni kinyume na alama ya kweli ya Mungu. Sabato ni alama au muhuri wa Mungu, kwa hakika Mungu mwenye anathibitisha ukweli huu kwa kusema, “…Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote;…” Kut. 31:13. (Kumbuka! maneno ishara, muhuri, alama ni visawe, na yanaweza kutumika kwa kuyachanganya-changanya).
Njia rahisi na nyepesi ya kugundua alama ya mnyama, ni kutafuta kujua kwanza alama ya Mungu., harafu utaona kwamba alama ya mnyama ni kinyume na alama ya Mungu.
Ufunuo 7:2-3 “Nikaona malaika mwingine, akipanda kutoka mawio ya jua, mwenye mhuri wa Mungu aliye hai; akawapigia kelele kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari, akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao.”
Kama tulivyoona huko nyuma kwamba muhuri na alama ni visawe! Hivyo watumwa wa Mungu wanawekwa alama katika vipaji vyao vya nyuso, kipaji cha uso hapa humaanisha akili, mawazo, au nia.
Wabrania 10:16 “Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika…”
Pia Wanafisikolojia hutuambia kuwa ubongo wa mbele wa cerebrum [paji la uso] ndipo shughuri kama uamuzi, hukumu, na uhuru wa kutaka vinapofanyikia. Hivyo, Wakristo wanawekwa alama katika vipaji vya nyuso zao, pale tu wanapomkubali Yesu kuwa Mwokozi wao na kutunza amri kumi zote kwa kuhiari, au kutaka wao wenyewe bila kulazimishwa. Hii ndiyo maana muhuri au alama ya Mungu haiwekwi mkononi, kwa sababu Yesu hatawalazimisha watu kumwabudu na kuzitii amri zake. Mkono humaanisha kulazimishwa kufanya kitu furani kinyume na nia zetu.
Jeremia 38:23 “Na watawatoa wake zako, na watoto wako wote, na kuwachukua kwa Wakaldayo; wala wewe hutapona na mikono yao, bali utakamatwa kwa mkono wa mfalme wa Babeli, nawe utakuwa sababu ya kuteketezwa kwa mji huu.”
Yesu kamwe hatatulazimisha sisi kumwabudu, kwani anapendezwa kama tutamwabudu na kutunza sheria zake zote, kwa hiari yetu bila kulazimishwa.
Ufunuo 13:15-17 “Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe. Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake.”
Alama ya mnyama inawekwa katika kipaji cha uso na kwenye mkono. Hivyo wale wote wanaokubali kwa hiari yao wenyewe kumfuata mnyama na kutii amri zake, hawa wamewekwa alama kwenye paji la uso; maana wamehiari wao wenyewe bila kulazimishwa. Na wale wanaopokea alama kwenye mkono, ni wale watakaotii amri za mnyama kwa kulazimishwa bila ridhaa yao. Kwa hofu ya kifo na kushindwa kununua wala kuuza, wanaamua kumtii mnyama ili wasipoteze vitu walivyovifanyia juhudi nyingi katika maisha yao na hili ni bonge la kosa.
Kwa sababu tumeelewa kwamba kuamua kumkubali Yesu kama Mwokozi wetu na kutunza mafundisho na amri zake zote, ni sawa na kupokea alama au muhuri wa Mungu. Tunatakiwa pia tuelewe kuwa kukubali amri, mafundisho, au mapokeo ya kanisa la Romani Katoliki au kanisa lingine lolote linalofuata imani ile ile na kufundisha mapokeo yake, inamaanisha tumepokea alama ya mnyama. Pia elewa kuwa kutakuwa na wengine ambao sio Wakatoliki lakini wanafanya kila kitu ambacho mnyama anaamru kwa kuogopa kufa, au kupoteza mahitaji ya kawaida kwa kuzuiliwa kuuza wala kununua, kitu ambacho kitapelekea kukubali kufuata matakwa ya mnyama. Hawa watapokea alama ya mnyama kwenye mkono kwa sababu wamelazimishwa kinyume na matakwa yao. Wakatoliki na Wakristo wengine ambao hukubali haya “mafundisho ya wanadamu” watakuwa wamepokea alama ya mnyama kwenye vipaji vya nyuso zao kwa sababu wamekubali kwa hiari kuwa kanisa lao liko sawa kwa kubadili maandiko na kuingiza “mapokeo” au “mafundisho ya wanadamu.” Na hii ilionywa katika unabii.
Wakolosai 2:8 “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”
Hivyo, kama ukipokea “alama” kwa kuchagua mwenyewe, hii inamaanisha umewekwa alama kwenye kipaji cha uso. Na kama ukipokea “alama” kwa kulazimisha, hii inamaanisha umewekwa alama kenye mkono wa kulia. Lakini kumbuka.
Mathayo 16:25 “Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.”
Mathayo 10:39 “Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.”
Yohana 12:25 “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.”
Tukirudi kwenye alama ya mnyama kanisa la Romani Katoliki bila ya kutambua linatimiza unabii huu kwa maelezo yafuatayo.
“Bila shaka kanisa la katoliki hudai kuwa badiliko, (la Sabato Jumamosi kwenda Jumapili) ilikuwa ni kitendo chake…na kitendo hicho ni ALAMA ya mamlaka yake katika mambo ya kidini.” –-H.F. Thomas, Chancellor of Cardinal Gibbons
“Jumapili ni ALAMA yetu ya mamlaka…kanisa liko juu ya Biblia, na uhamishaji huu wa utunzaji wa Sabato ni ushahidi wa jambo hilo la ukweli.” -–Catholic Record of London, Ontario Sept 1, 1923.
Kama unabii uko sawa unaposema jumapili ni alama ya mnyama, na Mungu anasema wazi wazi.
Kutoka 31:13 “…Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi.”
Ezekieli 20:12, 20 “Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua yakuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye…zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua yakuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.”
Maneno ishara, muhuri, na alama ni visawe, na yanaweza kutumika popote kwa kuyabadilisha-badilisha.
Hivyo, tuna uhakika wa ukweli wa Biblia kwamba Sabato ni ishara, muhuri, au alama ya Mungu. Na jumapili ni ishara, muhuri, au alama ya mnyama.
Imeandikwa na Aroon/JF
No comments