Kunenge atoa onyo kwa Viongozi wa Mitaa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge amewataka Viongozi ngazi za Mitaa kuhakikisha wanashughulikia ipasavyo kero na changamoto mbalimbali kwenye mitaa yao na kuhakikisha wanatoa taarifa mapema pale wanapobaini jambo lipo juu ya uwezo wao ili liweze kushughulikiwa na ngazi za juu.
Kunenge amesema hayo wakati wa kikao chake na Watendaji na Wenyeviti wa mitaa Jijini humo ambapo amesema ni jambo la fedheha kuona kiongozi wa ngazi ya juu anashughulikia kero ya mtaa wakati wahusika wa ngazi ya mtaa wapo wanapeta.
Aidha amewaelekeza Watendaji wa Mkoa huo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ambapo amesisitiza ukusanyaji wa Mapato usiwe wa kero wala wa kuua biashara za watu.
Pia, amewataka Viongozi wa Mitaa kusimamia ipasavyo suala la usafi wa mazingira kwenye mitaa yao ili kuwakinga wananchi na magonjwa ya Mlipuko.
Pamoja na hayo Kunenge amewasisitiza pia Viongozi hao kutoa taarifa pindi wanapobaini uwepo wa watu wanaohatarisha usalama ikiwemo kufichua nyumba zinazogeuzwa Madanguro, wanaowahifadhi wahamiaji haramu, wanaowatumia walemavu kujinufaisha na wauzaji wa dawa za kulevya.
Katika kikao hicho pia Kunenge amezielekeza Taasisi za umma zilizopo jijini humo kuhakikisha wanashirikiana na Watendaji wa Mitaa kwa kuwa hao ndio wapo karibu na wananchi na ndio wanaozijua zaidi kero za mtaa yao.
No comments