Hesabu za Simba dhidi ya AS Vita leo
Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa Afrika, klabu ya Simba SC itatupa karata yake ya kwanza kwenye mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya AS Vita, mchezo utakaochezwa leo saa 4:00 usiku huko Kinshasa Kongo, huu ni mchezo wa kundi A.
Huu ni mchezo wa kwanza wa Kundi A ambao utapigwa katika dimba la Stade des Martyrs jijini Kinshasa nchini DR Congo, timu hizi pia zilipangwa kundi moja, kundi D kwenye michuano hii msimu wa 2018-19. Mchezo wa kwanza Simba walifungwa mabao 5-0, nchini DR Congo na mchezo wa marejeano ambao ulipigwa jiji Dar es salaam Simba ilishinda kwa mabao 2-1.
Kocha wa Simba mfaransa Didier Gomes Da rosa amesafiri na kikosi cha wachezaji 27 huku wachezaji anaowakosa ambao hawajasafiri na timu ni nahodha John Bocco na Perfect Chikwende lakini pia kwa mujibu wa ripoti hakuna mchezaji mwenye majeruhi miongoni mwa wachezaji waliosafiri.
Simba wanakutana na AS Vita ambao wapo kwenye kiwango bora kwa sasa hawajapoteza mchezo hata mmoja kwenye michezo yao 24 ya mwisho kwenye mashindano yote, wameshinda michezo 16 na sare michezo 8 na mara ya mwisho kufungwa ilikuwa dhidi ya Raja Casablanca Januari 1, 2020, takribani mwaka mmoja umepita.
Simba wanacheza hatua ya makundi ya klabu bingwa Afrika kwa mara ya 3 katika historia ya klabu hiyo, na ni msimu wa pili wanafika hatua hii ndani ya misimu 3 ya mwisho, wekundu wa msimambazi wametinga hatua hii baada ya kuitoa FC Platinum ya Zimbabwe kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 kwenye mchezo wa hatua ya mtoano raundi ya kwanza.
Mchezo mwingine wa kundi hili utaikutanisha Al Ahly ya Misri ambao watakuwa wenyeji wa Al Merrikh ya Sudani mchezo utakao chezwa Februari 16.
No comments