Mfahamu Bilionea Wa Urusi Aliyefia Hotelini Z’bar, Alikuwa na Mwanamke Kabla ya Kifo Chake
Miongoni mwa habari zilizowashtua wengi katika msimu wa Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, ni kifo cha bilionea Igor Sosin (53), raia wa Urusi aliyekutwa amekufa hotelini visiwani Zanzibar, alikokwenda kwa mapumziko akiwa ameambatana na binti yake, Taisia (18).
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji, Sosin alikutwa amefariki usiku wa Desemba 23, 2020 katika chumba cha hoteli ya Park Hyatt iliyopo mtaa wa Mji Mkongwe mjini Unguja.
Mazingira ya kifo chake yamejawa na utata, kwani inaelezwa katika chumba alimofia, Sosin hakuwa peke yake.
Alikuwa na mwanamke wa Kitanzania, Arafa Ramadhan Mpondo (23), mkazi wa Fuoni Zanzibar ambaye inaelezwa kwamba alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi baada ya kufahamiana mtandaoni.
Kwa maelezo ya Arafa, inadaiwa kuwa siku ya tukio, majira ya saa 5:45 usiku, aligundua kwamba marehemu hakuwa vizuri kiafya lakini akaamua kulala naye mpaka asubuhi ili taratibu za matibabu zianze lakini kulipopambazuka, alijaribu kumuamsha bila mafanikio, alipoona haamki akaamua kutoa taarifa kwa uongozi wa hoteli na ndipo ilipobainika kwamba alishafariki dunia.
Kamanda Awadh anaeleza kwamba mwili wa marehemu ulipelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ambapo majibu ya awali ya uchunguzi wa kidaktari, yanaonesha kwamba bilionea huyo alikufa kifo cha kawaida lakini bado uchunguzi wa kina unaendelea kufanyika, huku Arafa akiendelea kushikiliwa na jeshi la polisi.
Msemaji wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Hassan Mcha Makame, alisema mwili wa marehemu umetolewa damu kwa uchunguzi wa kimaabara na tayari mwili huo umekabidhiwa kwa familia yake na tayari umesafirishwa kwenda nchini Urusi.
Gazeti la Daily Mail la Uingereza limeripoti kuhusu kifo cha bilionea huyo likieleza kuwa mapema mwaka huu aliugua na kupona ugonjwa wa corona na alipanga kusherehekea mwaka mpya akiwa visiwani Zanzibar.
No comments