Viongozi Simba, Yanga Watambiana Usajili wa Chama
KUPITIA mitandao mbalimbali ya kijamii viongozi wa Yanga na Simba wameendelea kutambiana juu ya usajili wa kiungo fundi wa Simba Clatous Chama ambaye mkataba wake na wekundu hao wa Msimbazi unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz kwenye ukurasa wake wa Instagram alichapisha picha ya jezi ya Chama huku akiwa ameikata na kuonekana namba 17 pekee ambayo ndio namba ya jezi anayovaa kiungo huyo na kuweka ujumbe uliosomeka hivi
"Tabia ya kutosema kweli huwa haidumu, hivi karibuni tutajua mbivu na mbichi," alimalizia kwa kumshukuru mkurugenzi wa uwekezaji wa kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wakuu wa timu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said pia mshauri wa mambo ya kiuongozi katika klabu hiyo Senzo Mazingisa.
Haikuishia hapo masaa machache baadae Ofisa Habari wa timu hiyo Hassan Bumbuli naye aliweka picha ya mchezaji wa Yanga, Farid Mussa na kuandika hiv;
"Tutalazimika kufanya mazungumzo na nyota wetu Farid Mussa juu ya Jezi no 17. Sijui naeleweka?" kauli hiyo ilitafsiriwa na wadau wa soka kuwa Yanga watalazimika kumshawishi nyota wao Farid Mussa kuachana na jezi namba 17 kwa lengo la kuimpa Chama akijiunga na wanajangwani hao kwakuwa ndio namba yake pendwa.
kauli ya tatu ilikua juu ya jibu la Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Yanga, Hersi Said kwa shabiki aliyemtania kuwa mkataba wa Mesut Ozil unaisha hivyo afanye mpango amsajili Yanga, Hersi akajibu kwa kuuliza yupi, Ozil wa Lusaka Zambia?
Mapicha picha hayo yametosha kuonesha mwanga kuwa Yanga wapo kwenye rada za kuinasa saini ya nyota wa Simba na timu ya Taifa ya Zambia Clotous Chama.
Pia upande wa pili (Simba), Ofisa habari wa klabu hiyo Haji Manara naye kupitia ukurasa wake wa Instagram alijibu mapigo kwa kuandika ujumbe huu
"Wanasimba Bad luck leo kazi zilikuwa nyingi sikuweza kuingia huku mitandaoni kwa muda mrefu.
Nimeona Utopolo wanaseti agenda kusudi ya kuitoa nchi kujadili maamuzi ya refa ya tarehe saba na kuzua uzushi wa kumsajili Clatous Chama, na ukitaka kuamini wanaseti agenda hii namna wanavyotumia nguvu kubwa kupitia watu wao na Waandishi (Maalum) kuaminishana huo UZUZU!! Katika Propaganda tunaita Qiurew Sicouse Propaganda, Guys Chama ni mchezaji wa Simba na dili yake ndio vileeeeeeeeeee!!" aliandika manara.
Tambo hizo ni kuelekea dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15 mwaka huu.
No comments