Majaliwa Athibitishwa na Bunge Zima Kuwa Waziri Mkuu
MBUNGE wa Ruangwa, Kassim Majaliwa Majaliwa amethibitishwa kwa kupigiwa kura za NDIYO wabunge wote 350 waliyokuwemo Bungeni leo Alhamisi, Novemba 12, 2020 na kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mhula wa pili mfululizo.
Awali, Rais Dkt. John Magufuli baada ya kumpendekeza, kupitia kwa mpambe wake, aliwasilisha Bungeni jina la Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kura zilizopigwa 350, hakuna kura ya Hapana wala hakuna kura iliyoharibika, hivyo Majaliwa ameshinda kura zote 350 ambazo ni sawa na asilimia 100.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Mahaliwa amesema; “Nimpongeze sana Rais Magufuli kwa ushindi mkubwa alioupata kutoka kwa Watanzania, kupitia uchaguzi tulioufanya ambao ameshinda kwa kishindo wenye imani kubwa ya Watanzania, kupitia uchaguzi uliofanyika kwa uhuru na haki.
“Jambo hili si dogo najua Mungu ameliongoza, namshukuru sana Rais @MagufuliJP kwa imani yake kubwa aliyonayo juu yangu na kuendelea kuniamini kama naweza kufanya hayo niliyoyafanya katika kipindi cha miaka 5 au zaidi kwa kipindi kijacho, nimshukuru sana.
“Niendelee kushukuru kwa kweli mmenifanyia jambo kubwa kwangu na familia yangu, idadi ya kura zenu nimefarijika, nawashukuru sana wabunge wenzangu nawashukuru hivi sababu najua tunao wabunge wa upinzani, kura 100% maana yake na wao wamepiga kura ya ndiyo.
“Niwaahidi nitapita kwenye maeneo yenu yote, kupata fursa ya kuona shughuli za maendeleo ambazo wabunge wenzangu mnazisimamia, nitafanya hivyo kwa majimbo yote ya CCM na kwa majimbo ya ndugu zetu vyama rafiki tukijua kuwa maendeleo hayana chama.
“Wote watakaopata uteuzi wa nafasi ya Waziri na Naibu Waziri wakiwa hapa, niwaahidi ingawa bado hawajachaguliwa kwamba tutawatumikia wabunge wote ili malengo ya serikali yaliyosheheni maendeleo yaweze kuwafikia Watanzania popote walipo,” amesema Majaliwa.
No comments