Mwalimu Matatani Ulawiti wa Wanafunzi 24
KIJANA Arnold Mlay almaarufu Big (31), mkazi wa Semtema A, Manispaa ya Iringa, ameingia matatani baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la ukatili wa kijinsia (ulawiti) wa wanafunzi 24 wa kiume kwa muda wa miaka mitatu.
Big ambaye ni mwalimu kiweledi amekutana na adhabu hiyo wiki iliyopita kulingana na Sheria ya Makosa ya Jinai kifungu namba 154, kifungu kidogo cha kwanza na cha pili cha kanuni ya adhabu.
Hukumu hiyo ya Big ambayo Gazeti la UWAZI lilikuwa likiifuatilia kesi yake hatua kwa hatua tangu Desemba, mwaka jana, inakuja baada ya kusikilizwa kwa mashahidi wakiwemo wazazi, marafiki watoto wenyewe na daktari aliyethibitisha kuingiliwa.
RUFAA IPO WAZI
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Paul Mayolyo alisema kuwa, hukumu hiyo ipo wazi kwa mshtakiwa kukata rufaa.
TAHARUKI KUBWA
Desemba, mwaka jana, kuliibuka taharuki kubwa kwa wakazi wa Mtaa wa Semtema A kufuatia mwalimu huyo aliyekuwa akiwafundisha watoto hao masomo ya ziada (tuition) kudaiwa kuwanajisi wanafunzi wake hao.
KAMANDA WA WAKATI HUO
Aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa wa wakati huo, ACP Reinada Millanzi alikaririwa akisema kuwa, mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni kwa ajili ya uchunguzi wa kuwadhalilisha watoto hao wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 10 hadi 16 kwa nyakati tofauti nyumbani kwake.
Kamanda wa Milanzi alikaririwa akisema kuwa, mtuhumiwa huyo ni mhitimu wa Ualimu na alidaiwa kufundisha wanafunzi masomo ya ziada kwenye kibanda ambacho pia anakodisha miakanda ya video (DVD).
MKUU WA WILAYA AINGILIA KATI
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Richard Kasesela aliingilia kati na kutoa siku tatu kwa wananchi kutoa taarifa za watoto waliodhalilishwa ili watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria.
MKUTANO WA DHARURA
Disemba, mwaka jana, baadhi ya wazazi wa watoto 24 wanaodaiwa kulawitiwa na kijana huyo walifikisha kilio chao kwa mkuu huyo wa Wilaya ya Iringa Mjini baada ya mkutano wa dharura.
Katika mkutano huo, wazazi hao walisema kuwa Mlay ana kituo cha kuchezesha michezo ya watoto (games) ambapo kwa nyakati tofauti alitumia nafasi hiyo, kuwafanyia ukatili watoto wao.
Aidha, kutokana na hali hiyo, Kasesela aliunda kamati ya watu 10 ili kubaini watoto ambao walikuwa wamefanyiwa ukatili huo wa kijinsia.
KAMANDA WA SASA
Akizungumza na UWAZI mwishoni mwa wiki iliyopita juu ya hukumu hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Issa Suleman alisema kuwa, hukumu hiyo imetokana na uchunguzi dhabiti uliofanywa na Jeshi la Polisi baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo Desemba, mwaka jana.
Alisema kutokana na uchunguzi huo Jeshi la Polisi lilifungua majalada ya kesi sita na manne kati ya hayo sita, yalifikishwa mahakamani mnamo Februari, mwaka huu.
Alisema kuwa, kesi moja kati ya nne ilianza kusikilizwa Februari 27, mwaka huu na kuita mashahidi mbalimbali tisa kutoa ushahidi wao mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa.
“Novemba 11 mwaka huu, mahakama imetoa hukumu kwa mhalifu huyo baada ya kumtia hatiani kisha kumhukumu kifungo cha Maisha jela. Kesi nyingine tano tunaendelea kuzisimamia kuhakikisha haki inapatikana,” alisema kamanda huyo.
MATUKIO YA UKATILI
Alisema kuwa, matukio ya ukatili bado yapo Iringa, lakini Jeshi la Polisi linaendelea kuyadhibiti.
“Tunaomba wananchi waondoe hali ya kumuonea huruma mtu, hata kama ni ndugu yao akitenda uhalifu wamripoti kwenye vyombo vya dola badala ya kumalizana hukohuko,” alisema.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Iringa Mjini waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa, hukumu hiyo ni funzo kwa mtu mwingine yeyote mwenye hulka kama za mwalimu huyo.
RIPOTI YA MATUKIO
Matukio ya ukatili dhidi ya watoto yameendelea kuripotiwa kwenye kona mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, bado ukatili wa kingono hasa ubakaji na ulawiti wa watoto ni changamoto kubwa nchini.
“Jitihada za kupambana na ukatili huo zinahitajika zaidi ili kusaidia kuondokana na ukatili huo ambao unawaathiri watoto kisaikolojia,” anasema Anna.
No comments