Waliotumia jina la Janeth Magufuli kutapeli waamriwa kulipa Milioni 16
Leo September 11, 2020 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, DSM imewahukumu watu wawili kulipa fidia Milioni 16, baada ya kukiri kutumia jina la Janeth Magufuli kutapeli.
Washitakiwa hao ni Masse Uledi (43) na Nkinda Shekalage (34). Mahakama pia imewahukumu kutumikia kifungo cha nje cha miezi saba kwa masharti ya kutotenda kosa lolote la jinai kwa muda huo.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando alisema Mahakama inawatia hatiani washitakiwa kwa kukiri makosa wenyewe, baada ya kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Alisema Mahakama inawataka washitakiwa kulipa fidia ya kutaifisha vifaa walivyokuwa wakivitumia kufanyia utapeli huo, ambavyo ni simu 12, kompyuta mpakato mbili, flashdisk tatu na modemu mbili kuwa mali ya serikali.
Wakili wa Serikali, Ladislaus Kimanga alidai washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na makosa matatu, likiwemo la kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Baada ya kuingia makubaliano, mashitaka mawili dhidi yao yalifutwa na kusomewa mashitaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
No comments