Header Ads

Header ADS

RAIS NKURUNZIZA: Kocha aliyehukumiwa kifo akaangukia URAIS, vita na mapenzi – Makala



Sio kila aliyelala na bundi huamka na mikosi, ndio sababu Pierre Nkurunziza aliyekuwa mkufunzi wa mpira wa miguu aliangukia urais wa Burundi baada ya kujikwaa kwenye kisiki cha hukumu ya kifo iliyofuatiwa na majaribio ya kuuawa akiwa mafichoni. Hata hivyo, kwakuwa kifo ni fumbo hakukiona kilipokuja rasmi kumchukua.

Alizaliwa Desemba 18, 1964 jijini Bujumbura, miaka miwili tu tangu Wakoloni Wabelgiji walipoiacha huru Burundi. Alikuwa sehemu ya tunda la juhudi za uhuru wa Burundi. Baba yake, Eustache Ngabisha alikuwa mwanasiasa aliyekuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa nchi hiyo. Mzee Ngabisha alikuwa Mhutu aliyemuoa mrembo Mtutsi ambaye ni mama yake Pierre. Mzee Ngabisha alikuwa mwanachama wa chama cha Union for National Progress, maarufu kama UPRONA. Hiki ndicho chama kilichowaletea warundi uhuru. Kwa kiasi kikubwa kilikuwa na Wahutu. Mzee huyu alipata nafasi ya kuwa Mbunge na Gavana wa majimbo ya Ngozi na Kayanza, kuanzia mwaka 1965.

Pierre, aliyezaliwa na baba Mhutu na mama Mtutsi alionja chungu ya siasa za chuki akiwa mtoto mwenye umri wa miaka nane tu. Baba yake alikamatwa na kuuawa kwa kunyongwa na tai akiwa gerezani mwaka 1972. Ilikuwa kipindi cha mauaji ya halaiki. Yaliyotokana na vita ya kikabila, ya Wahut una Watutsi. Mauaji hayo yaliyofanywa na wanajeshi, wakati huo jeshi lilikuwa na Wa-Tutsi wengi zaidi. Inaelezwa kuwa takribani watu 200,000 waliuawa.

Hata hivyo, maisha ya utotoni ya Pierre hayakuwa na kelele za namna yoyote ya uwanaharakati. Huenda ndio sababu kuu ya kumpa mazingira mazuri ya kupaa. Alipenda sana mpira wa miguu na michezo. Inaelezwa kuwa alianza kusakata kabumbu na kung’aa mtaani akiwa na umri wa miaka mitano tu. Walimpa jina la ‘Pita’.

Alisomea elimu ya michezo. Baadaye alikuwa mwalimu na mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Burundi. Hakuwahi kuliacha soka. Aliwahi kuwa kocha wa timu kadhaa za mpira wa miguu ikiwa ni pamoja na Mizinga FC. Hata alipokuwa Rais, aliendelea kucheza soka na wananchi wake.

Mwaka 1993, akiwa anafundisha Chuo Kikuu, Burundi iliingia kwenye kiza kinene baada ya Rais mpya aliyekuwa amechaguliwa kidemokrasia, Melchior Ndadaye kupinduliwa na kuuawa kikatili. Wanajeshi walioasi ikiwa ni pamoja na makomando wa kikosi cha pili cha jeshi la nchi hiyo, walivamia Ikulu Oktoba 20, 1993 na kumkamata. Walimkabidhi kwa askari wadogo na kuwaamuru wamuue. Askari hao walimchoma visu mara 14 na kumnyonga. Ilikuwa siku ya 104 tu tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa kidemokrasia tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa Wabelgiji.

Alikuwa Rais wa watu, aliyewatengenezea njia Warundi kupata amani na kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ni Mhutu aliyeingia madarakani tu na kumchagua Waziri Mkuu Mtusi. Ili kuhakikisha anawaleta Warundi pamoja, aliwapa wapinzani wake katika ulingo wa siasa theluthi moja ya nafasi kwenye Baraza la Mawaziri. Walipokula naye wakashiba wakamlipa kifo cha kikatili.

Ripoti ilieleza kuwa baada ya kumuua Rais Ndadaye, waliwaua pia viongozi wengi wa ngazi za juu. Baadaye walichimba shimo kubwa na kuwazika kwa pamoja Rais Ndadaye, Spika wa Bunge, Pontien Karibwami, Naibu Spika wa Bunge, Gilles Bimazubute, Waziri wa Mambo ya Ndani, Juvénal Ndayikeza na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Richard Ndikumwami.

Hata hivyo, baada ya kushauriana, waligundua kuwa Jumuiya za Kimataifa zingewaandama kwa mazishi yasiyo na heshima na mauaji ya kikatili. Hivyo, wanajeshi hao wakawafukua tena na kukabidhi miili kwa familia za viongozi hao.

Matukio hayo yalichochea moto wa kuanza kwa vita kali ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu hadi Mei 15, 2005. Juhudi za kuzima moto wa vita ya Burundi zilipewa nguvu na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Baada ya kufariki mwaka 1999, mzee Nelson Mandela alimpokea kijiti na kuendeleza mazungumzo ya kupata amani yaliyofanyika Jijini Arusha.

Nikurudishe kwa Nkuruziza aliyekuwa anafundisha Chuo Kikuu, miaka ya 1993. Baada ya kuzuka kwa mauaji hayo, mamia ya wanafunzi Wahutu waliuawa. Nkurunziza alikimbia, akatimkia msituni akiwa na Wahutu wenzake. Huko alibadili gia angani.

Wewe vita visikie tu kwenye radio. Vita haina macho na haichagui silaha. Wakati wa vita viwanja vya mpira havina kazi. Hivyo, Nkurunziza akajiajiri kwenye uwanja wa vita akiwa mhanga tayari kwani baba yake aliuawa na Watutsi, ambao kiuhalisia ni wajomba zake.

Nkurunziza ambaye ni kati ya watoto saba katika familia yao, ndugu zake watano waliuawa tangu kuanza kwa mauaji hayo hadi amani ilipopatikana. Hivyo, alipoteza baba mzazi na ndugu zake wa damu watano kwa sababu za machafuko.

Hatua ya kukimbilia msituni ilimtenganisha na mrembo,      Denise Bucumi, aliyekuwa amemuoa mwaka 1994 katikati ya mauaji ya halaiki. Hapo ndio utafahamu kwanini kwenye filamu za kivita msituni huwa kuna vipande vya mapenzi. Ni kwa sababu mapenzi ndiyo yanafanya dunia ijizungushe yenyewe kwenye mhimili wake… Ndiyo, hii ni sayansi ya mapenzi sio Jografia. Ndio maana kuna stori nyingi za watu waliowapata wake zao vitani.

Wakati Nkurunziza anaamua kukimbilia msituni, alimuacha mkewe akiwa na mtoto mdogo na ujauzito wenye umri wa miezi minne tu.

Akiwa msituni, Nkurunziza alijiunga na kundi la waasi waliojiita ‘CNDD–FDD’, ambalo liliundwa na Wahutu wengi. Alijiunga katika kikundi hicho pamoja na ndugu zake. Hivyo, mwaka 1998, Serikali iliyokuwa madarakani ilimfungulia mashtaka na kumkuta na hatia ya uhaini. Ikamhukumu kifo ingawa hakuwahi kufika mahakamani. Hivyo, alisubiri kukamatwa na kutumikia adhabu yake ambayo ni kifo. Mkewe aliyekuwa nchini Burundi, aliishi maisha ya kunyanyaswa na kuchukiwa sana kwa kuwa alikuwa mke wa muasi.

Akiwa hana msaada wa binadamu. Katikati ya manyanyaso, mke wa Nkurunziza aliamua kutubu dhambi na kumpokea Yesu Kristo. Akajiunga na imani maarufu ya ‘kilokole’ (Born again). Akaishi na imani akimuombea sana mumewe aliyekuwa msituni. Akawa mwimba kwaya, mhubiri na mwalimu wa Injili.

Adhabu ya kifo haikumnyong’onyeza, ilimpa nguvu zaidi Nkurunziza aliyekuwa msituni. Huko alianza kupanda vyeo kwenye chama chake cha CNDD-FDD. Mwaka huo wa 1998, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho. Mwaka 2001, alipanda na akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama.

Hata hivyo, siasa zina mengi. Hii ndio sababu wajuzi wa mambo wanasema ukipanga safari na mwanasiasa uwe na nauli mbili, kwa sababu anaweza kubadilika muda wowote… uwe na uwezo wa kupanda basi lingine na kuendelea na safari. Mwaka 2004, bundi aliingia kwenye chama hicho, kukawa na mgawanyiko. Lakini Agosti 2004, Nkurunziza alichangia kutuliza mpasuko na alichaguliwa tena kuwa Mwenyekiti. Na mwaka 2000 alitangazwa kuwa Rais wa CNDD-FDD.

Usione mtu kapanda tu vyeo katikati ya vita ukadhani alikuwa anakula ‘bata’ tu, lazima upishane na risasi kwakuwa unavyozidi kupanda unazidi kuwa ‘mlengwa mkuu’ wa adui zako. Mwaka 2001, Nkurunziza alinusurika kuuawa katika eneo la Gitega. Ndugu zake wa damu watatu waliuawa wakati wa mapambano ya CNDD-FDD. Hivyo, jumla alipoteza ndugu watano kwenye familia yake kupitia vita hiyo.

Baadaye alitangaza rasmi kuwa ameokoka, akawa mlokole wa kiplotestant kama mkewe. Maombi ya mkewe yakaendelea kuzaa matunda. Biblia inasema, ‘enyi wanawake waombeeni waume zenu waishi kwa namna ya kumpendeza Mungu’. Dada yangu mpedwa, muombee mumeo sio kumsema vibaya kwa mashosti na ndugu zako.


Nkurunziza akaweka nguvu kuwashawishi wanachama wenzake wa Kihutu kukubali Watutsi wajiunga na chama hicho, ili kiwe na sura ya kitaifa badala ya kuwa na sura ya kikabila.

Alianza kufanikiwa, kuanzia mwaka 2003, yalianza mazungumzo na upande wa Serikali, CNDD-FDD wakaingia kama chama cha siasa cha kitaifa. Hapo ikamsaidia Nkurunziza kuungana tena na mkewe na familia yake.

Baada ya mazungumzo ya amani, upande wa Serikali na Waasi wa walikubali kushirikiana na kuzima vuguguvu la vita. Wakaanza kuunda Serikali shirikishi. Nkurunziza aliteuliwa kuwa Waziri wa Utawala Bora kwenye Serikali ya Rais Domitien Ndayizeye. Ile hukumu ya kifo aliyopewa mwaka 1998 na Mahakama ikafutiliwa mbali.  Mwaka 2004, alichaguliwa tena kuwa Rais wa CNDD-FDD ambacho sasa kilikuwa chama rasmi cha upinzani; na akachaguliwa sasa kuwa mgombea Urais wa Burundi.

Mei 2005, vita ya kikabila nchini humo ilimalizika rasmi. Asante kwa Tanzania. Juhudi alizozianzisha na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na baadaye Mzee Nelson Mandela pamoja na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuongeza nguvu, zilizaa matunda.

Burundi ilifanya uchaguzi wa kidemokrasia kati ya Juni na Julai, 2005. Nkurunziza akiwa mgombea kupitia CNDD-FDD alichaguliwa rasmi kwa kura zilizopigwa na Wabunge pekee kuwa Rais wa Burundi. Aliingia rasmi Ikulu Agosti 26, 2005, hadi Juni 8, 2020 alipofariki dunia kwa mshtuko wa moyo, akisubiri kukabidhi rasmi kijiti cha Urais kwa Rais mteule, Evariste Ndayishimiye. Alipoingia tu ikulu, alimteua pia mkewe kuwa Waziri, nafasi aliyoishika hadi leo.

Nkurunzinza, aliiongoza Burundi kwa kipindi cha mihula miwili ya mwazo (2005-2010 na 2010 -2015). Kumbuka mwaka 2010, Nkurunziza alishinda kwa kishindo cha 91%, baada ya wapinzani wake kususia uchaguzi.

 Hali ilibadilika ghafla ilipotangazwa kuwa Nkurunziza atagombea tena mwaka 2015 kwa ajili ya muhula wa tatu. Wapinzani wake walipinga vikali hatua hiyo wakisema ni kinyume cha Katiba hiyo inayotoa nafasi ya mihula miwili tu ya Urais. Serikali ilitetea uamuzi huo ikieleza kuwa muhula wa kwanza wa Nkurunziza hauhesabiki kwani alichaguliwa na Bunge na sio kura za wananchi kama Katiba iliyopo inavyoelekeza.


Aprili 26, 2015 mwaka huo, maandamano ya kupinga uamuzi wa Nkurunziza yaliitishwa na wapinzani wake. Maandamano hayo yalizua vurugu kubwa kati ya waandamanaji na vyombo vya dola, na pia kati ya wanaopinga na wanaounga mkono uamuzi wa Rais Nkurunziza. Inaelezwa kuwa zaidi ya watu 24,000 waliikimbia Burundi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tu, kwa mujibu wa Wakala wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia Wakimbizi.

Hali iliendelea kuwa tete nchini humo, upinzani wa kisiasa ukazaa uasi. Mei 13, 2015 Rais Nkurunziza akiwa nchini Tanzania kuhudhuria mkutano na viongozi wengine wa Afrika, Jenerali wa Jeshi la Burundi, Godefroid Niyombareh alitangaza kuwa kupitia radio kuwa wameipindua Serikali ya Nkurunziza. Alikuwa ameondolewa kwenye kitengo cha Usalama wa Taifa miezi mitatu iliyopita.

Nkurunziza alijaribu kurejea nchini humo baada ya Serikali yake kutangaza kuwa wamezima jaribio la mapinduzi, lakini ndege yake ilishindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bujumbura kwakuwa ulikuwa umeshikiliwa na wanajeshi walioasi.

Hata hivyo, saa chache baadaye katika siku hiyohiyo, Nkurunziza alitangaza kuwa ameingia Burundi. Waliofanya jaribio la mapinduzi walikiona cha mtemakuni.

Maisha yalirejea kama kawaida, uchaguzi ulipoitishwa Julai 21, 2015, Nkurunziza alishinda kwa 69.41%, mpinzani wake, Agathon Rwasa alipata 18.99% ingawa alitangaza kutoshiriki. Wapinzani waliususia, chama tawala kikaona ‘ukisusa wenzio twala’. Wakala na kukomba sahani, maisha yakaendelea.

Alipokuwa anaapishwa, Agosti 20, 2015 kuwa Rais wa Burundi kwa kipindi kingine cha miaka mitano, aliwatangazia kiama waliotaka kuleta machafuko nchini humo. Alisema ‘watapigika kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na watatawanyika kama punje za unga zilizotupwa hewani’. Eti, kwanini asiwachakaze waliotaka kurejesha machungu ya kuwapoteza ndugu zake wa damu watano kwenye machafuko ya vita ya kikabila, na damu nyingi za Warundi? Inaelezwa kuwa watu 215,000 waliikimbia Burundi wakati Serikali ikiwasafisha waliotaka kuipoteza tena amani ya Burundi.

Yapo mengi mazuri ya kijamii aliyoyafanya Pierre Nkurunziza. Akiwa Waziri, mwaka 2004, alianzisha Academy ya mpira wa miguu ambayo ilitunza vipaji zaidi ya 300 nchini kote. Akiwa Rais, aliendelea kuhamasisha michezo kwa vitendo. Alikusanya wachezaji wenzake wa zamani (maveterani), wakaunda kikosi cha Hlleluia FC. Wakawa wanakipiga kama kawaida.

Fikiria, unapocheza soka na Rais wa nchi, unapaswa kuwa na adabu eeeh. Sasa Februari 3, 2018, iliripotiwa kuwa maafisa wawili wa Serikali walitupwa jela baada ya mechi kati ya timu aliyokuwa anachezea Nkurunziza na timu yao. Maafisa hao walidaiwa kumchezea madhambi (rough) makusudi Mheshimiwa Rais na kumfanya aanguke mara kadhaa. Hata hivyo, Rais Nkurunziza alifanikiwa kufunga goli kwenye mechi hiyo. Wazee wa kupinga kila kitu wakasema ‘ameachiwa goli afunge’. Duuh! Kama ni hivyo si angefunga magoli 100.

Wanasema bahari tulivu haimpimi nahodha. Nkurunziza alipewa meli ya Burundi iliyokuwa kwenye misukosuko mingi ya kivita na mauaji ya halaiki. Akaidhibiti na kuivusha licha ya kelele nyingi za kimfumo.

Nkurunziza, amefariki ghafla Juni 8, 2020 na kifo chake kikatangazwa Juni 9, 2020. Lakini ameacha alama kubwa. Ametunukiwa tuzo nyingi na jumuiya za kimataifa, ingawa alikuwa anapigwa vita sana na vyombo vya habari vya kimataifa na zaidi waafrika wenzake. Nabii hana heshima kwao, imesema Biblia Takatifu.

Kwa wanaothamini alipoitoa Burundi, kwenye shimo la vita lililowashinda marais nane waliomtangulia, walimpa tuzo nyingi za amani.

Mfano: Mwaka 2010, Taasisi ya Kimataifa ya India (Unity International Foundation), ilimpa tuzo Nyota ya Afrika inayong’aa, baada ya Mamlaka za India kumtambua kama kiongozi wa mfano katika kuleta amani na maendeleo kwa Afrika. Na Oktoba 2011 Taasisi ya Kimataifa ya masuala ya amani, ya ‘Peace and Sports International Organization’, ilimtunuku tuzo kwa jinsi alivyotumia michezo kama nyenzo ya kuleta amani na utulivu nchini kwake. Mkewe pia amepokea tuzo nyingi za kimataifa kwa kuwa mfano mzuri kwa jamii.


Denise Nkurunziza alipokea tuzo tatu kutoka kwa mashirika manne ya kimataifa kwa kuwa mfano mzuri kwenye jamii, Septemba, 2019. Mashirika hayo ni “Global Visionary Publishing”, “iChange Nations”, “Purses Pumps and Power Network”, na “Organization for Poverty Alleviator and Development (OPAD)
Kila mwenye kutenda mema kuna sehemu alijikwaa. Na doa huonekana zaidi kwenye vazi safi na tanashati. Alifanya yake duniani, Mungu amemchukua. Ameacha mjane akiwa amelazwa hospitalini jijini Nairobi nchini Kenya, na watoto sita. Tuwaombee na tuiombee Burundi na Rais mpya mteule, Evariste Ndayishimiye. 

Naamini mkewe anatumia maneno ya Biblia kujifariji. Naamini pia Nkurunziza kimoyomoyo alisema maneno haya yanayopatikana kwenye Biblia, Timetheo 4:7, “nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda.”

Nikuache na sahihi ya Nkurunziza, hii ukiweza kuigushi nakupa cheti cha diploma ya sanaa ya kunakili.


No comments

Powered by Blogger.