Mabosi Yanga SC Wamfungia Vioo Morrison
KWISHA jeuri yake! Ndivyo utakavyoweza kusema baada ya uongozi wa Yanga kupanga kumkomesha kiungo wao mshambuliaji Mghana, Bernard Morrison.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu kiungo huyo mwenye mbwembwe za kuupanda mpira, akanushe kuongezewa mkataba wa miaka miwili ya kuendelea kuitumikia Yanga.Mghana huyo hivi karibuni ilielezwa kuwa aliomba kuvunja mkataba huo kabla ya uongozi wa timu hiyo kugomea kwa kile kilichoelezwa kuwepo kwenye mipango ya kwenda kusaini Simba.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, uongozi na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Mbelgiji, Luc Eymael umepanga kutomtumia katika michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA baada ya kumaliza adhabu.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa lengo ni kumuonyeshea kiungo huyo hakuna mchezaji aliye juu ya timu, licha ya umuhimu mkubwa wa michezo hiyo waliyoibakisha ikiwemo FA.
Aliongeza kuwa kama akiendelea na ujeuri wake, basi kwenye msimu ujao atafanya mazoezi na timu yao ya vijana ya U20 iliyo chini ya kocha mzawa, Said Maulid.
“Labda abadilike ndiyo maamuzi yatabadilika lakini kwa kitendo ambacho amekifanya Morrison cha kukanusha kuwa hana mkataba wakati hivi karibuni alipewa wa miaka miwili na kuusaini.
“Kitendo hicho kimewakera viongozi wa Yanga na mabosi wa GSM ambao ndio waliofanikisha usajili wake katika usajili wa dirisha dogo, kitendo hicho wamekichukulia kama cha uchonganishi kati yao na mashabiki wa timu hiyo.
“Hivi sasa mabosi wa GSM hawataki kabisa kupokea simu za Morrison kutokana na kitendo hicho, yeye kama alikuwa anataka kuonekana angefuata taratibu za usajili ambazo zipo wazi ikiwemo hiyo klabu inayoonyesha nia ya kumhitaji kuwafuata na kukaa meza moja kujadiliana,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Injinia Hersi Said juzi alisema: “Niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwaambia kuwa, Morrison alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Yanga ambao ulisajiliwa TFF pamoja na Fifa.
“Kikubwa Morrison afahamu kuwa, hakuna mchezaji aliyepo juu ya timu, kama klabu tunasimamia misingi na kama kuna timu inamhitaji Morrison waje tukae meza moja tuzungumze, sisi tupo tayari kumuuza kwani hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu,” alisema Said.
No comments