Header Ads

Header ADS

Lukuvi Ataka Kila Mwenye Kiwanja Kuwa Na Hatimiliki



WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amemtaka kila mwananchi mwenye kiwanja hapa nchini kuhakikisha anakuwa na hati miliki ya kiwanja chake ili kuwa na ulinzi madhubuti wa eneo hilo. 

Alitoa mwito huo wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Ofisi ya Ardhi ya mkoa wa Singida iliyofanyika mjini hapa juzi. Alisema kuwa, kuwepo kwa mawe ( beacons) peke yake kwenye kiwanja sio ukamilifu wa kumiliki eneo, hivyo kuna umuhimu kwa kila mwenye kiwanja kuhakikisha anaomba na kupatiwa hati miliki, hatua ambayo ni kutimiza matakwa ya kisheria na kuongeza thamani ya eneo husika. 

“Hapa Singida tangu tupate uhuru mwaka 1961, viwanja zaidi ya 43,200 vimepimwa na kupewa wananchi lakini ni watu 6,300 tu ndio wenye hati miliki za maeneo yao na ndio wanaolipa kodi Serikalini. Wenye viwanja takriban 37,000 hawana hati miliki.

“Hali hii, mbali na kuisababishia serikali hasara kwa kuikosesha mapato pia inawanyima wenye viwanja hivyo fursa ya kujipatia mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha kwa kuwa bila hati miliki huwezi kupata mkopo hata kama nyumba yako ni ghorofa,” alisema. 

Waziri Lukuvi alisema kuwa hali hiyo huenda ilitokana na wenye viwanja kukutana na changamoto mbalimbali, ikiwemo urasimu wa watumishi na gharama za ufuatiliaji, ingawa pia sheria kwa siku za nyuma ilikuwa hailazimishi sana mtu kuwa na hatimiliki. 

“Sasa hiari hiyo imeondoka. Sheria inawataka mchukue hati; hivyo natoa siku 90 kwa kila mwenye kiwanja awe amepata hati miliki. Iwapo kila mmoja atatimiza masharti yote ya kuomba hati, ndani ya siku saba tu atapata hati miliki ya eneo lake bila hata kutoa rushwa,” alifafanua. 

Awali, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Singida, Speratus Ruteganya alimueleza waziri kuwa katika kutekeleza muundo mpya wa Wizara, mkoa unaendelea kuhimiza makampuni ya urasimishaji na upimaji kuhakikisha yanamaliza kazi zao ndani ya muda waliopewa.



No comments

Powered by Blogger.