Kiongozi wa Upinzani Malawi Ashinda Uchaguzi
Kiongozi wa upinzani nchini Malawi Lazarus Chakwera ameshinda uchaguzi wa wiki hii wa rais ulioamriwa kufanyika tena kwa asilimia 58.57 ya kura, tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imesema.
Malawi Opposition Lazarus Chakwera (Reuters/E, Chagara)
Ilikuwa ni mabadiliko makubwa ya majaaliwa kwa kiongozi aliyeko madarakani, Peter Mutharika, ambaye ushindi wake katika uchaguzi wa mwezi Mei 2019 ulibatilishwa na mahakama ya katiba, yakihusishwa na udanganyifu mkubwa.
Kiasi ya wapiga kura milioni 6.8 katika taifa hilo dogo la kusini mwa Afrika walijitokeza katika vituo vya kupigia kura siku ya Junanne. Na jana Jumamosi , tume ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Chifundo Kachale aliwaambia waandishi habari; “Tume imemtangaza Lazarus Chakwera , kwa kupata asilimia 58.57 ya kura, kuwa amechaguliwa kuwa rais wa Malawi.
Malawi Präsident Peter Mutharika PK Wahlen (picture-alliance/AP Photo/T. Chikondi)
Mutharika alikuwa wa pili kwa kupata kura 1,751,377, wakati mgombea ambaye hajulikani sana Peter Dominico Kuwani amepata kuwa 32,456.
Watu waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 64.81.
Tangazo hilo lilipokelewa kwa shangwe kubwa na vigelegele wakati waungaji mkono upinzani wakipepea bendera ya Malawi yenye rangi nyekundu , nyeusi na kijani na kuimba “serikali” katika lugha ya Kichechewa.
Mwezi Februari , mahakama ya juu ya Malawi iliona kuwa uchaguzi wa kwanza umegubikwa na mapungufu mengi , ikiwa ni pamoja na matumizi ya wino wa kufanyia marekebisho kubadilisha matokeo katika karatasi ya matokeo.
Ushindi kwa Wamalawi
Hukumu hiyo ya kihistoria imeifanya Malawi kuwa nchi ya pili ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara kubatilisha matokeo ya rais , baada ya Kenya mwaka 2017.
“Huu ni ushindi kwa Wamalawi , ni ushindi kwa demokrasia , ni ushindi kwa haki,” amesema Chakwera aliyechaguliwa baada ya ushindi wake kutangazwa.
“Ni ushindi ambao utaliwezesha taifa hili kuanza upya na kuanza kujenga aina mpya ya Malawi ambayo sisi wote tutahusika.”
Wakati huo huo , kundi la watu waliokuwa wakifurahia lilijikusanya kufyatua fashi fashi katika makao makuu ya chama cha Chakwera cha Malawi Congress Party katika mji mkuu Lilongwe.
Mutharika hakupenda kusema lolote juu ya kushindwa kwake.
Mapema jana Jumamosi , Mutharika alidai kuwa uchaguzi huo uliofanyika tena una mapungufu, akielezea kuhusu ghasia na kutishwa kwa waangalizi wa chama chake cha DPP.
“Hatuna maelezo zaidi ya kutoa,” msemaji wa Mutharika Mgeme Kalilani aliliambia shirika la habari la AFP baada ya matokeo. “Taarifa tuliyotoa mapema leo inatosha.”
Rais huyo anayeondoka madarakani wa chama cha Democratic Progressive Party DPP siku ya Ijumaa alitoa wito kwa tume ya uchaguzi ya Malawi kubatilisha matokeo ya kura ya pili na itangaze uchaguzi wa tatu.
No comments