Header Ads

Header ADS

Mfanyakazi TRA adaiwa kuuawa na mumuwe



MFANYABIASHARA na mkazi wa Mbweni Dar es Salaam, Isaya Mzava anadaiwa kumuua mke wake ambaye ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Irene Mzava na kutokomea kusikojulikana.

Irene ambaye alikuwa akihudumu TRA Tegeta kitengo cha magari, alifikwa na mauti juzi usiku wa kuamkia jana chumbani kwake ambako alikuwa amelala na mumewe.

HabariLEO lilifika nyumbani kwa Irene na kukuta ndugu, jamaa na marafiki wakiomboleza na mtoto wake Calvin Isaya alithibitisha kutokea kwa kifo cha mama yake na kueleza kuwa ilikuwa mapema kuzungumzia kifo hicho kwamba suala hilo linashughulikiwa na Polisi.

“Ni kweli mama amefariki dunia lakini siwezi kuzungumza lolote kwa sasa hadi pale uchunguzi utakapokamilika ndipo msemaji wa familia atazungumza, kwa sasa polisi wameshakuja kuanza uchunguzi,” alisema.


 
Hata hivyo, alipoulizwa kama baba yake yupo nyumbani alisema hayupo na hafahamu alipo baada ya kuamka asubuhi licha ya usiku kuthibitisha alilala nyumbani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Ramadhan Kingai alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa linafanyiwa uchunguzi na utakapokamilika umma utajulishwa.

“Ni kweli tuna taarifa ya tukio hilo la mume kudaiwa kumuua mkewe, polisi wetu wapo eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi, kati ya kesho (leo) au keshokutwa (kesho) majibu ya uchunguzi yatapatikana kuhusu kutoroka kwa mumewe kwani Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka huku uchunguzi nao ukiendelea,” alisema


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alithibitisha kuwa Irene ni mfanyakazi wa mamlaka hiyo na kwamba wapo kwenye majonzi kwa kuondokewa na mtumishi mwenzao.

“Taratibu za mazishi zinaandaliwa na familia kama ilivyo kwenye taratibu za kiutumishi tutashiriki,” alisema.


No comments

Powered by Blogger.