Mwanamke wa Afghanstan ajifungua ndani ya Ndege ya kijeshi ya Marekani wakati wakisafirishwa
Kutokana na vurugu zinazoendelea nchini Afghanstan imeelezwa kuwa mwanamke mmoja raia wa Afghanstan amejifungua mtoto wa kike ndani ya ndege ya jeshi ya Marekani wakati wa safari ya kuikimbia nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la anga la Marekani imeeleza kuwa mwanamke huyo alipata uchungu wakati ndege ikiwa njiani kuelekea Ramstein Air Base kambi ya jeshi hilo la Anga iliyopo nchini Ujerumani.
Taarifa inaendelea kusema kwamba wataalam wa afya waliokuwa ndani ya ndege hiyo ya kijeshi walimsaidia kujifungua salama.
Mpaka sasa jeshi la Marekani limewasafirisha raia 17,000 wa Afganistan wanaokimbia machafuko tangu wanamgambo wa Taliban kuuweka utawala wa nchi hiyo chini ya himaya, ikitarajiwa takribani raia 60,000 watapatiwa hadhi ya ukimbizi nchini Marekani na wengine katika mataifa mengine endapo watafikia makubaliano.
No comments