Lengai Ole Sabaya Asema Hakumbuki Kushitakiwa Kwa Kujifanya Usalama wa Taifa
Aliyekua mkuu wa wilaya ya HAI, Lengai Ole Sabaya ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa alikua akimiliki kihalali Bastola aina ya Glock 17 na kudai hakuwa nayo katika eneo ambalo anatuhumiwa kufanya kosa la unyanga'nyi wa kutumia silaha.
Akihojiwa na wakili wa serikali mkuu Tumaini Kweka ambaye alimuuliza Sabaya iwapo ana miliki silaha na ni silaha ya aina gani, ambapo Sabaya alieleza mahakama kuwa alikuwa anamiliki silaha hiyo kihalali kwa ajili ya ulinzi binafsi.
Wakili wa serikali mkuu alimuuliza Sabaya iwapo ana maadui, Sabaya alipojibu kuwa anao maadui na alianza kumiliki silaha hiyo tangu machi mwaka huu kwa ajili ya ulinzi binafsi kutokana na kutishiwa kuuwawa.
Sabaya aliulizwa kuwa kwenye ushahidi wake wa msingi alieleza Mahakama kuwa aliiacha silaha yake nyumbani Boma Ng'ombe wakati akielekea Arusha kutekeleza maelekezo kutoka kwenye mamlaka husika na alipoulizwa ni aina gani ya silaha uliiacha nyumbani.
Sabaya akajibu kuwa hawezi kuitaja aina ya silaha hiyo kwakuwa wakati anatoa ushahidi wake wa msingi hakuulizwa, Wakili kweka alimuuliza Sabaya kuwa wakati anatoka hai kuja Arusha na timu yake alipitia njia gani.
Sabaya alijibu kuwa alipitia barabara ya Kia- Mererani - Arusha.
Wakili aliuliza kwanini walipitia njia hiyo na asipite barabara kuu ya Arusha-Moshi, mshitakiwa huyo alijibu kuwa alichagua kupita njia hiyo kwa ajili ya usalama wake.
Pia aliulizwa kwanini ulikua unatishiwa kuuawa wakati alikua kiongozi serikalini na anatumikia wananchi.
Sabaya alijibu kuwa alitishiwa kuuawa kwa sababu ya majukumu aliyokuwa akiyafanya na kwasababu ya aina ya siasa za Arusha na Hai,
Sehemu ya Mahojiano....
Wakili: Katika ushahidi wako wa msingi umeieleza mahakama unamiliki silaha
Sabaya: ni sahihi
Wakili: Unamiliki silaha ya aina gani
Sabaya: Hakimu kwa sababu ni kifaa cha moto sijui kitatumikaje nikieleza kilivyo.
Wakili: Nataka kujua ni silaha
Sabaya: Kwa usalama wa silaha hiyo na kwa sababu nipo gerezani naomba nisieleze silaha gani. Ni silaha ndogo inaitwa Glock 17
Wakili: Ulianza kumiliki lini silaha?
Sabaya: Nilianza kuimiliki Machi 24, 2021
Wakili: Kwenye ushahidi wako wa msingi siku ukiondoka kuja Arusha Februari 9, 2021 uliacha silaha yako nyumbani Bomang'ombe.Ni sahihi siku ile ulikuwa ukimiliki silaha?
Sabaya: Sikuwahi kumiliki silaha ya moto kwa wakati huo nilikuwa na silaha ila haikuwa silaha ya moto
Wakili: Nilikusikia wakati unatoa ushahidi wako kuwa mamlaka ya utezi iliunda tume akaja Dk Bashiru na kesi iliyokuwa inakukabili mahakamani iliondolewa na DPP?
Shahidi: Ndiyo
Wakili: Ni sahihi ulifikishwa mahakamani kwa kosa la kujitambulisha wewe ni ofisa usalama wa Taifa ‘undercover’.
Shahidi: Sikumbuki.
Wakili: Shahidi ni sahihi kesi hiyo ya jinai ndiyo ilipeleka ukatenguliwa nafasi yako ya uenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha?
Shahidi: Siyo kweli
Wakili: Shahidi wa sita wa jamhuri (Bakari Msangi) aliieleza mahakama alikuwa mjumbe, wewe ukiwa mwenyekiti na moja ya sababu za kuondolewa ilikuwa ni kesi hiyo na tume iliundwa makao makuu?
Shahidi: Sikumbuki Bakari alisema nini kuhusu kutenguliwa, lakini hakueleza hayo.
Wakili: Kuanzia Julai 2018 hadi Mei 2021 ukiwa katika Wilaya ya Hai, ulikuwa ukifahamika kama mkuu wa wilaya?
Shahidi: Kila mtu alikuwa na namna yake ya kunitambua
Wakili: Hapa mahakamani kwa mara ya kwanza Julai 16, 2021 ulisomewa mashtaka matatu yanayokukabili?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Uliulizwa majukumu yako ya DC ni yapi?
Shahidi: Nilieleza majukumu ya DC kusimamia shughuli zote za maendeleo, kusimamia usalama na atatekeleza majukumu mengine yoyote atakayopewa na mamlaka iliyomteua
Wakili: Kwa hiyo utakubaliana pamoja na Katiba, sheria iliyokuwa inaongoza majukumu yako ni sheria inayosimamia Tawala za Mikoa?
Shahidi: Ni moja ya sheria hizo.
Wakili: Kwa mujibu wa sheria hiyo, ulikuwa unawajibika chini ya mkuu wa mkoa Kilimanjaro.
Shahidi: Sijaisoma hiyo sheria
Wakili: Kwa hiyo ulikuwa hujui unatekeleza majukumu yako chini ya seria gani?
Shahidi: Sijui.
Wakili: Uliapishwa tarehe ngapi kuwa mkuu wa wilaya?
Shahidi: Tarehe 1/ 8/2018
Wakili: Uliapishwa wapi na nani alikusimamia kula kiapo?
Shahidi: Nilikula kiapo mbele ya mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Wakili: Nani aliyekupa kiapo?
Shahidi: Simfahamu.
Wakili: Baada ya kuapa ulimfahamu alikuwa ni nani?
Shahidi: Dk Anna Elisha Mghwira
Wakili: Unaieleza mahakama ulikuwa humjui mkuu wa mkoa aliyekuwa anakuapisha ni nani.
Shahidi: Kwa wakati nimeshika biblia naapa, sikuwa namfahamu ila nilimfahamu baada ya kuapa.
Wakili: Mamlaka yako ya uteuzi kuwa DC ni nani wakati huo?
Shahidi: Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Wakili: Kama mamlaka iliyokuteua ni Rais kwa nini ulienda kuapa kwa mkuu wa mkoa?
Shahidi: Aliniapisha kwa niaba ya Rais.
Wakili: Kwa hiyo moja ya misingi hiyo uliapa mbele ya mkuu wa mkoa, hiyo inaonyesha majukumu yako ulitakiwa utekeleze kupitia yeye.
Shahidi: Yeye pamoja na wengine.
Baada ya upande wa jamhuri kumaliza kumhoji mshitakiwa huyo, wakili wa Sabaya, Moses Mahuna alimuuliza Sabaya maswali.
Mahuna alimuuliza Sabaya wakati anahojiwa na wakili msomi kweka alisema ulikua ikimiliki silaha, kihalali 24 machi na tarehe 9 feb 2021 alikuwa na silaha, Je, anaweza kufafanua hayo maelezo mawili.
Sabaya akajibu kuwa tarehe tisa alikua anamiliki silaha lakini hakuulizwa ni aina gani ya silaha.
Wakili mahuna alimuuliza Sabaya kuwa kwanini alisema hamkumbuki mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro aliyemuapisha na baadae baada ya madodoso ya wakili wa serikali akamtaja.
Sabaya akajibu kuwa wakili wa serikali kweka alijaribu kumchanganya na maswali yalikua yakipandana hata maswali mengine alikua hayasikii na hata tuhuma nyingine hazijui.
Kwa upande wake mshatakiwa wa pili Sylvester Nyegu alianza kutoa ushahidi wake akiongozwa kwa maswali na wakili wake Sylvester kahunduka ambapo alimuuliza silvester kuwa 9 feb 2021 kuanzia saa kumi na mbili asubuhi mpaka saa nne usiku alikua wapi Silvester akajibu alikua nyumbani Boma Ngo'mbe.
Wakili kahunduka alimuuliza Sylevester kuwa kuna mashahidi walikuja Mahakamani wakatoa ushahidi kuwa tarehe hiyo ulikua dukani kwa Mohamed Hajirin unanini cha kuiambia Mahakama.
Silvester alijibu kuwa ni uongo kwasababu hafahamu chochote na hapafahamu hapo ambapo mashahidi wamepataja.
Alipoulizwa kuwa katika mahakama hiyo anashtakiwa kushiriki kufanya vitendo vitatu vya unyang'anyi wa kutumia silaha katika duka la Mohamed Saad Hajirin.
Silvester aliieleza mahakama kuwa mashtaka hayo ni ya uongo, hayafahamu na hakuna shahidi yeyote aliyeletwa hapa mahakamani aliyesema kuwa amefanya kitu chochote katika mashtaka yote matatu kwamba yeye nimeiba hela milioni mbili na laki saba na elfu 69,kwamba amempiga mtu yeyote kati ya mashahidi hao.
Kwamba amemfunga pingu kwamba ameiba laki 3 na elfu 90 na kwamba ameiba 35 na simu ya Tecno Pop 1 na kuendelea kusisitiza mahakamani hapo kuwa mashtaka hayo ni ya uongo dhidi yake.
Kesi hiyo ya jinai namba 105 ya mwaka inayomkabili Sabaya na wenzake wawili inaendelea kunguruma Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na watuhumiwa wako katika Gereza Kuu Arusha kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana.
No comments