Msiende na Matokeo Yenu Kwenye Mechi ya Dabi
LEO Jumamosi shughuli ni moja tu, pale kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Temeke, jijini Dar ambapo mapacha wa Kariakoo watashuka dimbani majira ya saa 11:00 jioni kwenye vita ya dakika tisini kutafuta nani mbabe.
Hii ni mechi muhimu kwa timu zote mbili ambapo itatoa taswira ya ujumla kuelekea mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao upo chini ya utawala wa Simba kwa msimu wa tatu mfululizo.
Yanga ilikuwa kwenye kiwango bora mzunguko wa kwanza wakifanikiwa kuongoza ligi kwa muda mrefu kabla ya mambo kuwaendea ndivyo sivyo kwenye raundi ya pili ambapo walijikuta wanashushwa kileleni na watani zao Simba, hivyo unaona ni kwa namna gani mchezo huu ni muhimu kwa timu zote mbili.Simba wanahitaji kushinda ili wazidi kutanua wigo kuelekea mbio za ubingwa ambao unawaniwa kwa ukaribu na Azam FC walioko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Vikosi vya timu zote vimesheheni wachezaji ambao wanaweza kuamua matokeo ya mchezo huo muda wowote endapo wasipowekwa chini ya uangalizi wa walinzi kwa upande wa Simba wachezaji kama Clatous Chama, Luis Miquissone na Bernard Morrison ni miongoni mwa wachezaji hatari ambao wanaweza kubadilisha matokeo ya mchezo muda wowote.
Kwa upande wa Yanga wachezaji kama Saido Ntibazonkiza, Yacouba Sogne na Tuisila Kisinda pia ni miongoni mwa wachezaji ambao wanaweza kubadili matokeo ya mchezo muda wowote.
Hivyo basi ukiutazama mchezo huu kwa ukubwa wake unaona ni kwa namna gani timu iliyofanya maandalizi bora itakuwa na nafasi ya kuibuka na ushindi hii leo, Simba wanaingia kifua mbele kwenye mchezo huu ikiwa ni timu pekee iliyoshinda mechi nyingi kwenye ligi kuliko timu yoyote ambapo imeshinda jumla ya mechi 19 hadi sasa.
Yanga ikiwa chini ya kocha mpya Naserdinne Nabi imezidi kuimarika ambapo kwenye mechi mbili walizocheza chini ya kocha huyo wameshinda mechi moja na wamepoteza moja, kwa upande wa Simba ambayo ipo chini ya Mfaransa Didier Gomes haijapoteza mechi yoyote kwenye ligi hadi sasa kwenye mechi 10.
Mashabiki mnapaswa kutambua mpira wa miguu ni mchezo wa tofauti sana, tayari presha imekuwa kubwa nje ya uwanja ambapo kila shabiki anatamba kikosi chake kuibuka na matokeo kwenye mechi ya leo.
Mnapaswa kutambua kuwa mpira ni mchezo wenye matokeo ya kikatili sana, hivyo hampaswi kujipa asilimia mia moja kuwa timu zenu zitaibuka na ushindi ni lazima mtambue kuwa mpira una matokeo matatu na muwe tayari kuyapokea endapo mtakutana na moja ya matokeo hayo iwe ushindi, kufungwa au sare.Hatutarajii kuona mnakuwa sehemu ya uvunjifu wa amani kwenye mechi ya leo kisa tu matokeo ambayo mliyatarajia hamjayapata.
STORI NA BONIFACE PAWASA
No comments