Rais Samia: Nitadumisha Mazuri Yaliyopita na Kuleta Mapya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa dira na mwelekeo wa awamu ya sita itakuwa ni kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya.
Rais Samia ametoa kauli hiyo Aprili 22, 2021 wakati akilihutubia Bunge la Tanzania kwa mara ya kwanza tangu alipokuwa Rais pamoja na kutoa mwongozo wa serikali ya awamu ya sita.
“Naomba nieleze Bunge hili tukufu pamoja na Watanzania kuwa dira na mwelekeo wa awamu ya sita itakuwa ni kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya. Kimsingi ndio dhana na maana halisi ya kauli mbiu au salamu yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kazi iendelee, tutaenzi na kuendeleza mambo yote mazuri lakini pia tutafanya mabadiliko pale itakapobidi kwa lengo la kukuza ufanisi na tija,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa, “Nimekuja kulihutubia Bunge baada ya Nchi yetu kupita kwenye kipindi kigumu, kama inavyokumbukwa March 17 Taifa letu lilipata msiba mkubwa wa kuondokewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Magufuli,hivyo tusimame kumuombea Mpendwa wetu”.
Katika hatua nyingine amemshukuru aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dkt. John Magufuli kwa kumuamini na kumpendekeza kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi wa 2015 ambapo alipata nafasi ya kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke na hatimaye kuwa Rais.
“Kuniamini kwa Hayati Magufuli kuwa Mgombea Mwenza wake kumeniwezesha leo hii kuwa Mwanamke wa Kwanza Tanzania kushika nafasi ya Umakamu wa Rais na hatimaye sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niliwahi kusema na leo narudia tena kwamba Mimi na Hayati Magufuli ni kitu kimoja, kwahiyo mengi ambayo nimepanga kuyatekeleza ni yale ambayo yalielezwa na Hayati Magufuli wakati akilizindua Bunge hili”, ameongeza Rais Samia.
No comments