Kagere Awapania AS Vita Kwao
MSHAMBULIAJI wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere amefunguka kuwa wanakwenda kucheza na AS Vita ambao wanawajua vizuri hivyo hawatokuwa wanyonge kwa kuwa wanataka matokeo mazuri.
Februari 12, mwaka huu Simba itacheza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, ambao unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Pentecost Martyrs.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kagere alisema kuwa wanakwenda katika mchezo huo kwa lengo la kuhakikisha wanapata matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wao kwani hawataki kuwa wanyonge msimu huu.
“Tunakwenda kucheza mechi ngumu kwa sababu ni wapinzani ambao wanatujua na tunawajua vizuri lakini jambo kubwa ambalo tunaliangalia ni kuweza kupata matokeo kwa kuwa ndiyo itakuwa mechi yetu ya kwanza katika hatua hii.
“Nadhani kila mmoja wetu anawajua vizuri AS Vita kwa sababu ni timu yenye uzoefu mkubwa lakini hatuwezi kukubali kuwa wanyonge wa kucheza ugenini, naamini haitokuwa mechi nyepesi ila tunataka matokeo mazuri kwa ajili kuweza kufika mbali,” alisema Kagere.
Stori: Ibrahim Mussa, Dar es Salaam
No comments