Familia yapata pigo, watoto wapoteza babu, bibi wazazi
Morogoro. Familia ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Delphina Mamiro imepata pigo ndani siku 28 kwa kupoteza watu wanne, akiwamo profesa huyo.
Awali, wazazi wa profesa huyo walifariki dunia katika familia Januari mwaka huu wakipishana siku tatu, baada ya kuanza mama yake na kufuatiwa na baba yake.
Hata hivyo, wakati machungu hayo hayajapoa, Profesa Delphina alianza kujisikia vibaya mwanzoni mwa mwezi huu na kufariki dunia akipatiwa matibabu hospitali na siku chache baadaye mumewe alifariki dunia.
Akizungumza na Mwananchi jana nyumbani kwa marehemu eneo la Kihonda Manispaa ya Morogoro kabla ya kukataa kuzungumza zaidi, Anna Mamiro, ambaye ni mtoto wa Profesa Delphina, alisema vifo vya wazazi wao ni pigo kwa familia.
Anna alisema Januari 13 mwaka huu mkoani Kilimanjaro walimpoteza bibi yao mzaa mama aliyemtaja kwa jina la Franciska Kyessi baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Alieleza kuwa wakati wakiombeleza kifo cha bibi yao, Januari 16, mwaka huu wakapata pigo jingine la kifo cha babu yao mchungaji Lucas Kyessi, ambaye alifariki ghafla.
“Mama na baba walitoka Morogoro na kwenda Moshi kwa ajili ya kuzika na baada ya hapo walirejea Morogoro na kuendelea na majukumu yao.
“Hata hivyo, baada ya siku chache mama akawa analalamika hajisikii vizuri. Baadaye akaugua na ikabidi kumpeleka hospitali ya mkoa kwa matibabu zaidi,” aliongeza Anna.
Anna alisema mama yao alifariki Jumamosi iliyopita, Februari 6, huu baada ya kuzidiwa.
“Wakati tukiendeleza maandalizi ya mazishi na kusafirisha mwili wa mama kwenda mkoani Kilimanjaro, usiku wa kuamkia Februari 9 (jana) mwaka huu, tukapata msiba mwingine mzito wa baba yetu,” alisimulia Anna.
Alisema Dk Peter Mamiro alifariki dunia nyumbani kwake maeneo ya Veta Kihonda baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Mwananchi ilifika nyumbani kwa marehemu na kukuta watu waombelezaji wakiwa kwenye eneo la nyumba ya familia ya profesa na Dk Mamiro.
Akizungumzia msiba huo, Makamu mkuu wa SUA, Profesa Paphael Chibuda alisema kama wanajumuiya wa chuo wamepoteza sehemu ya wanafamilia wamempoteza Profesa Delphina ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Mimea Vipando na Bustani(Department of Crop Science and Horticulture).
“Kwa kweli tuna majonzi kutokana na ufanisi wa Profesa Mamiro (Delphina) kazini na kuibua vipaji vya vijana, ambao walikuwa wanasoma chuoni hapa.
“Tumepoteza gwiji, nguli na mhadhiri mwandamizi, tunapitia kwenye kipindi kigumu kwa sababu kupoteza mtu muhimu ambaye kuziba pengo lake itachukua muda mrefu,” alisema Profesa Chibunda.
Profesa Delphina pamoja na kuwa mhadhiri wa SUA, pia alikuwa anatumika katika masuala ya ushauri kwenye taasisi mbalimbali za umma.
Profesa Chibunda alisema familia hiyo walipoteza wazazi wao na walienda wilayani Moshi kwa mazishi na waliporudi walianza kuumwa.
Wakati kwa Dk Peter alikuwa amestaafua kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sokoine.
Kabla ya kustaafu alikuwa mhadhiri wa kitivo cha Chakula na Lishe katika Chuo Kikuu cha Sokoine.
Dk Peter katika utumishi wake alikuwa kati ya wabobezi masuala ya chakula sio ndani ya nchi pekee bali pia nje ya nchi.
No comments