Raia wa Kenya akana kuhusika na biashara ya pembe za ndovu Marekani
Raia wa Kenya amekana mashtaka dhidi yake nchini Marekani, alikoshutumiwa kusafirisha pembe za ndovu na faru, zenye thamani ya mamilioni ya dola.
Pia amekana kujihusisha na vitendo vya utakatishaji fedha na biashara ya dawa za kulevya na alishikiliwa bila dhamana, Shirika la habari la AP limeeleza.
Waendesha mashtaka wa Marekani wamesema mshukiwa, Mansur Mohamed Surur, alikuwa sehemu ya wala njama wa kimataifa ambao wamehusika na vitendo vya kuwaua zaidi ya tembo 100 na faru kadhaa.
Bwana Surur alirudishwa kutoka Kenya na aliwasili Marekani Jumatatu ili kushtakiwa. Alikamatwa mwaka jana katika mji wa Mombasa nchini Kenya.
Yeye na wezake watatu kutoka Guinea, Liberia na Kenya wanashutumiwa kukubali kufanya biashara haramu na wanunuzi mjini Manhattan, kadhalika wanunuzi wengine kutoka Kusini Mashariki mwa bara la Asia.
Mwendesha mashtaka Audrey Strauss amesema Bw. Surur alihusika na uwindaji haramu wa karibu faru 35 na zaidi ya tembo 100.
No comments