Header Ads

Header ADS

Aliyemkwepa DPP jela miaka 20, faini Sh65 mil kesi kucha za simba

Dar es Salaam. Mshtakiwa Daud Maturo, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kukutwa na meno 10 na kucha 18 za simba, kukwepa kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.


Mbali na kifungo hicho, Maturo ametakiwa kulipa faini ya Sh65.9 milioni.


Wakati Maturo akihukumiwa, mwenzake Hassan Ahmed waliokamatwa pamoja alikiri kosa hilo walipofikishwa mahakamani na kutakiwa kulipa faini ya Sh1 milioni na fidia ya Sh65.9 milioni.


Kupitia wakili wake, Gwasika Sambo, mshitakiwa Ahmed alionyesha nia ya kufanya makubaliano na DPP, ili kumaliza kesi dhidi yake, huku mwenzake alikana na kuendelea na kesi hiyo.


Washtakiwa hao walikamatwa Juni 21, 2017 mkoani Arusha wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota IST na meno 10 na kucha 18 za simba, vyote vikiwa na thamani ya dola za Marekani 14,700 (Sh32.9 milioni).


Walishtakiwa kwa kosa la kukutwa na nyara za Serikali kinyume cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, lenye adhabu ya kifungo cha si chini ya miaka 20 na faini mara mbili ya thamani ya nyara walizokutwa nazo.


Walivyokamatwa


Juni 19, 2017, askari polisi mmoja alipopokea taarifa kutoka kwa msiri kuhusu biashara ya kucha na meno ya simba iliyopangwa kufanyika mkoani humo.


Siku mbili baadaye, askari huyo alitaarifiwa kuhusu kutiliwa shaka kwa gari lililoegeshwa katika eneo la Arusha Star na kumchukua mwenzake kufuatilia.


Walipofika walilikuta gari hilo aina ya Toyota IST likiwa na watu wawili ndani. Walisogea karibu na kugonga dirisha la gari hilo ambalo lilifunguliwa.


Baada ya kujitambulisha, kazi ya upekuzi wa gari hilo ilianza, huku ikishuhudiwa na askari mwingine na shahidi wa kujitegemea.


Wapelelezi hao walikuta rula na bahasha ya kaki kwenye dashibodi ikiwa na meno 10 na kucha 18 za simba. Idadi hiyo inamaanisha simba watatu waliuawa. Watuhumiwa wote walisaini hati ya ukamatwaji wa nyara hizo kwa maandishi na kuweka dole gumba. Watuhumiwa hao pamoja na gari lililokuwa wakitumia walipelekwa hadi kwenye ofisi za Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili Kanda ya Kaskazini (KDU) na baadaye kushitakiwa mahakamani.


Utetezi wa Maturo


Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Maturo alikana kumjua mshitakiwa wa kwanza aliyeachiwa hadi siku alipokutana naye mahakamani. Pia alikana kukamatwa na nyara za Serikali.


Alidai alikamatwa na askari nyumbani kwake eneo la Kikatiti kwa madai ya kuiba gari na akiwa kituo cha polisi cha Ngurdoto alipigwa, huku akilazimishwa kuwataja waliohusika na wizi wa gari hilo.


Maturo pia alileta shahidi ili aupe nguvu utetezi wake kuwa hakuwepo eneo la tukio wakati kosa hilo lilipodaiwa kutendeka. Shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio alikuwa na mshtakiwa kuanzia jioni hadi walipoachana saa 2 usiku.


Jaji atupa utetezi


Akitoa hukumu hiyo, Jaji Immaculata Banzi alisema kushindwa kwa mshtakiwa kupinga ushahidi kuwa alikuwepo eneo la tukio akiwa na nyara za Serikali, ulisaidia kuthibitisha kosa dhidi yake.


Jaji Banzi aliukataa utetezi wa Maturo kuwa hakuwepo eneo la tukio siku kosa hilo likitendeka, akisema mshtakiwa alipaswa kuijulisha mahakama kuwa angetumia ushahidi huo kujitetea wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi dhidi yake.


“Japokuwa mshtakiwa wa pili ameleta shahidi wake katika jitihada za kuupa nguvu utetezi wake kwamb, hakuwepo eneo la tukio muda uliodaiwa kutendeka kosa, lakini nilikuwa na fursa ya kumfuatilia shahidi huyo akiwa kizimbani.


“Tabia yake kwa nje haikufurahisha. Hata hivyo, yeye aliachana na mshtakiwa saa mbili ambapo ni kabla kosa halijatendeka,” alisema Jaji Banzi.


Mwananchi



No comments

Powered by Blogger.