2020 ilivyoondoa Umaarufu wa Makonda Ghafla
Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, mapema mwezi Julai alitia nia ya kuwania ubunge wa jimbo la Kigamboni, ambapo katika kura za maoni alitupwa mbali na aliyekuwa mshindani wake Dkt Faustine Ndugulile, baada ya yeye kupata kura 122 na mwenzake kupata kura 190.
Mara baada ya Makonda kutangaza nia na kuchukua fomu ya kugombea, baadaye jioni Rais Dkt. John Magufuli, alimteua na kumtangaza mrithi wa nafasi ya Makonda ya ukuu wa mkoa, nafasi ambayo ilijazwa na aliyekuwa katibu tawala wake wa mkoa, Aboubakar Kunenge.
Licha ya Makonda kushindwa kwenye kura za maoni, watu wengi waliamini kwamba huenda jina lake lingerudishwa na Kamati Kuu ya CCM, lakini hali haikuwa hivyo na badala yake Kamati Kuu ilimchagua Dkt. Faustine Ndugulile, kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28.
Mara baada ya Makonda kuondolewa kwenye nafasi ya ukuu wa mkoa, na Kamati Kuu ya chama chake kumbwaga kwa mbali, umaarufu wake ulizima ghafla, huku watu wengi kwenye mitandao ya kijamii, wakieleza ni kwa namna gani wanaikumbuka Dar es Salaam, iliyokuwa chini yake kwa kuwa ilikuwa na mambo mengi.
Kabla ya kuondoka katika nyadhifa hizo Makonda, alifanya mambo kadha wa kadha ikiwemo, kampeni yake ya kuwataja wauzaji wa madawa ya kulevya jijini humo, kampeni yake ya usafi wa kila Jumamosi, kampeni yake yake ya kuzuia watu ambao hawajaoga kuingia mjini wakati wa mikutano ya SADC, pamoja na kuagiza kuwakamata wabunge wote wa upinzani waliomo ndani ya jiji hilo bila ruhusa ya Spika Ndugai.
Mbali na hizo Makonda pia aliwahi kuanzisha kampeni ya kusikiliza kero ya wanawake, wakiwemo wajane na wale ambao wametelekezwa na watoto na kushinikiza kila Baba anapaswa alee mtoto wake, lakini pia Makonda alikuwa ni msaada mkubwa kwa watu wenye ulemavu baada ya kuanza kugawa vifaa mbalimbali vya walemavu ikiwemo miguu bandia na viti mwendo.
Makonda pia alikuwa mstari wa mbele wa kusimamia miradi ya maendeleo ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa Hospitali, ukarabati wa miundombinu ya barabara ndani ya mkoa wake pamoja na ujenzi wa masoko mapya na ya kisasa.
Makonda pia hawezi kusahaulika ndani ya jeshi la polisi Dar es Salaam, kwani alisaidia ukarabati wa magari mengi ya doria ya polisi yaliyokuwa yamechakaa na kuacha kutumika.
No comments