Utajiri wa Marehemu Ginimbi Wazua Gumzo!
MITANDAO mbalimbali ya kijamii ‘imechafuka’ kwa picha za magari na mijengo ya kifahari ya kijana maarufu katika ukanda wa nchi za kusini mwa Afrika, Genius Kadungure ambaye pia ni maarufu kwa jina la ‘Ginimbi’. AMANI linakupakulia.
Ginimbi ambaye ni raia wa Zimbabwe aliyezaliwa Oktoba 1984, ameacha gumzo kutokana na utajiri wake unaokadiriwa kufikia zaidi ya Sh bilioni 200.
Gumzo hilo limeibuka siku chache baada ya kufariki kutokana ajali mbaya ya gari iliyotokea Novemba 8 mwaka huu wakati akitoka kwenye sherehe kuzaliwa ‘birthday party’ ya mchepuko wake aliyefahamika kwa jina la Michelle Amuli maarufu Mimi Moana (26).
Ndani ya gari hiyo ya kifahari aina ya Rolls Royce Wraith, mbali na Ginimbi na mwanadada Moana, walikuwepo watu wengine wawili ambao wote kwa pamoja walipoteza maisha.
Kwa mujibu wa Gazeti la Harere watu hao wengine wawili ni Limumba Karim ambaye ni raia wa Malawi aliyekuwa akitafutwa kwa tuhuma za utapeli na mwanamke mmoja raia wa Msumbiji aliyetambulika kwa jina la Alichia Adams.
Inaelezwa kuwa Ginimbi ambaye alikuwa anaendesha gari hiyo kwa kasi hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na gari nyingine ina ya Honda kisha kupoteza mwelekeo na kuparamia mti. Gari hiyo iliwaka moto uliowaunguza pakubwa watu wanne waliokuwa ndani yake.
Polisi wa Zimbabwe walithitisha kuwa watu watatu walifariki papo hapo baada ya kuungua lakini Ginimbi alifariki dakika tano baada ya kutolewa ndani ya gari hiyo kwa mujibu wa mashuhuda.
ZARI AMLILIA
Awali mwanadada mashuhuri na mzazi mwenza wa Msanii maarufu wa Bongo Fleva, Nasib Abdul ‘Diamond Platinums’, Zarina Hassan ‘Zari, aliposti kwenye akaunti yake ya Instagram kuelezea mshtuko na masikitiko yake kuhusu kifo hicho.
Zari ambaye anadaiwa kuwa rafiki wa karibu na aliyekuwa mke wa Ginimbi, Zodwa Mkandla aliandika; “Siwezi kuelezea… bado nimepigwa na butwaa, G wangu siwezi kuvumilia maana inaumiza sana. Siamini kama ukurasa wako wa maisha ndio umefungwa. Kitabu kina mwisho na sio sehemu ya pili, Mwenyezi Mungu akupe pumziko la milele,” aliandika Zari.
MCHUNGAJI ALIKIONA KIFO CHAKE
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, inaelezwa kuwa Mchungaji wa kanisa moja jijini Harare ambaye pia ni wakili, Joshua Zim alidai kutabiri kifo cha Ginimbi saa 72 kabla ya tukio hilo la ajali.
Mchungaji huyo anaelezwa kuwaambia Wazimbabwe wamuombee Ginimbi kwa kuwa alikuwa amepata maono ya jambo baya liloweza kumtokea.
ALINUNUA JENEZA LAKE
Aidha, katika hali ya kushangaza taarifa zinaeleza kuwa wiki moja kabla ya kifo chake, Ginimbi alinunua jeneza lake lenye thamani kubwa kwa ajili ya kutumika siko atakapotoweka duniani.
Jeneza hili limeelezwa kukutwa ndani ya mojawapo ya chumba cha Ginimbi jambo ambalo liliwafanya watu wabaki midomo wazi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC), Ginimbi na mpenzi wake Mimi Moanna wanadaiwa kuona viashiria vya mwisho wao.
Katika posti yake ya mwisho, Ginimbi aliposti video kwenye akaunti yake ya Instagram ikimuonesha akiingia kwenye gari yake kwenda kusherehekea birthday hiyo katika klabu marufu ya usiku ‘Dreams Night Club’ ambayo anaimiliki.
Katika video hiyo alisema, “Tunaenda kufungua shampeni, unakwenda kuwa usiku wa kuogelea shampeni.”
SAFARI YA UTAJIRI WAKE
Wakati mazishi yake yakiendelea kuwa gumzo, upande wa pili utajiri wake pia nao umezidi kuwaweka watu njia panda kutokana na magari ya kifahari na majumba aliyokuwa anayamiliki kijana huyo.
Ginimbi ambaye anakadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya Sh bilioni 200, safari yake kimaisha aliianza mwaka 2000 kwa kuanza kujishughulisha na uuzaji wa mitungi ya gesi ambayo alikuwa akiisambaza majumbani mwa watu.
Wakati huo akiwa na umri wa miaka 17 anaida kuifanya biashara hiyo ambayo ilimpatia uzoefu mkubwa uliomkutanisha na rafiki yake aliyekuwa anafanya kazi katika ofisi za Shirika la Ndege la Angola.
Kwa mujibu wa taarifa zake, hapo ndipo siri ilipojificha kwani tangu alipokutana na rafiki yake huyo, inaelezwa mambo yalimnyookea Ginimbi ambaye alianzisha kampuni yake ya kusambaza gesi ijulikanayo kama ‘Pioneer Gases.
Kampuni hiyo ambayo sasa ni kubwa katika ukanda huo ina matawi nchi za Zimbabwe, Botswana na Afrika Kusini.
Ndani ya miaka miwili alipata magari mawili ikiwamo gari la thamani aina ya Mercedes Benz S class.
Ginimbi alikuwa akiongoza Kampuni hiyo ya Pioneer inayosambaza gesi majumbani, kwenye viwanda vikubwa na kwa wauzaji wa rejareja mitaani.
Aidha, mkewe aliyefahamika kwa jina la Zodwa Mkandila ambaye wana watoto wawili, pia ni mfanyabiashara mkubwa nchini Zimbabwe. Anamiliki kampuni ya Traverze Travel ambayo alianzisha mwaka 2003 baada ya kuacha kazi ya mapokezi ‘receptionist’ katika ofisi moja.
ANAVYOMILIKI NI BALAA
Ginimbi ana miliki majumba ya kifahari yaliyopo majiji ya Harare, Johanessburg Afrika Kusini na Gabarone Botswana. Pia anamiliki magari ya kifahari aina mbalimbali kama vile RR, Autobiograph Range, Bentely, Lamborghini, Ferrari yote yanakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.1.
Wakati wengi wakitilia shaka utajiri wake, Oktoba 3, mwaka huu aliongeza gari ya kifahari aina ya Lamborghini mpya yenye thamani ya dola za Kimarekani 600,000 (Sh bilioni 1.3). Gari lake hilo la kifahari lilizua gumzo kwa watu wengi katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.
MISUKOSUKO
Mei 2014, Ginimbi alikamatwa kwa madai ya utapeli zaidi ya Sh milioni 200. Alituhumiwa kumtapeli mbunge wa chama tawala nchini Zimbabwe (Zanu-PF), Chegutu Magharibi Dexter Nduna.
Nduna ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Badon Enterprises na mchimba madini ambaye pia ni maarufu nchini humo kwa jina la Gatawa.
Ginimbi alituhumiwa kusajili kampuni ya uongo inayoitwa Transco Civil Engineering huko Afrika Kusini na kufungua akaunti ya katika benki moja. Kisha aliwasiliana na mbunge huyo kwa njia ya simu kuwa yeye ni mkurugenzi wa kampuni hiyo na kwamba anatafuta soko la pampu zinazotumika katika uchimbaji wa madini.
Gatawa alidaiwa kumtuma kaka yake Enock kwenda Afrika Kusini kununua pampu hizo. Ginimbi alidaiwa kumwelekeza Enock kuweka kwenye akaunti ya benki ya kampuni kiasi cha fedha zaidi ya milioni 300 kwa ajili ya kununua pampu hizo 10.
Baada ya uhamisho huo wa fedha, Enock aliambiwa na maofisa wa Kampuni ya Ginimbi, Transco Civil Engineering arejee Zimbabwe na kusubiri kifurushi chake baada ya siku tatu.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa baada ya muda huo alipokea kifurushi kilichojazwa chaja za Smartphone.
Misukosuko mingine ikiwamo utakatishaji fedha pamoja na ukwepaji wa kodi pindi alipokuwa ananunua magari yake.
Ginimbi alidaiwa kukwepa kulipa ushuru hatua ambayo ilimsababishia kukutana na makucha ya Mamlaka ya Mapato Zimbabwe (Zimra) wakati aliponunua gari aina ya Bentley Continental GT.
AKATAYEHUDHURIA KUNUNUA POMBE YAKE KWENYE MAZISHI
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, sherehe ya mazishi yake iliyofanyika jana katika moja ya majumba yake ya kifahari lililopo Domboshava jijini Harare- Zimbabwe.
Kwa mujibu wa msemaji wake, aliyefahamika kwa jina la Shelly, kila mmoja aliyehudhuria sherehe hiyo atatakiwa kwenda na kinywaji chake (kilevi) kwani tangu enzi za uhai wake Ginimbi hakupenda kumnunulia mtu kilevu.
No comments