Mwamuzi FIFA Afunguka…. Ile Penalti Ya Yanga Mh!
UTATA wa penalti waliyoipata Yanga juzi kwenye mchezo dhidi ya Simba, umezidi kuwa mkubwa kiasi cha Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Soud Abdi Mohammed ambaye ni mwamuzi mkongwe mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kupatwa na kigugumizi.
Yanga juzi ilipambana na Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar ambapo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Waamuzi wa mchezo wa juzi walikuwa sita, lakini aliyesimama kati alikuwa Abdallah Mwinyimkuu ambaye aliwapa Yanga penalti ambayo ilizua utata mkubwa wengi wakisema faulo ilichezeka nje ya boksi lakini yeye akaiweka ndani.
Ilikuwa dakika ya 28, Tuisila Kisinda akielekea langoni kwa Simba kufunga, akaangushwa na Joash Onyango, mwamuzi akaweka penalti iliyokwenda kufungwa na Michael Sarpong na kuipa Yanga bao la uongozi dakika ya 31.
Wachezaji wa Simba walionekana kupinga sana juu ya penalti hiyo, lakini kulalamika kwao hakukubadili mawazo ya mwamuzi.
Hata hivyo, dakika ya 84, Simba ilisawazisha kupitia kwa Onyango aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Luis Miquissone.
Bosi huyo wa waamuzi, aliliambia Spoti Xtra kuwa: “Mechi nimeiangalia, lakini siwezi kusema moja kwa moja kwamba ile ilikuwa penalti au la, tuwaachie kamati wakae kujadili matukio ya mechi zote ikiwemo hiyo, kisha watakuja na majibu.
“Kama kutakuwa na dosari yoyote, basi itafahamika.”
Mwinyimkuu juzi hadi mchezo unamalizika, alikuwa ametoa kadi sita za njano, tatu upande wa Simba zilizokwenda kwa Joash Onyango, Jonas Mkude na Aishi Manula, huku Yanga nao wakipata tatu, Farid Mussa, Tuisila Kisinda na Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Kabla ya juzi, mwamuzi huyo aliwahi kuzichezesha timu hizo dhidi ya timu zingine kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo wakati Simba ikifungwa na Ruvu Shooting bao 1-0, aliwapa Simba penalti na kumuonyesha kadi nyekundu Shaban Msala wa Ruvu.
Mechi ya mwisho kuichezesha Yanga kabla ya juzi, ilishuhudiwa Yanga ikishinda 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania. Mechi hizo zote zilichezwa Uwanja wa Uhuru, Dar.
Mchezo ulipomalizika, mwamuzi huyo aliondolewa akiwa chini ya ulinzi mkali ili kumlinda asiletewe fujo na mashabiki wenye hasira kali.
Juzi wakati matokeo yakiwa hivyo, rekodi imeandikwa kwenye Dabi ya Kariakoo baada ya nyota wawili wa kimataifa, Michael Sarpong wa Yanga na Joash Onyango wa Simba kufunga mabao kwenye dabi yao ya kwanza tangu wajiunge na timu hizo msimu huu.
Wawili hao ndiyo walioamua matokeo ambapo Sarpong alianza kufunga dakika ya 31 baada ya Tuisila Kisinda kuangushwa na Onyango kwenye eneo la hatari.
Kuingia kwa bao hilo, kukaufanya mchezo kuwa mgumu zaidi hasa upande wa Simba ambao walifanya mashambulizi ya mara kwa mara, lakini safu ya ulinzi ya Yanga ikiongozwa na nahodha wake, Lamine Moro, ilikaa imara kulinda lango lao.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Yanga kuongoza kwa bao 1-0 ambapo kipindi cha pili, fasta Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck akafanya mabadiliko kwa kumtoa Rally Bwalya na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Dilunga.
Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Lamine alionekana kupata maumivu makali zaidi kwenye goti na kulazimika kubebwa na machela na kutolewa uwanjani.
Baadaye dakika ya 49, akatoka kabisa na nafasi yake kuchukuliwa na Said Juma Makapu.
Kutoka kwa Lamine, kukawapa nafasi zaidi Simba kulishambulia lango la Yanga ambapo walisubiri hadi dakika ya 84 kusawazisha bao hilo kwa kichwa kilichopigwa na Onyango.
Ikumbukwe kuwa, juzi ilikuwa ni mechi ya 105 katika Ligi Kuu Bara tangu watani hao wa jadi waanze kukutana Juni 7, 1965.
Rekodi zinaonesha kwamba, katika mechi hizo, Yanga imeshinda 37 na Simba imeshinda 31, wakati sare zikiwa 37.
Bao la Sarpong juzi lilikuwa la 209 katika dabi hiyo, huku likiwa la 110 kufungwa na Yanga dhidi ya Simba, huku lile la Onyango likiwa na 210 katika dabi.
TAKWIMU
Yanga na Simba zikiwa zimejaa mafundi wengi vikosini mwao, juzi walioneshana ufundi huo ambapo ilishuhudiwa Clatous Chama wa Simba, akiwafunika wote kwa kupiga pasi nyingi ambazo ni 76.
Kipindi cha kwanza, Chama alipiga pasi 45 na cha pili akipiga pasi 31, huku nyota wengine wa Simba kama Dilunga akipiga pasi 25, Mzamiru Yassin (53) na Bwalya (24).
Upande wa Yanga, Fei Toto alipiga pasi 15, Kisinda (29), Tonombe Mukoko (26) na Farid Mussa (17).
Manula juzi alikuwa vizuri langoni, licha ya kufungwa bao moja la penalti, lakini aliokoa hatari sita zilizoelekea langoni kwake.
Wakati Manula akiokoa hatari hizo, upande wa kipa wa Yanga, Metacha Mnata, hakuwa na purukushani nyingi kwani aliokoa hatari mbili tu muda wote wa dakika tisini.
Baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa juzi, kiungo wa Yanga, Mukoko Tonombe alikabidhiwa mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni moja baada ya kuibuka kuwa mchezaji bora wa mechi
TONOMBE AMFUNIKA CHAMA
Katika eneo la kiungo, juzi Tonombe alimfunika Chama kiasi cha kumfanya kiungo huyo kushindwa kung’ara kama kawaida yake.
Tonombe ambaye alikuwa na mchezo mzuri, alitawala eneo lote la kiungo muda wote wa dakika tisini.
WAANDISHI: SAID ALLY, HUSSEIN MSOLEKA NA MARCO MZUMBE
WAANDISHI WETU, Dar es Salaam
No comments