Kiba Aibua Mchezo Mchafu wa Mondi
MKALI wao ndani ya Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’, ameibua mchezo mchafu ambao hufanywa na baadhi ya wasanii ili kujipatia tuzo, Gazeti la IJUMAA linakushushia habari nzito.
Licha ya kutowataja majina, lakini ni dhahiri shahiri kauli yake inakwenda moja kwa moja hasimu wake kimuziki, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’ ambaye juzikati alishinda Tuzo ya Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki 2020.
YUMO PIA ZUCHU
Mbali na Mondi, kwenye tuzo hizo mashuhuri za muziki Duniani za All Africa Music Awards (AFRIMMA), Zuhura Othman ‘Zuchu’ naye alishinda Tuzo ya Mwanamuziki Bora Chipukizi Afrika Mashariki.
Msanii mwingine kutoka Bongo aliyeshinda tuzo hiyo ni Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ aliyenyakua Tuzo ya Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki.
KIBA AMKUBALI NANDY
Gazeti la IJUMAA lilipomtafuta Kiba ili kumsikia maoni yake kuhusiana na tuzo hizo ndipo alipompongeza Nandy pekee kwa kusema kweli alistahili kushinda, lakini hakuwazungumzia Mondi na Zuchu kama wanastahili.
MAHOJIANO KAMILI
Kwenye mahojiano hayo na Gazeti la IJUMAA, Kiba anasema yeye haimbi muziki ili apate tuzo kwa sababu siku hizi tuzo hizo zimepungua ile thamani iliyokuwepo mwanzo.
Anasema kuwa, kwa mtazamo wake kwenye tuzo nyingi zinazotolewa, kuna figisu nyingi hivyo haoni sababu ya kujivunia kitu ambacho hakina uhalisia.
MAMBO YALIKUWA HIVI…
IJUMAA: Mambo vipi Kiba?
KIBA: Poa tu, niambie…
IJUMAA: Safi, Nandy ni binti ambaye umeshiriki kufanya naye kazi ya Nibakishie na kwa bahati nzuri naye ni miongoni mwa wasanii waliopata tuzo kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki, una lipi la kumwambia?
KIBA: Kwanza nimpe hongera, la pili, tuzo za sasa hivi ni kama show-off mimi ninavyoona, unaweza ukawa unajua, lakini watu hawajakupigia kura, labda mashabiki zako walikuwa bize au huna kabisa hao mashabiki wa kukupigia kura.
Na vilevile mambo ya Corona nayo yameingilia kati kwa hiyo mwisho wa siku kura zitapigwa, lakini lazima mshindi apatikane.
FULU KUMSIFIA NANDY…
Kwa hiyo Nandy amepambana na kupigania kazi yake, sasa hivi hakuna msanii wa kike ambaye unaweza ukamuongelea kama Nandy na ukweli ni kwamba amestahili kupata tuzo hiyo.
IJUMAA: Sasa vipi kwa upande wako? Maana hatuoni ukishiriki kabisa na huu mwaka umetoa ‘hit songs’ za kutosha.
KIBA: Mimi sifanyi muziki ili nipate tuzo.
IJUMAA: Unamaanisha nini unaposema hivyo?
KIBA: Kwa sababu zamani tuzo zilikuwa kweli zina value (thamani), lakini siku hizi thamani yake imeshuka kabisa.
Unapopewa tuzo, watu hawamaanishi, yaani kuna wengine huwa wanapewa tu na ushahidi nipo nao kutokana na tulishapigiwa mpaka simu, wanakupigia simu, wanakuambia vipi utakuja kupafomu? Ukiwaambia nakuja kupafomu, unapata tuzo.
IJUMAA: Eheee!
KIBA: Eeh! Yaani kuna hongo huwa zinafanyika.
IJUMAA: Unamaanisha kuna wasanii huwa wanahonga pesa ili wapate tuzo?
KIBA: Watu wanahonga na ukionyesha unasapoti ndiyo na wao wanakusapoti, kwa hiyo ile thamani ya tuzo imeshuka.
IJUMAA: Kwani tuzo anatakiwa apate msanii mwenye vigezo gani?
KIBA: Unajua maana ya tuzo ni kumtunuku mtu ambaye amefanya kazi na anastahili na siyo ujanjaujanja.
Kiba hakutaka kuingia kwa undani sana kuhusu ujanjaujanja unaofanywa, lakini alisisitiza kwamba tuzo hizo hazina thamani.
Licha ya Kiba kutowataja majina Kiba na Zuchu wala waandaaji wa tuzo walizopata, lakini mitandaoni kumekuwa na maoni tofautitofauti kuhusu Tuzo za AFRIMMA ambazo Mondi na Zuchu walipata.
Kuna baadhi ya watu walisema kuwa, wanahisi kuna figisu zinafanyika kwani kwa mwaka huu, Mondi hakuwa na ngoma kali iliyompa uhalali wa kushinda tuzo hiyo tofauti na Kiba aliyekuwa na nyimbo kali.
Ngoma pekee ya Mondi aliyotoa peke yake ni Jeje huku Kiba akiwa ameachia Mediocre, Dodo na So Hot ambazo zote zilifanya vizuri huko mjini YouTube.
Licha ya kuwepo kwa watu hao walioponda uhalali wa tuzo hizo, wapo wengine walipongeza kwa kusema wasanii hao walistahili kwa kuwa wanafanya vizuri.
TUJIKUMBUSHE
Kwa muda mrefu sasa, Kiba na Mondi wamekuwa ni mahasimu wakubwa; yaani ni kama paka na panya huku chanzo cha bifu lao kikidaiwa kuwa ni kutofautiana katika shughuli za kimuziki.
No comments