FIFA yatangaza mageuzi kulinda wanasoka wajawazito
Fifa inapanga kuchukua hatua kadhaa kwa ajili ya kulinda wanasoka wajawazito, ikiwa ni pamoja na kuweka sheria ya likizo ya lazima ya uzazi ya "angalau wiki 14", shirikisho hilo la soka duniani limetangaza leo Alhamisi (Novemba 19).
"Tunataka kuona wanawake wanacheza soka na wakati huohuo wawe na familia," alisema Sarai Bareman, ofisa mkuu wa soka la wanawake wa Fifa, alipoongea na waandishi wa habari.
Chombo hicho kimesema kitawasilisha mapendekezo kadhaa ya mageuzi kwa kamati ya utendaji ya Fifa mwezi ujao, na hivyo kuyafanya yaanze kutumika mara moja kwa wanachama wote 211.
Likizo ya lazima ya wiki 14 itawahakikishia wachezaji kupata angalau theluthi mbili ya mshahara wao, huku Fifa ikionyesha itaweka mazingira magumu kwa klabu kuwaacha wachezaji wajawazito, ikisema "hakuna mchezaji atakayetakiwa asumbuke kwa sababu ya kuwa mjamzito".
Katika mapendekezo hayo, kama mchezaji anaachwa kwa sababu ya kupata ujauzito, klabu husika itakabiliwa na adhabu ya kifedha na kimichezo.
Klabu zitatakiwa pia kuwa na wachezaji hao wa kike na kuwapa "huduma za kutosha za afya na za kimwili" baada ya kujifungua.
Awali mashauri ya wachezaji wanawake kurejea mashindanoni baada ya kujifungua yalikuwa ya nadra, ingawa Alex Morgan,31, ambaye alitwaa Kombe la Dunia akiwa na Marekani, alipata mtoto Mei mwaka huu na amerejea uwanjani na kusaini mkataba na klabu ya Tottenham Hotspur ya England.
No comments