ZINGATIA ..Haya ni Mambo Matatu Ambayo Hupaswi ‘Kuya-Google’ Kamwe..!!!
Google imerahisisha njia za kufahamu mambo mengi ambayo binadamu angepaswa kutumia muda mwingi kuyatafuta au hata kulipia ili aweze kuyafahamu.
Kupitia Google unaweza kuwa na shule ya ziada ya ufahamu wa mambo mbalimbali yakiambatana na picha za aina unazotafuta. Ili mradi tu kuna mtu duniani aliwahi kuweka kwenye mtandao kwa ajili ya umma. Unachopaswa kuwa nacho ni kifaa cha mfumo wa ‘computer’ chenye mtandao.
Naweza kusema kuwa Google ni kama kioo cha ubongo wako, chochote unachotaka kukiangalia ndicho kitakachojitokeza kwenye kioo cha computer au simu yako yenye mtandao.
Wengi tumepata elimu kubwa sana na ufahamu wa mambo mengi makubwa na muhimu kupitia Google. Tunapata habari, burudani na mengine mengi.
Lakini nakumbuka mwalimu wangu wa chuo aliwahi kuniambia kuwa google ni msaada mkubwa kwa masomo yako, lakini ni chanzo kikubwa cha ‘kukupumbaza’ (google will make you stupid).
Kauli hiyo ndiyo iliyonifanya niweze kufikiria, ni mambo gani ambayo sipaswi kuya-google ili yasinifanye kuwa mpumbavu au yanayoweza kunidhuru kwa kuyaangalia?
Kwa bahati mbaya, wataalam wa Saikolojia wanaeleza kwamba akili ya binadamu hutamani sana kuangalia mambo yaliyozuiliwa kuangalia, kuliko mambo yaliyowekwa bayana.
Tukumbuke kuwa Google ni kama soko huria la mawazo ambalo karibu kila utakacho utapata, lakini huwezi kununua usichotaka. Kila aina ya usafi na uchafu hutupwa Google.
Mambo ambayo hupaswi kuya-google ni mambo yote ambayo, kwanza yatakubadili saikolojia yako na kufuata mambo ambayo kabla ya kuyagoogle ulijua kabisa hayafai katika jamii uliyopo.
Pili, ni mambo yote ambayo ni haramu kuyatamka au kuyazungumzia katika jamii yako, jiulize unataka kuyafahamu ili upate faida gani? Je, unahisi ukiyaona yatakusaidia kuendeleza zaidi maisha yako au yatakuondoa kwenye reli ya maadili na imani yako?
Tatu, mambo yote ambayo yanaweza kukuharibia siku kisaikolojia, unaweza kuona mateso, uchafu na mambo kama hayo ambayo yatakugharimu na kuichafua akili yako. Usijaribu ku-google vitu unavyovichukia, kisaikolojia vitakugharimu… hususan kama hakuna sababu muhimu na chanya zaidi ya kuviona.
Baki salama, usi-google kila kitu. Google isikufanye kuwa mpumbavu, google kwa malengo chanya na matokeo yatarajie kukujenga zaidi badala ya kukubomoa.
No comments