Mbowe na Lissu Wazuiliwa Kumuaga Mpaka, Waitaka Serikali Kutoa Kauli kwa nini Wazuiliwe
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitaka serikali itoe kauli ni kwa nini viongozi wakuuu wa chama hicho wamezuiliwa kuingia kumuaga Hayati Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa leo katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chadema leo katika vyombo vya habari imeeleza kuwa viongozi wakuu wa Chadema walifika katika uwanja wa Uhuru kwa ajili kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa Rais mstaafu Mkapa na kuzuiliwa kuingia.
Msafara wa viongozi wakuu ukiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ukiongozwa na makamu mwenyekiti, Tundu Lissu, Katibu Mkuu, John Mnyika, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Hashimu Juma Issa , Wajumbe wa kamati kuu , Ester Matiko, Mjumbe wa kamati kuu, Suzan Kiwanga pamoja na viongozi wengine kutoka makao makuu ya chama.
“Uamuzi huo ulizingatia ratiba ya shughuli ya msibba ya Hayati Rais Mstaafu Benjamini Mkapa ambayo Chadema kilipelekewa nakala ikionyesha tarehe, siku,muda,tukio na mhusika/wahusika. Ni ratiba iliyotumiwa uongozi wa juu wa chama kuahirisha na kusogeza mbele tarehe za vikao vya kitaifa ili kutoa heshima kwa kiongozi huu mstaafu wa nchi,”.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kwa mujibu wa ratiba leo Julai 28, 2020 waombolezaji walipaswa kuanza kuwasili uwanja wa uhuru kuanzia saaa 2:30 hadi saa 3:30 asubuhi kissha viongozi wa kitaifa walitakiwa kuwasili uwanjani hapo kuanzia saa 3:30 hadi saa 4:20 asubuhi.
Viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti Mbowe waliwasili geti la kuingia viongozi majira ya saa 3:00 asubuhi baada ya kuwasiliana na msajili wa vyama vya siasa na kupewa maelekezo ya itifaki ya kuingia uwanjani hapo kwa upande wa vyama vya siasa kabla ya kuzuiliwa na polisi waliokuwa wakilinda getini hapo wakiwataka wakajipange mstari.
Chadema imeeleza kuwa wakati viongozi wakuu wakizuiliwa getini hapo kulikuwa na magari ya viongozi wengine wa kiserikali na binafsi yalikuwa uwanjani hapo mengine yakiwashusha viongozi wa serikali , dini na wengine.
“Chadema inataka serikali itoe kauli kuhusu jambo hilo na kueleza sababu kwanini viongozi wakuu wa Chadema wamezuiliwa kuingia uwanja wa Uhuru, kushiriki shughuli za kitaifa, kutoa heshima za mwisho na kumuaga hayati Rais Mstaafu Mkapa,” taarifa hiyo ilieleza.
No comments