Waliokacha’ Kuchukua Hati za Ardhi Kuanza Kudaiwa kodi Julai Mosi
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema kuanzi Julai Mosi mwaka huu wananchi wote wasiochukua hati za ardhi huku maeneo yao yakiwa yamepimwa na michoro yake kuidhinishwa wataanza kudaiwa kodi ya pango la ardhi.
Hatua hiyo inafuatia Bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Sheria inayomtaka mwananchi aliyepimiwa ardhi na michoro kuidhinishwa kuchukua hati katika kipindi kisichozidi siku tisini na asipofanya hivyo ataanza kudaiwa kodi ya ardhi.
Akizungumza na wananchi mkoani Njombe jana wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya ardhi ya mkoa huo, Naibu Waziri Mabula alisema, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wamiliki wa ardhi kukwepa kuchukua hati za ardhi wakati taratibu zote zikiwa zimekamilika ikiwemo kuidhinishwa michoro na kuwekewa alama za mawe.
Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, kuanzia Julai Mosi mwaka huu muarobaini kwa wamiliki wasiotaka kuchukua hati za ardhi umefika kwa kuwa atakayeshindwa kuchukua hati atalazimika kudaiwa kodi kuanzia pale michoro yake ilipoidhinshwa.
‘’Kuanzia leo wamiliki wa ardhi hapa Njombe ambao wamepimiwa na michoro yao kuidhinishwa waende halmashauri za wilaya kurekebisha kumbukumbu zao na baada ya hapo asiyerekebisha baada ya siku tisini tunaanza kumdai’’ alisema Dkt Mabula
Aliwaagiza maafisa ardhi katika halmashauri za wilaya kuhakikisha kuanzia Julai mosi wanawapelekea hati ya madai wale wote waliopimiwa na michoro kuidhinishwa ili waanze kulipa kodi ya pango la ardhi.
Alisema, pamoja na wananchi wakiwemo wa Njombe kufurahia usogezwaji huduma za sekta ya ardhi karibu lakini ni lazima wawajibike kwa kulipa kodi ya ardhi na kupatiwa hati aliyoieleza kuwa inaongeza thamani ya ardhi sambamba na hati miliki yake kutumika katika shughuli za kiuchumi.
Aidha, amezitaka ofisi za ardhi katika halmashauri zote nchini kutoa elimu kwa wananachi wa maeneo yao kuhusiana na umuhimu wa kuchukua hati ili kujua takwa la kisheria hasa ikizingatiwa wengi wao wameshindwa kuchukua hati kwa sababu mbalimbali.
Akiegeukia uchukuaji hati za ardhi kwa mkoa wa Njombe, Dkt Mabula alisema mkoa huo una jumla ya hati 42,516 zilizoidhinishwa lakini kati ya hizo ni hati 11,246 tu ndizo wamiliki wake walijitokeza kuzichukua huku wamiliki 31,270 wakiwa hawajachukua.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri aliyemuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Njombe katika hafla ya uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa alisema, uanzishwaji ofisi za ardhi katika mkoa wa Njombe utaondoa changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika masuala ya ardhi kwenye mkoa huo.
Mkuu huyo wa wilaya ya Njombe alibainisha kuwa, mkoa wa Njombe ni maarufu kwa kilimo cha Miti, Chai, Mahindi, Viazi na Parachichi na baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo hawana hati miliki za ardhi hivyo uanzishwaji ofisi hizo unafungua milango kwa wamiliki wa mashamba kumilikishwa kwa haraka.
Naye Kamishna Msaidizi wa ardhi Wilson Ruge ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo, alisema uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa ni moja ya mikakati iliyopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya tano katika kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kubainisha kuwa tayari kazi kubwa imefanyika ikiwemo usambazaji vifaa na kuwataka wananchi kujitokeza kumilikishwa ardhi zao.
No comments