Header Ads

Header ADS

Urais Chadema: Lazaro Nyalandu Nae Atangaza Kuwania URAIS Kutekeleza Mambo 23 akiwa Rais




LAZARO Nyalandu, ametangaza kutoa nia ya kugombea Urais wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku akibainisha vipaumbele 25 atakavyovifanya ndani ya siku 100 endapo atapewa ridhaa na Watanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Nyalandu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (Chadema) kanda ya Kati ametangaza nia hiyo leo Jumapili tarehe 14 Juni 2020 mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo anakuwa wa nne kujitosa katika kinyang’anyiro hicho kinachohitimishwa kesho Jumatatu tarehe 15 Juni 2020 cha wanaotaka kutia nia kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa Chadema.

Wengine waliokwisha tia nia ni, Dk. Maryrose Majige, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara na Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Katika hotuba yake, Nyalandu amesema,  leo, “nimemwandikia burua Katibu Mkuu wa nikimjulisha kusudio langu la kutia nia katika kinyang’anyiro cha kuwa Mgombea Urais kupitia CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2020..”

“Nasimama mbele yenu na mbele ya umma wa Watanzania, huku moyo wangu ukiwa umejaa shauku kubwa nikitamani kuiona Tanzania, nchi tuipendayo kwa moyo wote inapata ustawi na kuendeleza matamanio, matarajiona ndotoza watu wake.”

“Katika kuwapatia maendeleo endevu likiwa ni Taifa linalosimamia uhuru na  haki za watu, utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari,na demokrasia ya kweliinayowapa wananchi mamlaka ya juu kuhusu mustakadhi na mwelekeo ya nchi kupitia chagua zilizo huru na za haki,” amesema Nyalandu

Amesema, “Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliamini katika ulazima wa kuwaunganisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili waishi katika udugu, umoja, usawa, na mshikamano katika Taifa lililo huru na lenye amani, na kuifanya Tanzania kuwa kitivo cha amani na shauku ya wengi barani Afrika na ulimwenguni pote.”

Nyalandu amesema, wakati Tanganyika inapata uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza mwaka 1961, Baba wa Taifa alisema ‘Tuwashe Mwenge, na tukauwe Kilimanjaro, ili uangaze ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.

Palipo na chuki kukawe na furaha, palipo na giza kukawe na nuru”.  Hii ndio asili ya Tanzania na hii ndio inayopaswa kuwa daima ya Tanzania.

“Watanzania wana matamanio na ndoto za maendeleo, vijana wao wana vipaji lukuki na wamejawa na uthubutu katika kutafuta maisha na kujiendeleza, huku  wakiamini katika ahadi ya ukuu wa Taifa lao, na uwepo wa amani tuliyo nayo tangu uhuru,” amesema

“Watanzania wanaamini katika kujenga jamii ya watu huru na wenye ushujaa, huku wakizifuata fursa za kujiendeleza kiuchumi na  kukabiliana na changamoto za maisha yao.”

1. Tutarekebisha sheria ya ardhi kuruhusu wananchi kumiliki ardhi bila ukomo (Freehold lease) na kuwapimia wananchi maeneo ya ardhi kote nchini ili kurasimisha utajiri wa watanzania wote kupitia ardhi tunayoimiliki.

Hatua hii italeta ukomo kwa serikali kuu kupitia Rais wa nchi kuwa mmiliki wa ardhi ya watanzania, jambo linalowafanya wananchi wote kuwa wapangaji katika nchi yao wenyewe.

Aidha, hati zote za umiliki ardhi zitakuwa na thamani katika mabenki na amani za kifedha na kumwezesha mwananchi wa kawaidi kukopesheka na kuwa na mali isiyohamishika.

2. Kwa kuwa wajibu wa kiongozi mkuu  wa nchi kuhakisha watu wake wanao ulinzi na usalama, na kwamba wanaweze kumudu kujikimu kimaisha, nitahakikisha tunafanya kila linalowezekana kuongeza ajira kwa vijana na watanzania kwa ujumla, huku sekta binafsi ikiwa kipaumbele kama sekta kiongozi kwenye upatikanaji wa ajira nchini.

3. Tutaanza mara moja kuipitia upya rasimu ya Katiba Mpya ya Tanzania, kwa kuanzia na rasimu ya Jaji Warioba.

4. Tutairekebisha sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA ili iwe taasisi inayojitegemea na isiyolalamikiwa kuhusu uendeshaji wake au kuingiliwa kisiasa.

Hatua hii itahusisha pia kupunguza utitiri wa kodi, na kuwa na mfumo wa kodi ulio wazi na wa kueleweka kwa lengo la kupanua wigo wa walipa kodi na kuongeza mapato ya serikali kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

5. Tutaweka sera mpya itakayosimama sekta ya kilimo na uvuvi, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa pembejeo, uhakika wa masoko, kilimo cha umwagiliaji, na kuboresha shughuli za uvuvi katika maziwa na bahari kuu kwa lengo la kuwanufaisha wavuvi wadogo wadogo na kuthibiti wizi wa raslimali zetu katika bahari kuu.

6. Tutaipitia upya na kuirekebisha sheria ya Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB) kwa lengo la kuwaondolea wanafunzi faini za malimbikizo, na kuondoa ulazima wa kuanza kurejesha mkopo kabla ya mwanafunzi husika kupata ajira.

Aidha, tutarekebisha na kupunguza kiwango cha asilimia ya marejesho anayopaswa kuyafanya mwanafunzi ili kumpa unafuu wa kumudu maisha kwa kuongeza muda wa malipo.

7. Tutaweka sera mpya kuongoza sekta ya afya na kuinua kiwango cha utoaji huduma ya kitabibu nchini. Tupitia upya mpango wa Taifa wa upatikanaji wa maji safi na salama vijijini, na mijini.

8. Tutatunga sera mpya na wezeshi ili kufufua sekta ya mafuta na gesi na kuruhusu uwekezaji wa mitaji mikubwa-FDIs, na kuruhusu serikali kuhodhi asilimia ya hisa kwa niaba ya wananchi wa Tanzania.

Hatua hii itawezesha kuanzishwa Liquidified Natural Gas Plant-LNG katika ukanda wa Mtwara na kuifanya Tanzania kuwa nchi kiongozi katika uzalishaji wa gesi asilia na mafuta katika ukanda wa Afrika mashariki na SADC.

Hatua hii pia itahusisha kuihusha sekta ya madini iwafaidishe wachimbaji wadogo wadogo na kuruhusu uingizwaji wa mitaji mikubwa katika sekta hii, ikiwepo dhahabu, tanzanite, graphite, na urani.

9. Tutaimarisha mahusiano ya kikanda kwa kuidhinisha itifaki ya Afrika Mashariki kuhusu ‘Free Movement of persons, goods and services”, na ushirikiano wa ulinzi na usalama-Mutual Defense Pact, na kuongeza ushirikiano wa mafunzo katika kuimarisha Majeshi yetu ukanda wa Afrika Mashariki.

10. Tutarejea upya makubaliano ya biashara kati ya ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya-EPA, na kuidhinisha ushirikiano wenye maslahi kwa wafanyabiashara wa Tanzania hasa kwa fursa ya kuuza bidhaa zetu bila kodi katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

11. Tutaingia mara moja kwenye “Bilateral Negotiation” kwa mkataba mpya wa kibiashara kati ya Tanzania na United Kingdom, kwa kuwa UK sio tena mwanachama wa EU.

12. Tutaongeza idadi ya nchi ambazo Watanzania wanaweza kusafiri bila ulazima wa kuwa na visa (visa free) kupitia makubalino baina ya nchi na nchi na kwa kuzingatia utaratibu wa kidiplomasia wa “resprocity”.

Hatua hii itaongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini, na itawawezesha Watanzania kusafiri kwa shughuli za kibiashara au vinginevyo katika mataifa mengi na kuiletea heshima pasipoti ya Tanzania.

13. Tutaweka sera ya kudumu ya kuimarisha utayari wa Majeshi ya ulinzi na usalama katika kuilinda chi yetu dhidi ya maadui na kulifanya Jeshi la Wanachi wa Tanzania (JWTZ) liendelee kuwa la kisasa Zaidi.

14. Tutatunga sheria kuruhusu ‘Dual Nationality”, ambako Mtanzania yeyote anayekubali uraia wa nchi nyingine hawezi kunyang’anywa haki ya Utanzania wake.

Hatua hii itawasaidia Watanzania waliopo nchi za nje kuweza kuendelea kuwekeza kiuchumi katika nchi yetu na kuongeza pato la Taifa huku tukiendelea kuhakikisha kila mtanzania anabaki kuwa raia wa Tanzania.

15. Tutaruhusu shughuli zote za kisiasa kutoka kwa vyama vya upinzani na wanaharati katika kukusanyika na kuwa na uhuru wa kuikosoa serikali.

Hatua hii itaongeza wigo wa demokrasia na kuvipa vyama vya upinzani nafasi ya kujiandaa kisera na kimuundo kwa ajili ya uchaguzi unaofuata.

16. Tutarekebisha sheria ya Habari ili kuruhusu uhuru kamili wa vyombo vya habari, na uhuru kamili wa wanahabari (reporters), ikiwa ni pamoja na  haki ya kulinda vyanzo vya habari kama nguzo muhimu kwa upatikanaji wa habari.

17. Tutarejesha Bunge live.

18. Tutaendeleza uhuru uliopo wa kuabudu, na kuweka zuio la kudumu ili kusiwe na tozo za kodi kwa mashirika ya dini, na taasisi za kiraia ili ziendelee kushiriki kama wadau wa maendeleo nchini.

19. Tutaruhuru vyombo vya usafirishaji vyote (Mabasi, malori, meli, ndege, nk) kuwa huru kufanya safari zao usiku na mchana. Hatua hii itaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

20. Tutaboresha sekta ya elimu nchini, na kupitia upya haki na stahiki za walimu, kuanzia kupandishwa madaraja na mishahara, haki ya kupata uhamisho kujiunga na familia kwa wale waliioa au kuolewa, na malimbikizo ya mishahara kwa ngazi zote za elimu ya umma nchini.

21. Tutaimarisha uhifadhi, na kuongeza utalii nchini kwa kurekebisha mifumo ya kodi, tozo, mitaji, rasilimali watu, masoko, na uendeshaji wa sekta hii.

22. Tutaimarisha ushiriki wa Tanzania katika jitihada za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi na athari zinazotarajiwa kulikumba eneo la Ikweta, ambako nchi yetu ipo.

23. Tutaimarisha ushiriki wa Tanzania katika Taasisi ya Kimataifa na kuimarisha mahusiano na ushirikiano wa kikanda, na kimataifa, na kuongeza nguvu ya diplomasia ya Tanzania katika Nyanja za kiuchumi, kisiasi, kiulinzi, na kijamii.

“Taifa letu linahitaji mabadiliko, na saa ya ukombozi imefika. Ungana nami (kupitia tovuti yangu lazaronyalandu.com) katika safari ya kuleta tumaini jipya kwa Watanzania. Sote tunaowajibu kwa nchi yetu,” amesema Nyalandu.

No comments

Powered by Blogger.