Umoja wa Ulaya wagawanyika kuhusu kufungua mipaka yake kwa mataifa yalioathirika zaidi na corona
Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yamegawanyika kuhusu iwapo yaendelee kuzuia wasafiri kutoka mataifa yalioathirika zaidi na janga la virusi vya corona kuingia katika nchi hizo kama vile Marekani wakati yatakapofungua mipaka yao Julai mosi.
Hii leo, wanadiplomasia bado walikuwa katika mazungumzo ya siku nzima kuweka mikakati ya kufungua mipaka hiyo huku baadhi ya mataifa yakiwa na hofu kuhusu uhakika wa takwimu kutoka China kuhusu virusi vya corona.
Lakini huku chumi za mataifa hayo zikikumbwa na misukosuko kutokana na janga hilo, Ugiriki, Uhispania, Ufaransa na mataifa mengine yenye kiwango cha juu cha Utalii yanatarajia kutumia fursa ya majira ya kiangazi na kufungua mipaka yake kwa wageni.
Usafiri usiokuwa wa lazima ulipigwa marufuku katika Umoja huo tangu kati mwa mwezi Machi na vikwazo hivyo vinatarajiwa kuondolewa pole pole kuanzia Julai Mosi huku janga hilo likipungua angalau barani Ulaya.
No comments