"Mwizi wa Tecno Utapigwa Kama Mwizi wa Dreamliner" - Paul Makonda
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amewataka wazazi kuhakikishe wanawachunga watoto wao kwa kuwa, hakuna kibaka atakayesalimika kutokana na msako maalum ulioanzishwa na Polisi wa kuwasaka vibaka wote wanaopora na kuiba, kwani watapigwa kipigo cha Kimataifa kama wezi wa Dreamliner.
Makonda amesema kuwa oparesheni hiyo kabambe imeanza Juni 4, 2020, ambapo amemuelekeza Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, kuhakikisha wanawashughulikia ipasavyo baadhi ya vijana hao kwani wanarudisha nyuma maendeleo ya watu.
"Natoa rai kwa wananchi kila mmoja achunge mtoto wake, nimetoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kugonga kikamilifu na adhabu utakayoipata haina tofauti uibe tecno au pochi haina kitu tutakuhesabu kama mwizi wa Dreamliner, kipigo chako ni cha Kimataifa, wale mnaotaka kuonja nafasi ya ukibaka kama ni nzuri onjeni na tusilaumiane, hakuna mtu yuko tayari kuharibiwa kazi yake kwenye hiki kipindi cha mwisho tunafunga mahesabu"amesema Makonda.
Makonda ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo Wilaya ya Temeke, iliyoenda sambamba na uzinduzi wa majengo ya madarasa 124, matundu 124 ya vyoo na Madawati 7,179, kwenye Shule ya Sekondari Mbagala na Shule nyingine 16.
No comments