Header Ads

Header ADS

Mbelgiji Yanga Ataka Molinga Apewe Mkataba




INAELEZWA kuwa Klabu ya Yanga inaweza kumpa mkataba mpya mshambuliaji wao, David Molinga baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Luc Eymael kuonyesha nia ya kutaka kuwa na nyota huyo kwa mwaka mmoja zaidi.

 

Hayo yameibuka juzi katika kikao ambacho viongozi walikaa na kocha Eymael wakati wanajadili sababu zilizomfanya Molinga agomee kusafiri na timu juzi Jumatano kuelekea Shinyanga kuvaana na Mwadui FC.



Chanzo makini kutoka ndani ya uongozi wa Yanga kililiambia Championi Jumamosi kuwa, Eymael aliuambia uongozi kwamba anahitaji kuwa na Molinga kwa msimu mmoja zaidi kwa kuwa anaamini nyota huyo anaweza kuwa msaada msimu ujao katika eneo la ushambuliaji kama akifanikiwa kuwasajili nyota wazuri katika eneo la kiungo ambao ameagiza viongozi wawasajili.

 

“Tulikuwa na kikao na kocha juzi, mara baada ya yeye kuwasili nchini akitokea Ubelgiji, tulizungumza mambo mengi ikiwemo sababu za Molinga kugoma kuondoka na timu, baada ya kumaliza suala la Molinga, ndipo aliomba mchezaji huyo aongezewe mkataba akiamini anaweza akafanya vizuri msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.

 

Championi lilimtafuta Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz lakini simu yake haikupokelewa.Baada ya kumkosa Nugaz, tulimsaka Mkurugenzi wa Mashindano na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Thabit Kandoro ambapo alisema: “Tulikuwa na kikao na mwalimu ndiyo na tulizungumza mambo mengi ikiwemo ishu ya Molinga kugoma kusafiri na timu, ila hayo ya kumuongezea mkataba siyajui.”

Stori: Issa Liponda, Dar es Salaam




No comments

Powered by Blogger.