Mauaji ya wanawake Afrika Kusini yawasha moto wa kampeni mitandaoni
Wimbi kubwa la mauaji ya wanawake nchini Afrika Kusini katika wiki za hivi karibuni, yakiwemo mauaji ya mwanammke mmoja mwenye ujauzito mpevu aliyedungwa visi na baadaye kutundikwa kwenye mti, kumeongeza udharura wa kuchukuliwa hatua kali na polisi za kupambana na unyanyasaji wa wanawake. Makundi ya kutetea haki za wanawake nchini Afrika Kusini yamelaani vikali wimbi hilo.
Siku mbili baada ya Afrika Kusini kumaliza wiki tisa za marufuku ya uuzaji wa pombe, Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo amelihusisha wimbi ipya la ubakaji na mauaji ya wanawake na suala la kuondolewa marufuku iliyokuwa imewekwa nchini humo kufuatia janga la corona. Ramaphosa amesema, hii ni wiki ya aibu kwa Afrika Kusini.
Ametaja majina ya wanawake watatu ambao mauaji yao yamekuwa ajenda kuu ya kampeni kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akiwemo mwanamke aliyekuwa amekaribia kujifungua aliyejulikana kwa jina la Tshegofatso Pule, 28 ambaye maiti yake imepatikana ikiwa imetundukwa juu ya mti. Mwanamke mwengine ni Naledi Phangindawo aliyeuawa kwa kuchomwa visu. Mwanamke wa tatu aliyetajwa kwa jina na Rais Ramaphosa ni Sanele Mfaba ambaye maiti yake iliokotwa pembeni mwa mti katika mji wa Soweto.
Wanaharakati wa kupigania haki za wanawake nchini Afrika Kusini wamepongeza hatua hiyo ya Rais Ramaphosa ya kulipa uzito suala la kupambana na ukatili na unyanyasaji wanaofanyiwa wanawake hata hivyo wamesema, wimbi la mauaji hayo halitokani tu na kuondolewa marufuku ya corona bali kimsingi katika historia ya Afrika Kusini kuna idadi kubwa ya kesi za kudhalilishwa na kunyanyaswa wanawake majumbani.
Idadi ya wanawake wa Afrika Kusini wanaouliwa na waume, wanaume na watu wao wa karibu ni mara tano zaidi ikilinganishwa na wastani wa mauaji hayo duniani. Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, (WHO).
No comments