Gambia Yataka Uchunguzi wa Mauaji ya Mtoto wa Mwana Diplomasia Nchini Marekani Yaliyotokea Wakati wa Maandamano
Serikali ya Gambia imeitaka Marekani ianzishe uchunguzi mara moja wa mauaji ya mtoto wa kiume wa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa nchi hiyo ya Kiafrika katika jiji la Atlanta, jimboni Georgia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Gambia imeutaka ubalozi wa nchi hiyo mjini Washington kuzishinikiza mamlaka husika nchini Marekani kuanzisha uchunguzi huru, wa wazi na wenye itibari wa mauaji ya Momodou Lamin Sisay, mwana wa kiume wa Lare Sisay, mwanadiplomasia wa Gambia katika Umoja wa Mataifa.
Inaarifiwa kuwa, mtoto huyo wa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Gambia aliuawa Ijumaa iliyopita kwa kupigwa risasi na polisi wa Atlanta waliokuwa wakikabiliana na maandamano yanayoendelea kushuhudiwa katika pembe mbalimbali za Mmarekani ya kulaani mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd.
Tayari maafisa sita wa jiji la Atlanta wamekamatwa wakikabiliwa na mashitaka ya kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya wananchi.
Hadi sasa watu 13 wameuawa kote Marekani katika maandamano ya kulaani mauaji ya George Floyd huku hali ikiendelea kuwa mbaya. Utawala wa Marekani umelaaniwa kote duniani kwa kutumia mabavu kuwakandamiza waandamanaji wanaotetea haki.
No comments